Bei mpya za mafuta hizi hapa, petroli yapaa kwa Sh261, dizeli Sh209
- Sh10,000 sasa itanunua lita 2.46 za petroli Dar es Salaam, kutoka lita 2.63 mwezi uliopita.
Dar es Salaam. Watumiaji wa vyombo vya moto nchini Tanzania huenda wakauanza mwezi Oktoba kwa maumivu baada ya kupanda kwa bei ya mafuta petroli na dizeli licha ya kushuka kwa mwezi uliopita.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) leo Oktoba 7, 2026 imesema bei ya rejareja ya petroli imepanda kwa Sh261 na Sh209 dizeli.
Kwa viwango hivyo vipya, lita moja ya petroli inayopitia Bandari ya Dar es Salaam itauzwa kwa Sh4,057 kutoka Sh3,796 mwezi Septemba huku huku dizeli ikipanda hadi Sh4,086 kutoka Sh3,877.
Mafuta ya taa nayo yanauzwa kwa Sh4,067 kutoka Sh3,713 mwezi uliopita.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa kiwango hicho cha bei ya mafuta Oktoba ndiyo cha juu zaidi kurekodiwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Kuanzia Januari 2023 hadi Septemba 2026 kiwango hicho cha bei ya petroli, na dizeli kilikuwa ikipanda na kushuka kwa wastani wa bei ya Sh2,819 hadi Sh3,295.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura, ongezeko hilo la bei ya mafuta limechagizwa na mgogoro wa kisiasa katika Mashariki ya Kati, ulioibuka tena mwezi Septemba 2026 na hivyo kuendelea kuathiri uzalishaji, upatikanaji na usafirishaji wa mafuta duniani.
Watumiaji wa vyombo vya moto walianza kuionja shubiri ya kupaa kwa bei ya mafuta mwezi Machi, 2026 baada ya vita vya Marekani, Israel na Iran.
Tangu wakati huo bei ya mafuta duniani ilipaa suala lilosababisa maumivu kwa watumiaji wa vyombo vya moto na wananchi wa kawaida baada ya bei ya baadhi ya bidhaa muhimu pia kuongezeka.
Hata hivyo, bei hii imepanda baada ya kushuka kwa miezi mitatu mfululizo jambo ambalo linatarajia kuanza kuleta maumivu kwa wamiliki na watumiaji wa vyombo vya moto ikiwemo wasafiri.
Sanjari na kupanda kwa bei hizo, Ewura imewataka wafanyabiashara kuuza mafuta kulingana na bei elekezi huku hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yeyote atakayekiuka agizo hilo.
Kwa bei mpya za Dar es Salaam, Sh10,000 sasa itanunua lita 2.46 za petroli, ikilinganishwa na lita 2.63 zilizopatikana mwezi Septemba.
Kwa dizeli, kiasi hicho kitamwezesha mtumiaji kupata lita 2.44 kutoka lita 2.57 zilizopatikana kwa Sh10,000 mwezi uliopita.