Hayati Magufuli, Rais Samia walivyoichonga historia ya Bwawa la Mwalimu Nyerere

August 22, 2026 4:20 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Historia hii imenza enzi za Ukoloni kabla Tanzania haijapata uhuru.
  • Imegharimu takribani Sh7.79 trilioni kutimia.

Dar es Salaam.Macho na masikio ya Watanzania hii leo yapo Rufiji mkoani Pwani ambapo Serikali inazindua mradi wa kihistoria wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) uliogharimu zaidi ya Sh7.7.

Lakini nyuma ya shangwe na shamra shamra za uzinduzi wa mradi huu kuna safari ndefu iliyochukua zaidi ya karne moja, ikipita katika nyakati tofauti na chini ya viongozi watano wa Tanzania ikipata msukumo zaidi wakati wa Hayati John Magufuli na Rais Samia Suluhu Hassan.

Ili kuelewa vizuri safari hii, hebu turudi nyuma zaidi ya miaka 100, hadi mwaka 1903, wakati wazo la kutumia Mto Rufiji kuzalisha umeme lilipoanza. 

Fikiria eneo lilipojengwa Bwawa la Mwalimu Nyerere tunaloliona hivi sasa kupitia mitandao ya kijamii na televisheni lilikuwa pori kubwa lenye miti iliyoshona pande zote.

Hakuna barabara za lami wala magari ya kisasa yaliyoweza kufika huko kilichokuwepo ni ukimya mzito, sauti za wanyama wa mwituni na maji ya Mto Rufiji yaliyokuwa yakitiririka kwa nguvu na kugonga miamba kwa kishindo kikubwa.

Kwa mtu wa kawaida, eneo hilo lingeonekana kuwa la hatari lisoloweza kufikika lakini sivyo ilivyokuwa kwa Mhandisi Mjerumani aliyejulikana kwa jina la Stiegler.

Wakati wengine walipoona maporomoko, miamba na maji yakipotelea mtoni, Stiegler aliona zaidi ya mandhari. Aliona nguvu, umeme na uwezekano wa kugeuza nguvu ya Mto Rufiji kuwa chanzo cha maendeleo.

Hakuwa akijua kwamba wazo hilo dogo, lililozaliwa katikati ya pori, lingekuja kuwa moja ya ndoto ndefu zaidi katika historia ya Tanzania.

Mwaka 1904, wazo likawa mpango, mwaka 1905, mpango ukaidhinishwa na Bundestag, Bunge la Ujerumani kabla ya kuanza utekelezaji rasmi mwaka 1906.

Julai 12,1907, matumaini ya kuendelea kwa mradi yalififia baada ya Stiegler kushambuliwa na tembo akiwa kazini aliyesababisha umauti wake muda mchache baadae.

Stiegler alifikiri tembo wa Tanzania ni rafiki kama ilivyo kwa wale waliopo nchini India suala lilomfanya aondoe uoga na kujiingiza katika hatari hiyo iliyoondoa uhai wake na kukwamisha ujenzi wa bwawa hilo, hata Vita vya Kwanza vya Dunia vilipozuka kuanzia mwaka 1914 hadi 1918.

Na kuanzia siku hiyo, eneo hilo likaanza kujulikana kama Stiegler’s Gorge yaani bonde la Stiegler’s.

Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), Rufiji mkoani Pwani.Picha| Ikulu Mawasiliano.

Wazo halikufa wakati wa ukoloni

Baada ya Ujerumani kushindwa vita na Waingereza kuchukua utawala wa Tanganyika, wazo la kutumia Mto Rufiji kwa maendeleo liliendelea kufanyiwa tafiti.

Kati ya mwaka 1928 na 1933, wahandisi wa Uingereza waliandika upya mipango ya mradi huo. 

Tafiti nyingine zikaendelea kati ya mwaka 1939 na 1941 lakini mradi huo uliendelea kusalia katika makaratasi.

Mwaka 1956, wakoloni wa Uingereza waliukabidhi mradi huo kwa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), ambalo lilikamilisha andiko la mradi mwaka 196, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa Waziri Mkuu.

Baada ya wasilisho, Mwalimu alitaka mradi huo uzalishe zaidi ya umeme, ukichochea kilimo, umwagiliaji, viwanda na matumizi mengine ya maji. 

Baada ya uhuru, andiko hilo lilifanyiwa mapitio na kukamilika mwaka 1964, likilenga pia umwagiliaji katika Bonde la Rufiji na kudhibiti mafuriko.

Hata hivyo, changamoto za kifedha, kiuchumi na kiteknolojia ziliifanya ndoto hiyo isubiri kwa miaka mingi zaidi.

Baada ya Nyerere, Serikali zilizofuata ziliendelea kutazama uwezekano wa kuendeleza mradi huo.

Katika kipindi cha Rais Ali Hassan Mwinyi, kuanzia mwaka 1985 hadi 1995, juhudi za maendeleo ya sekta ya nishati ziliendelea, lakini Stiegler’s Gorge haikufikia hatua ya ujenzi.

Rais Benjamin William Mkapa, aliyeongoza kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, aliendelea kuwekeza katika miundombinu na nishati. Hata hivyo, ujenzi wa Stiegler’s Gorge bado haukuanza.

