Ubalozi wa Japan watangaza ufadhili wa masomo vyuo vitano
- Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Tokyo, Tsukuba, APU, Tohoku na Nagoya vilivyopo nchini Japan.
Dar es Salaam. Ubalozi wa Tanzania nchini Japan umetangaza fursa za masomo katika vyuo vikuu vitano vya Japan, hatua inayofungua milango kwa Watanzania wanaotaka kuendeleza elimu ya juu kimataifa
Taarifa ya ubalozi huo iliyochapishwa katika kurasa Instagram Septemba 8, 2026 inasema fursa hizo za masomo zilizotangazwa ni kwa ajili ya watanzania wanaotaka kuendeleza masomo kwa ngazi ya shahada ya kwanza, uzamili hadi uzamivu.Â
Kwa mujibu wa ubalozi wa Japan fursa hizo za masomo zinapatikana kupitia vyuo vitano ikiwemo, Chuo Kikuu cha Tokyo, Chuo Kikuu cha Tsukuba, Ritsumeikan Asia Pacific University (APU), Chuo Kikuu cha Tohoku na Chuo Kikuu cha Nagoya
Chuo Kikuu cha Tokyo
Chuo Kikuu cha Tokyo kimetangaza programu mbili, zikiwemo International Program in Agricultural Development Studies (IPADS), inayohusu kilimo na maendeleo, na programu ya fani mseto za uhandisi (IME).
Programu hiyo inatoa nafasi za uzamili na uzamivu katika fani za uhandisi, ikiwemo umeme, mitambo, anga, kemia na bioengineering. Maombi ya IPADS yatafungwa Oktoba 18, 2026, huku usajili wa IME ukitarajiwa kufungwa Oktoba 14, 2026.
Chuo Kikuu cha Tsukuba
Chuo Kikuu cha Tsukuba kinatoa programu ya uzamili ya Uchumi na Sera za Umma (PEPP), inayofundishwa kwa Kiingereza, huku wanafunzi wakihimizwa kuangalia ufadhili kupitia World Bank/JJ-WBGSP na ADB-JSP.Â
Kwa waombaji Watanzania, Ubalozi wa Japan umeshauri kuzingatia zaidi ufadhili wa World Bank/JJ-WBGSP, huku maombi ya programu hiyo yakiwa yamefunguliwa Oktoba 1 na kufungwa Novemba 15, 2026.
Ritsumeikan Asia Pacific University (APU)
APU imetangaza programu mbalimbali za shahada ya kwanza zinazofundishwa kwa Kiingereza, pamoja na ufadhili wa ada (APU Tuition Reduction Scholarship) unaoweza kupunguza ada kwa asilimia 30, 50, 65, 80 au 100.Â
Ufadhili huzingatia nyaraka za mwombaji, hali yake ya kifedha na mahojiano yaliyorekodiwa, huku tarehe za mwisho za maombi zikitegemea msimu wa kuanza masomo mwaka 2027.
Chuo Kikuu cha Tohoku
Chuo Kikuu cha Tohoku kinatoa International Graduate Program for Advanced Science (IGPAS), inayolenga wanafunzi wanaotaka kujiunga na masomo ya uzamili na uzamivu katika sayansi.Â
Dirisha la maombi ya awali limefunguliwa Oktoba 1 hadi Novemba 15, 2026, huku maombi rasmi yakipokelewa Novemba 1 hadi 30, 2026; miongoni mwa masharti muhimu ni kupata ridhaa ya msimamizi anayetarajiwa kabla ya kuwasilisha maombi.
Chuo Kikuu cha Nagoya
Chuo Kikuu cha Nagoya kinatoa programu za kimataifa za G30 zinazofundishwa kwa Kiingereza na kutoa fursa kwa wanafunzi wa kimataifa kujiunga na shahada ya kwanza.Â
Maombi yanatarajiwa kufunguliwa Novemba 2, 2026, hivyo waombaji wanashauriwa kuandaa nyaraka zinazohitajika mapema na kufuata masharti ya programu wanayolenga.
Jinsi ya kutuma maombi
Waombaji wanatakiwa kutuma maombi moja kwa moja kupitia mifumo rasmi ya vyuo husika badala ya kuyawasilisha Ubalozini. Maombi ya Chuo Kikuu cha Tokyo yanafanyika kupitia mifumo ya IPADS na IME, Tsukuba kupitia PEPP, APU kupitia mfumo wake wa udahili na ufadhili, Tohoku kupitia IGPAS na Nagoya kupitia G30.
Waombaji wanashauriwa kusoma kwa makini vigezo vya udahili, mahitaji ya nyaraka, masharti ya ufadhili na tarehe za mwisho za kila programu kabla ya kuwasilisha maombi, kwa kuwa sifa na taratibu hutofautiana kati ya vyuo na programu.