Faida za kuzingatia usawa wa jinsia katika upatikanaji wa nishati Tanzania
- Ni pamoja na kuimarisha ustawi wa wanawake na kupunguza athari za kiafya.
- Wadau wa nishati waja na mpango kuongeza usawa wa nishati nchini.
Dar es Salaam. Nishati ni miongoni mwa hitaji muhimu kwa binadamu awaye yoyote, kwa kuwa si tu nyenzo inayofanikisha utendaji wa shughuli mbalimbali bali ndio msingi wa maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na Taifa husika kwa ujumla.
Licha ya Tanzania kufanikiwa kusambaza huduma ya nishati hususani ya umeme katika baadhi ya maeneo nchini, bado imebainika usawa wa kijinsia umekuwa hauzingatiwi wakati wa usambazaji wa nishati hiyo ili kuhakikisha jinsia zote zinanufaika na upatikanaji wake.
Ripoti ya Hali ya Upatikanaji na Matumizi ya Nishati ya mwaka 2020 inaonesha kuwa ni asilimia 8.1 pekee ya kaya nchini Tanzania zinatumia vyanzo vya nishati safi kwa kupikia.
Katika asilimia 92 ya kaya, ni wanawake hasa wanaowajibika kutafuta nishati ya kupikia ambapo wanabeba mzigo wa kukusanya kuni na kutumia teknolojia zisizo na ufanisi jambo linalo athiri afya zao, muda, na ufanisi.
Wizara ya Nishati inatambua kwamba upatikanaji wa nishati ya uhakika na gharama nafuu ni chachu ya kuimarisha ustawi wa wanawake hususan vijijini.
Soma zaidi: Mapinduzi ya teknolojia kilimo cha muhogo Tanzania
January Makamba, aliyekuwa Waziri wa Nishati wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo mwezi Mei, 2023 bungeni jijini Dodoma alibainisha kuwa nishati ya umeme vijijini itawezesha wanawake kupata elimu kupitia vyombo vya habari kuhusu masuala mbalimbali yanayowahusu kama vile elimu ya masuala ya afya ya uzazi, lishe na malezi bora,na haki za wanawake.
“nishati ya umeme vijijini inawezesha uboreshaji wa huduma za afya vijijini, ikiwemo za uzazi na pia kuwapunguzia wanawake adha ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kutafuta nishati ya kuni ambayo pia matumizi yake yana athari za kiafya hususan katika mfumo wa kupumua,” alisema Makamba.
Wadau wajitokeza
Kwa kutambua umuhimu wa usawa wa jinsia katika upatikanaji wa nishati nchini Tanzania Mtandao wa Kijinsia na Nishati Endelevu wa Tanzania (TANGSEN), kwa kushirikiana na ENERGIA, umezindua mpango wa miaka minne (Januari 2023-Desemba 2026) uitwao Mpango wa Usawa wa Kijinsia Katika Upatikanaji wa Nishati Safi na Hatua za Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania.
Kwa mujibu wa Tangsen Mpango huo una lengo la kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa za kuongoza na kunufaika na upatikanaji wa nishati ukitambua kuwa huduma hiyo ni haki muhimu kwa maendeleo.
Soma zaidi : Nishati jadidifu itakavyowainua kiuchumi wanawake Pwani
Aidha, mpango huo unalingana na Mpango Mkakati wa TANGSEN (2021-2025), wa kuendelea kuwawezesha wanawake katika sekta ya nishati na kusaidia mazingira yanayojumuisha zaidi jinsia katika sekta ya nishati nchini Tanzania.
Thabit Mikidadi ambaye ni Afisa Miradi kutoka Tangsen amebainisha kuwa mpango huo utajikita katika maeneo makubwa matatu ambayo ni sera, uwezeshaji, pamoja na utoaji wa elimu.
“Mpango huu unaangalia namna utakavyoweza kushawishi mabadiliko ya kisera katika sekta ya nishati hususani kwa taasisi za nishati zilizochini ya Serikali kama Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini (Rea) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), je sera zao zinazingatia masuala ya usawa wa kijinsia,” amebainisha Mikidadi.
Mikidadi ameongeza kuwa kutokana na maumbile, mifumo ya kijamii wanaume na wanawake hawana mahitaji yanayofanana ya nishati.
“Unakuta mama anahitaji zaidi nishati kwenye kupika au kuchota maji, baba yeye anahitaji zaidi kwenye shughuli za uzalishaji kama kuendesha mitambo, lakini baadae wote watahitaji nishati kwa ajili ya mwanga, au kupata habari,” amefafanua Mikidadi.
Kwa upande wake mtaalamu wa jinsia na nishati kutoka Tangsen Gisela Ngoo amebainisha kuwa sehemu ya pili ya mpango huo ni uwezeshaji kiuchumi ambapo kipaumbele kitakuwa kwa wanawake.
Ripoti ya Hali ya Upatikanaji na Matumizi ya Nishati ya mwaka 2020 inaonesha kuwa ni asilimia 8.1 pekee ya kaya nchini Tanzania zinatumia vyanzo vya nishati safi kwa kupikia.Picha l Tangsen
“Tunapokuja kwenye usawa tunaangalia nani yupo juu zaidi na tunamsaidiaje aliyepo chini kunyanyuka bila kumkandamiza aliyeko juu, ili waweze kwenda pamoja,” amesema Ngoo.
Ngoo ameongeza kuwa uwezeshaji wa kiuchumi utajikita zaidi katika kuwaongezea uwezo wanawake kuzalisha kwa kutumia rasilimali za nishati zilizopo maeneo yao katika shughuli za uzalishaji kama kupika, ufundi, ushonaji, au ususi.
Mikidadi amesisitiza kuwa, ili kuhakikisha mpango huo ambao umeanza kutekelezwa rasmi tangu Septemba 2023, watahakikisha wanatoa elimu kwa wadau wataoshirikiana ili kuwaongezea uelewa na waweze kutambua umuhimu wa mpango huo.
Maeneo, watu watakaonufaika
Kwa sasa mpango huo utaanza kutekelezwa katika Mikoa ya Pwani na Singida hususan katika Wilaya za Kisarawe na Ikungi, ambapo Tangsen wamebainisha kuwa uzoefu walioupata katika utekelezaji wa miradi mingine maeneo hayo ndio jambo lililowashawishi kuanza kutekeleza mpango huo huko.
Takribani watu 60,000 wanatarajiwa kuwa wanufaika wasio wa moja kwa moja wa mpango huo ambao utatekelezwa katika ngazi ya serikali za mitaa, ambapo katika kila wilaya zitateuliwa kaya 100 kwa ajili ya utekelezaji wake.
Mikidadi amewataka wadau wa nishati nchini kuitizama kwa jicho la tatu sekta hiyo kwa kuwa ina fursa nyingi zinazoweza kubadili hali ya kiuchumi na kijamii ya na kushawishi mifumo ya kiutawala huku akisisitiza kuzingatia suala la jinsia.
“Ni muhimu wadau wa nishati wakaanza kutizama nishati kwa jicho jingine, karibu kila nyanja ya maendeleo inahitaji nishati ili ifanikiwe lakini lazima tuhakikishe hatumuachi mtu nyuma,” amebainisha Mikidadi.