Faida Vodacom Tanzania yapaa mara tano, yafikia Sh47 bilioni
- Faida hiyo ni mara tano zaidi kulinganisha na faida ya Sh8.5 bilioni iliyokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imeanza mwaka mpya wa fedha kwa neema kwa kuripoti faida baada ya kodi ya Sh47.3 bilioni katika robo mwaka iliyoishia Juni 2026, ikiwa ni zaidi ya mara tano ya kiwango kilichoripotiwa mwaka jana.
Faida hiyo ni kubwa ikilinganishwa na Sh8.5 bilioni iliyopatikana katika kipindi kama hicho mwaka 2025 ikichochewa zaidi ukuaji wa mapato ya huduma za data na M-Pesa.
Kwa mujibu wa ripoti ya kifedha ya robo mwaka unaoishia June 30, 2026 mapato ya Vodacom Tanzania PLC yaliongezeka kwa asilimia 18.2 na kufikia Sh515.3 bilioni kutoka Sh435.9 bilioni yaliyorekodiwa katika robo iliyoishia Juni 2025.
Mapato hayo ya kampuni hiyo, yenye zaidi ya wateja milioni 28, yanaonyesha kuendelea kuimarika kwa kampuni hiyo kubwa ya mawasiliano iliyokuwa ikiripoti hasara miaka mitatu iliyopita.
M-Pesa, data ‘zaboost’ biashara
Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka mitatu sasa mapato yatokanayo na huduma ndiyo yanatunisha zaidi kibubu cha makusanyo ya kampuni hiyo mashuhuri ya mawasiliano nchini.
Mapato hayo yaliongezeka kwa asilimia 21.7 ndani ya mwaka mmoja na kufikia Sh510.89 bilioni yakichangia asilimia 99.15 ya mapato yote, uchambuzi wa ripoti hiyo ya kifedha uliofanywa na Nukta Habari, umebaini.
Vodacom inaeleza katika ripoti hiyo kuwa ukuaji huo ulisukumwa zaidi na ongezeko la matumizi ya huduma za data na M-Pesa ambayo yalikuwa kwa asilimia 26.3 na asilimia 26.0, mtawalia, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wateja pamoja na matumizi makubwa ya huduma za kifedha kupitia simu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, amesema maboresho ya mfumo wa M-Pesa ambao ulibadilishwa kutoa G 2.0 na kwenda Fintech 2.0 yaliongeza uwezo wa mfumo kuchakata miamala kwa kasi zaidi, kuimarisha usalama wa miamala na kurahisisha upanuzi wa huduma za kifedha kwa Watanzania wengi zaidi.
“Ninafurahi kuripoti mwanzo mzuri wa mwaka wa fedha 2027, uliotokana na utekelezaji thabiti wa mkakati wetu na uwekezaji endelevu katika mtandao na uwezo wa kidijitali, ambao umeendelea kuimarisha ukuaji wa biashara,” amesema Besiimire.
M-Koba, M-Wekeza, malipo ya kidijitali vyashika kasi
Mbali na matokeo ya kifedha, ripoti hiyo inabainisha huduma za kifedha za kidijitali zinaendelea kubadilisha namna Watanzania wanavyoweka akiba, kuwekeza na kufanya malipo.
Huduma ya M-Koba sasa inahudumia zaidi ya watumiaji milioni 1.5, huku akiba kupitia jukwaa hilo ikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 60, hasa miongoni mwa wanawake na vikundi vya kijamii.
M-Wekeza imeendelea kukua kwa kasi ambapo thamani ya uwekezaji kwa mwezi, kwa mujibu wa ripoti hiyo, imezidi Sh50 bilioni, ikiwa karibu mara tatu ya kiwango cha mwaka uliopita.
M-Wekeza ni miongoni mwa huduma kupitia simu za mkononi nchini zilizoleta fursa ya watu wa kawaida kuwekeza kiwango chochote cha fedha ili kupata faida na kutoa ushindani mkubwa kwa mifuko mingine ya uwekezaji.