Maphosa: Siwezi kuisahau saladi ya Juliana Tetti
- “Sijawahi kula mboga tamu kama ile tena na ugali tangu mwaka 2008”.
- Ni mboga yenye virutubisho vingi ikiwemo vitamin A, B1, C, D na E.
Kuna baadhi ya ladha hazifutiki kirahisi kwenye kumbukumbu. Hata upite miaka mingapi, kuna chakula ukikiona tu unarudi moja kwa moja kwenye siku ya kwanza ulipokila.
Hivyo ndivyo ilivyo kwa mwanadada Maphosa Banduka licha ya miaka 18 kupita, hadi leo hawezi kusahau kabisa saladi (watercress) aliyopikiwa mwaka 2008.
“Sijawahi kula mboga tamu kama ile hata siku moja. Alikuwa akiikata kidogo kidogo, anaitia nazi na nyama kwa ndani weee. Ladha yake ilikuwa ya kipekee,” anasimulia Maphosa huku akitabasamu anapokumbuka miaka hiyo.
Alipokuwa kidato cha sita, Maphosa alikuwa akiishi pamoja na Juliana Tetti (mama mlezi) ambaye hasa ndiye mtaalamu wa pishi la saladi lililomchanganya walipokuwa pamoja katika kijiji cha Mbokomu Kibonloni, wilayani Moshi vijijini.
Saladi ni mboga gani?
Saladi ni mboga ya majani inazopatikana zaidi katika maeneo yenye maji mengi kama vile chemchemi na kando ya mito.
Mara nyingi hupatikana zaidi katika maeneo yenye hali ya hewa ya baridi kama vile Kilimanjaro, Arusha na Iringa.
Mbali na kuwa na harufu nzuri, saladi ni mboga laini yenye ladha tamu ambayo wengi hupenda kula na ugali.
Kulingana na tovuti ya masuala ya afya, healthline saladi ni mboga ya majani yenye virutubisho vingi inayotoka katika familia ya ‘Brassicaceae’.
Kikombe kimoja cha saladi kina takribani kalori 4 pekee, lakini hutoa zaidi ya asilimia 100 ya kiwango cha kila siku kinachohitajika cha vitamini K, vitamini A na vitamini C.
Pia, ina viambata muhimu vya asili vinavyojulikana kama ‘antioxidants’ na ‘isothiocyanates’, ambavyo tafiti zinaonyesha vinaweza kusaidia kuilinda mwili dhidi ya baadhi ya magonjwa sugu, ikiwemo magonjwa ya moyo na aina mbalimbali za saratani, kama saratani ya utumbo mpana, mapafu, tezi dume na matiti.

Juliana na pishi la saladi
Maphosa anasimulia kuwa kabla ya kuanza mapishi, Juliana aliichambua vizuri saladi na kuisafisha vizuri kwa maji safi kabla ya kuanza kuikata.
Wakati akisubiri saladi ichuje maji, Juliana aliandaa tui la nazi pamoja na viungo vingine ikiwemo kitunguu maji, nyanya, karoti, giligilani pamoja na binzari nyembamba.
Pishi hili pia huchangwanywa na nyama, hivyo wakati anaandaa viungo tayari, nyama ya ng’ombe ilikuwa inaiva jikoni. Hakika kama ungeona maandalizi ya pishi hilo ungedhani kuwa Juliana anaandaa rosti ya biryani, lahasha ilikuwa ni saladi!
Juliana alianza kupika saladi kwa kuweka mafuta ya kupikia robo kijiko kwenye chungu cha asili kilichokuwa jikoni, kisha vitunguu ambavyo alikaanga mpaka vilipo pata rangi ya kahawia na kuegeza kwa dakika 2 kabla ya kuweka karoti na nyama.
“Kwa jinsi alivyokuwa fundi wa mapishi natamani angekuwa na Pressure Cooker kutoka jikosokoni.co.tz kama ninayotumia sasa, maana pishi lingekuwa pambe hatari,” anasimulia Maphosa ambaye uso wake ulikuwa na bashasha kana kwamba alikuwa anaona pishi hilo wakati huo na si miaka 18 iliyopita.
Baada ya kuweka nyama Juliana aliweka nyanya na kuzipika kwa dakika 5 hadi zikalainika kabla ya kuweka saladi juu ya mchuzi kisha akafunika kwa dakika mbili kabla ya kuweka tui la nazi na kuiacha ichemke tena kwa dakika saba.
“Aliniambia kwamba siku nikipika mwenyewe basi nihakikishe kuwa pishi hilo haliivi kupita kiasi kwani saladi ni mboga yenye maji mengi na laini hivyo huiva kwa haraka sana,” anasema Maphosa.
Maphosa anasimulia kuwa chakula kilipoandaliwa na kuwekwa mezani, hakuna siku alikula kama hiyo, anasema alitamani ugali usiishe kwenye sahani.

Ni miaka 18 sasa imepita tangu apikiwe pishi hilo, lakini kwa Maphosa saladi ya Juliana Tetti bado inabaki kama kipimo cha mboga tamu zaidi kuwahi kula.
Wakati mwingine, si chakula pekee kinachobaki kwenye kumbukumbu, bali ufundi wa mapishi na jinsi unavyokiandaa chakula chako unapokuwa jikoni.
Je, na wewe una chakula ambacho kimebeba simulizi ya maisha yako?, Kama jibu ni ndio unaweza kukoment hapa.