Wanawake zaidi 123 wanufaika na elimu, teknolojia ya nishati safi Pwani
- Wamesema matumizi ya nishati safi yameboreshaafya zao.
- Wanaufaika hao ni kutoka Wilaya ya Kisarawe, Kibaha na Mkuranga.
Dar es Salaam. Maisha yake yamebadilika, ndivyo unavyoweza kusema. Hapati tena magonjwa ya mfumo wa upumuaji, macho kuuma na kuwa mekundu. Pia hatumii muda mwingi jiko, bali katika shughuli za kujiingizia kipato kwa ajili ya familia yake.
Huyu ni Elizabeth Magnus, mkazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani ambaye ameachana na matumizi ya kuni kupikia. Sasa anatumia nishati ya gesi iliyochakatwa ya majumbani (LPG).
“Nilikuwa natumia kuni na mara nyingi moshi ulikuwa unanisumbua macho. Sasa napika kwa haraka zaidi na afya yangu imeimarika,” amesema Elizabeth.
Elizabeth ni miongoni mwa wanawake 123 wa Pwani waliofikiwa na elimu ya matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia na uzalishaji iliyotolewa wakati wa utekelezaji wa mradi wa EP7 ulioendeshwa na taasisi ya Mtandao wa Jinsia na Nishati Endelevu Tanzania (Tangsen) kuanzia Agosti 2023 hadi Juni 2026.
Wanawake hao wanatoka katika vikundi 56 vilivyopo katika Wilaya za Kibaha, Mkuranga na Kisarawe zilizopo mkoani humo.

Mratibu wa mradi huo, Mhandisi Leonard Pesambili akizungumza Julai 30, 2026, wakati wa kuhitimisha EP7 jijini Dar es Salaam amesema mradi huo uliwalenga wanawake wajasiriamali kwa kuwawezesha kutumia nishati safi kupikia na shughuli za uzalishaji zinazoongeza kipato.
“Tulilenga kuhakikisha wanawake wanapata teknolojia na maarifa ya kutumia nishati safi katika kupikia na uzalishaji ili kuboresha maisha yao na kuongeza fursa za kiuchumi,” amesema Pesambili.
Wanawake hao walifundishwa kutengeza na kuuza majiko banifu yasiohama na yanayohama, kupewa elimu ya ujasiriamali, kuwajengea uwezo wa kujiamini na kutafutiwa fursa za biashara ya bidhaa za nishati kupitia maonesho mbalimbali.
Mradi huo ulitekelezwa kwa ushirikiano na Wizara ya Nishati, Jinsia na Maendeleo ya jamii, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Shirika la Umeme Tanesco, halmashauri za maeneo husika pamoja na sekta binafsi.
Mhandisi huyo amesema uelewa mdogo wa matumizi ya nishati safi na gharama za awali za ununuzi wa vifaa bado ni miongoni mwa vikwazo vinavyokwamisha wanawake wengi kuhamia katika matumizi ya nishati hizo.
Amesema Tangasen itaendelea kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali kuwafikia wananchi kwa elimu na teknolojia ili wanufaike na faida za nishati safi ikiwemo kuinuka kiuchumi.
Utekelezaji wa mradi huo unaenda sambamba Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), unaolenga kuongeza matumizi ya nishati safi kutoka asilimia tisa hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Nishati, matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini kwa sasa yamefikia asilimia 28.6, ikiwa imesalia miaka nane kufikia lengo la mkakati huo.
Shule zafaidika
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Chole iliyopo Kisarawe, Sylvester Nzoa, amesema jiko banifu lililojengwa shuleni hapo kupitia mradi huo limepunguza matumizi ya kuni kutoka malori matatu hadi lori moja kwa mwaka.
Amesema hatua hiyo imepunguza gharama za ununuzi wa kuni kwa zaidi ya Sh1.6 milioni kwa mwaka, huku ikipunguza ukataji wa miti na kuhifadhi wa mazingira ya Mkoa wa Pwani.
Kwa mujibu wa Nzoa, jiko hilo lina uwezo wa kupika chakula cha wanafunzi 150 kwa kutumia vipande viwili vya kuni pekee, tofauti na majiko ya mafiga matatu yaliyokuwa yakitumia kuni nyingi zaidi.
Afisa Mazingira wa Mkoa wa Pwani na Mratibu wa Nishati Safi, Hadija Rajabu, amesema matumizi ya nishati safi yanapunguza magonjwa yanayosababishwa na moshi wa kuni, ikiwamo magonjwa ya mfumo wa upumuaji na macho, huku yakipunguza muda unaotumiwa na wanawake kupika.
“Nishati safi inampa mwanamke muda wa kushiriki shughuli nyingine za maendeleo ya familia na kuongeza kipato,” amesema.
Hadija amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali kutoa elimu na kuhakikisha wananchi wa Pwani wanatumia nishati safi.