Kisha akaja Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Katika kipindi chake, kuanzia mwaka 2005 hadi 2015, wazo la kujenga Stiegler’s Gorge lilifufuliwa kwa nguvu mpya.

Mwaka 2010 Serikali ilianza kutafuta washirika na wawekezaji wa kimataifa kwa kuanza na Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva.

Rais huyo alitembelea Tanzania akiwa na ujumbe wa wafanyabiashara, akiwemo mwakilishi wa kampuni ya Odebrecht iliyokuwa imeonyesha nia ya kushiriki katika mradi huo.

Mwaka 2012, Rais Kikwete alitembelea Brazil katika juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kutafuta washirika wa miradi ya nishati.

Lakini pamoja na juhudi hizo, ujenzi wa bwawa haukuanza. Miaka iliendelea kupita na ndoto ya Stiegler’s Gorge bado haikuwa imegeuka kuwa uhalisia.

Taswira ya Mitambo 9 ya kuzalisha umeme, Rufiji mkoani Pwani. Picha|Ikulu Mawasiliano.

Magufuli na uamuzi wa kulivunja giza la kusubiri

Mabadiliko makubwa yalikuja mwaka 2015, wakati wa Serikali ya Hayati John Pombe Magufuli.

Wakati huo, kufikia eneo hilo kulihitaji miundombinu ambayo haikuwa rafiki kama ilivyo leo.

Lakini Magufuli aliona jambo moja kubwa, Tanzania haiwezi kuendelea kusubiri.

Mahitaji ya umeme yalikuwa yakiongezeka, wakati Taifa lilikuwa na rasilimali kubwa ya maji ambayo ingeweza kutumika kuzalisha umeme.

Mwaka 2017 Serikali ikaamua kuchukua hatua utekelezaji wa mradi huo ukapewa msukumo mkubwa.

Hatimaye, Desemba 12, 2018, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ilisaini mkataba wa ujenzi na ubia wa kampuni za Misri, Arab Contractors na Elsewedy Electric.

Kazi za ujenzi zikaanza rasmi Julai 26, 2019 ambapo, Rais Magufuli alifika eneo la mradi na kuzindua rasmi ujenzi wa Bwawa la Stiegler’s Gorge, ambalo baadaye lilipewa jina la Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere.

Hata baada ya Tanzania kumpoteza Rais Magufuli mwaka 2021 wakati ujenzi wa mradi huo ukiwa asilimia 33 Serikali mpya chini ya Rais Samia iliamua kuendeleza mradi huo.

Hatua kwa hatua, bwawa likajazwa maji, miundombinu ikakamilishwa na Februari 22, 2024, umeme ulianza kuzalishwa rasmi baada ya mtambo wa kwanza kuanza kufanya kazi.

Baada ya miaka mingi ya mipango, tafiti, kusubiri na ujenzi, maji ya Mto Rufiji sasa yalikuwa yakigeuza nguvu yake kuwa umeme wa kuingia katika Gridi ya Taifa.

Mpaka kufikia Machi 28, 2025, vitengo vyote tisa vya kuzalisha umeme vilifanikiwa kuunganishwa na kusawazishwa na Gridi ya Taifa.

Mitambo 9 ya kuzalisha umeme ndani ya Jengo la mitambo (Power House) katika Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP). Picha| Ikulu Mawasiliano.

Nguvu ya Mto Rufiji kwa Taifa

Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere lina uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme kupitia mitambo tisa, kila mmoja ukiwa na uwezo wa takribani MW 235.

Mradi unakadiriwa kuzalisha takribani gigawati-saa (GWh) 6,307 kwa mwaka.

Hii inaifanya kuwa kituo kikubwa zaidi cha kuzalisha umeme nchini Tanzania na sehemu muhimu ya mkakati wa Taifa wa kuongeza upatikanaji na usalama wa nishati.

Lakini umuhimu wake hauishii kwenye umeme. Mradi pia una malengo ya kusaidia udhibiti wa mafuriko, usimamizi wa maji na kuhakikisha mtiririko wa maji unaohitajika kwa mazingira ya Mto Rufiji unaendelea kudumishwa.

Ni historia ya zaidi ya karne moja iliyovuja jasho na damu, hadi leo, Agosti 22, 2026, tunapoitazama historia, tunagundua kwamba si hii hadithi ya bwawa lililojengwa tu ni hadithi ya ndoto iliyotimia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
22 Aug, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
22 Aug, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Lissu akutwa na kesi ya kujibu, ataja mashahidi 11, yumo Rais Samia

Lissu akutwa na kesi ya kujibu, ataja mashahidi 11, yumo Rais Samia

Nukta TV

EXCLUSIVE: Namna sahihi ya kunyonyesha baada ya kujifungu | Part 2

EXCLUSIVE: Namna sahihi ya kunyonyesha baada ya kujifungu | Part 2

Nukta TV

EXCLUSIVE | TEASER | Namna sahihi ya kunyonyesha baada ya kujifungua

EXCLUSIVE | TEASER | Namna sahihi ya kunyonyesha baada ya kujifungua

Nukta TV