Rais Samia: Bwawa la Julius Nyerere, si ‘tembo mweupe’
- Kauli hiyo imekuja kufuatia minong’ono kutoka kwa baadhi ya watu.
- Amesema mradi huu una manufaa makubwa kwa Taifa.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), akisisitiza kuwa mradi huo sio ‘tembo mweupe’.
Kiongozi huyo ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo kwa ukosoaji mkubwa kutoka kwa wanasiasa na wanamitandao ikiwa ni takriban miaka saba tangu kuanza kwa utekelezaji wake.
Wakosoaji hao walikosoa changamoto ya kukatika katika kwa umeme kunakozorotesha baadhi ya shughuli za kiuchumi za Wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
“Wakati tunasema bwawa limekamilika, kuna watu walikuwa wanasema limekamilika lakini ni ‘white elephant’ yaani ni lijitembo jeupe limejilaza kwamba hakuna matumizi, hakuna njia kuu za kusafirishia umeme, sasa ujenzi wa njia kuu unaendelea kwa kasi kubwa na mradi huu ni mradi wa manufaa makubwa kwa Taifa na sio ‘white elephant’,” amesema Rais Samia.
Mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 umezinduliwa leo Agosti 22, 2026 Rufiji, mkoani Pwani ukigharimu takribani Dola za Marekani bilioni 2.9, zaidi ya Sh7.79 trilioni.
Kwa mujibu wa Rais, aliyekuwa akizungumza wakati wa uzinduzi huo amesema, ongezeko la uzalishaji wa umeme limesaidia kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, hali iliyokuwa ikiathiri shughuli za viwandani, hospitalini na majumbani.
Amesema upatikanaji wa umeme wa uhakika pia utafungua fursa zaidi za biashara, ajira na uwekezaji, hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa zitakazotokana na uwekezaji huo.

Watanzania watakiwa kulinda mradi
Rais Samia pia ametoa wito kwa Watanzania kushirikiana katika kulinda miundombinu ya JNHPP na miradi mingine ya kitaifa inayojengwa kwa gharama kubwa.
Ameziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama katika mikoa na wilaya, Wizara ya Nishati, Wizara ya Maji, Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu kuratibu na kusimamia kwa karibu juhudi za kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji vinavyolisha Bwawa la Julius Nyerere.
“Tunzeni kidumu,” amesema Rais Samia, akiwataka Watanzania kutambua kuwa mradi huo ni mali ya Taifa na unapaswa kulindwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Pia ameitaka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na wataalamu wanaosimamia kituo hicho kuhakikisha mitambo inatunzwa ipasavyo ili iendelee kufanya kazi kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Awali akizungumza Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange, amesema kituo hicho kilianza kuzalisha umeme Februari 2024 baada ya Tanesco kupokea mtambo wa kwanza kutoka kwa mkandarasi.
Kwa mujibu wa Twange, mwaka 2025 JNHPP ilichangia asilimia 43.5 ya umeme wote ulioingizwa kwenye Gridi ya Taifa, huku mwaka 2026 kituo hicho kikichangia takribani nusu ya umeme wote ulioingizwa kwenye gridi.
Twange pia amesema asilimia 95 ya wafanyakazi walioshiriki katika ujenzi wa JNHPP walikuwa Watanzania, jambo linaloonyesha mchango wa mradi huo katika kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani.