Serikali yaziita ‘startups’ kuchangamkia mkopo wa Sh5 bilioni
- Maombi yote yatapokelewa kwa njia ya kidijitali kupitia mfumo wa jamiihunt.mawasiliano.go.tz hadi kufikia Mei 30, 2027.
Dar es Salaam. Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICTC), imefungua rasmi dirisha la maombi ya mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kuwawezesha vijana na kampuni changa za Tehama nchini.
Mikopo hiyo iiyopewa jina la Startups Wezesha Fund ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia ya Sh200 bilioni kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana na wamiliki wa kampuni changa nchini ambapo tayari Sh5 bilioni zimeshatolewa kufanikisha programu hiyo.
Taarifa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inabainisha kuwa mpango huo unalenga kupunguza changamotoo ya aira nchini.
“Kupitia mpango huu, Serikali inalenga kuongeza ajira kwa vijana, kukuza ujasiriamali na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa,” imesema taarifa hiyo.
Maombi yote yatapokelewa kwa njia ya kidijitali kupitia mfumo wa jamiihunt.mawasiliano.go.tz hadi kufikia Mei 30, 2027.
Sifa za Waombaji na Kampuni
Ili kupata mkopo huo Wizara ya Mawasiliano imeanisha sifa 12 ambazo waombaji binafsi wanatakiwa kuwa navyo ikiwemo kuwa raia wa Tanzania mwenye umri kati ya miaka 18 hadi 35
Vigezo vingine ni kuwa na kitambulisho cha Taifa (NIDA) au namba ya NIDA, pamoja na anwani ya makazi iliyosajiliwa kwenye Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA).
Kwa upande wa kampuni, inapaswa iwe imesajiliwa kisheria nchini na kutambulika na Tume ya TEHAMA (ICTC). Kwa kampuni ambazo hazijasajiliwa, zinatakiwa kujisajili kupitia mfumo wa usajili mtandaoni tanzaniastartups.ictc.go.tz/register.
Aidha, kigezo kingine cha msingi, waanzilishi wanapaswa wasiwe waajiriwa wa Serikali au sekta binafsi, na kampuni inapaswa iwe na waajiriwa wasiopungua wawili, lakini pia kampuni iwe tayari ina biashara yenye wateja wa awali na mapato ya mwaka yasiyozidi Sh500 milioni.
Kwa mikopo ya kati au mikubwa, kampuni inatakiwa kuwa na uendeshaji usiopungua miaka mitatu, wakati kampuni ndogo zisizokuwa na taarifa za kimahesabu za miaka mitatu zitapaswa kuwa na mdhamini.
Nyaraka Zinazohitajika Wakati wa Kuomba
Taarifa hiyo inasisitiza kuwa, waombaji wote wanatakiwa kuwasilisha nyaraka muhimu kupitia mfumo wa maombi, kama vile barua ya maombi na barua ya utambulisho kutoka Ofisi ya Serikali ya Mtaa, nakala za NIDA, Cheti cha BRELA, namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN), hati safi ya kodi na Leseni ya Biashara.
Waombai wanapaswa pia kuambatanisha andiko la biashara au la Mradi lisilozidi kurasa tano linaloonyesha uendelevu na mchango kwa uchumi wa kidijitali.
Kwa upande mwingine mwombaji anapaswa kuwasilisha Picha ya hivi karibuni aghalabu iliyopigwa ndani ya miezi 3, taarifa za fedha zilizokaguliwa yaani ‘Audited financial reports’ za miaka mitatu endapo zipo pamoja na makadirio ya mtiririko wa fedha yaani.
Nyaraka nyingine ni pamoja na hati ya udhamini kutoka Bodi ya Kampuni, Azimio la Bodi, Mkataba na Kanuni za Kampuni (MEMARTS), na Katiba ya kikundi, nyaraka za upekuzi wa kampuni kutoka BRELA na taarifa za akaunti za benki.
Wizara imefafanua kuwa tathmini ya maombi yote itakuwa ikifanyika kila baada ya miezi mitatu, na majina ya wanufaika yalatangazwa mara baada ya kila tathmini kukamilika, huku ikisisitiza kuwa maombi ya mkono hayatapokelewa.