Urasa Sarakikya ateuliwa Kaimu Mkurugenzi TSL
- Uteuzi huo unakuja kufuatia kuondoka kwa George Shumbusho aliyekuwa akiongoza kampuni hiyo kwa miaka mitatu.
Dar es Salaam. Kampuni ya Tanzania Securities Limited (TSL) imemteua Urasa Sarakikya kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo kufuatia kuondoka kwa George Shumbusho aliyeongoza kampuni hiyo kwa miaka mitatu.
Taarifa ya Justin Masawe, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TSL iliyochapishwa Oktoba 9, 2026 imebainisha kuwa uongozi wa Shumbusho ulikoma wiki moja iliyopita.
“Siku yake ya mwisho kazini (George Shumbusho) ilikuwa Oktoba 2, 2026…Bodi inamshukuru kwa utumishi wake na inamtakia mafanikio mema katika shughuli zake za baadaye,” imesema taarifa ya Masawe.
TSL ni kampuni inayojishughulisha na udalali wa dhamana za kifedha, ushauri wa uwekezaji na uendeshaji wa mifuko ya uwekezaji wa pamoja.
Hivyo, katika kipindi atakachokuwa akiiongoza kampuni hiyo, Sarakikya ana jukumu la kusimamia shughuli za kampuni, kuhakikisha huduma kwa wateja na wawekezaji zinaendelea kama kawaida wakati bodi ikiendelea na mchakato wa kumpata Mkurugenzi Mtendaji wa kudumu.
Sarakikya, ambaye ameteuliwa kukaimu nafasi hiyo kuanzia Oktoba 3, 2026, amekuwa Mkuu wa Utafiti na Ushauri wa TSL tangu Agosti 2025 akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika sekta ya benki na huduma za kifedha.
Katika kipindi chake cha uongozi, Shumbusho alisimamia mabadiliko ya kidijitali ya kampuni hiyo pamoja na uzinduzi wa mifuko miwili ya uwekezaji wa pamoja, Kesho Tulivu Fund na Imara Fund.
Bodi ya wakurugenzi ya TSL imesema ina imani na uwezo wa Sarakikya kuiongoza kampuni hiyo katika kipindi cha mpito, huku ikiendelea na majukumu yake ya kuongoza kitengo cha Utafiti na Ushauri.
Boss wa kudumu kupatikana 2027
Kwa sasa kinachosubiliwa ni mchakato wa kumpata bosi mpya wa kudumu atakeyeiongoza kampuni hiyo wakati Sarakikya akitekeleza majukumu yake ya uongozi wa muda.
Kwa mujibu wa TSL, bodi imeanza mchakato rasmi wa kumpata Mkurugenzi Mtendaji wa kudumu, unaotarajiwa kukamilika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2027.
Kampuni hiyo imeeleza kuwa itatoa taarifa nyingine baada ya kuthibitisha uteuzi wa kiongozi huyo wa kudumu.