Mambo ya kuzingatia kabla ya kuchukua mkopo 

June 30, 2026 4:38 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Angalia hali ya kipato chako, usikope kufanya anasa, nidhamu ya fedha ni muhimu.
  • Mkopo wenye riba nafuu na unaorejeshwa kwa muda mrefu ndio rafiki.

Dar es Salaam. Kwa baadhi ya watu, mkopo ni daraja la kuzifikia ndoto za kuanzisha biashara, kuongeza mtaji au kugharamia mahitaji muhimu ya maisha lakini kwa wengine ni mwanzo wa madeni sugu ambayo huwayumbisha kimaisha na wakati mwingine kuwarudisha kwenye umaskini.

Licha ya Serikali kuanzisha utaratibu maalum wa utoaji wa mikopo kwa makundi mbalimbali ikiwemo vijana, wanawake na makundi maalum, baadhi ya watu hukimbilia benki za biashara, taasisi za fedha, vikundi vya kijamii na hata majukwaa ya kidijitali yanayotoa mikopo bila kuwa na malengo suala linalowarudisha nyuma kiuchumi.

Hali hiyo mara nyingi haitokani na mkopo wenyewe, bali maamuzi ya kuuchukua bila kufanya tathmini ya kutosha kuhusu uwezo wa kuurejesha, sababu ya kuukopa au masharti yanayoambatana na mkopo husika.

Usikope kufanya anasa

Mtaalamu wa fedha na uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo, ameiambia Nukta Habari kwamba mikopo si tatizo au kitu kibaya, bali changamoto hujitokeza pale watu wanapokopa bila kuelewa kikamilifu masharti ya mkopo au wanapotumia fedha hizo katika matumizi yasiyozalisha mapato.

Kwa mujibu wa Kinyondo, watu wengi huvutiwa na kiasi cha fedha wanachoweza kukopa bila kufanya hesabu ya gharama halisi ya mkopo, hali inayowafanya wajikute wakishindwa kutimiza wajibu wa marejesho.

Anasema pia baadhi ya wakopaji hususan vijana na wanawake hufanya makosa ya kutumia mikopo kwa ajili ya matumizi ya anasa kama vile kununua simu za gharama, kufanya sherehe na kugaramia mtindo wa maisha unaozidi uwezo wao wa kifedha badala ya uwekezaji unaoweza kuzalisha kipato. 

“Mwingine kwanza anachukua mkopo alafu ndio anajiuliza afanye nini, mwingine amemuona mwenzake amefanya kitu fulani nayeye anachukua mkopo afanye kitu hicho bila kujua ni muda gani mtu ametumia kusimama imara, haya yote ni makosa ambayo vijana wengi wanakosea,” amesema Profesa Kinyondo.

Kuwa na nidhamu ya fedha 

Akifafanua kuhusu mambo ya kuzingatia yanayomhusu mkopaji mwenyewe Profesa kinyondo anasema ni vizuri kuangalia kitu unachoweka kama dhamana kwenye mkopo.

Anasema kuwa tofauti na mtu ambaye ameweka mshahara wake kama dhamana na kukatwa moja kwa moja, nidhamu ya hali ya juu inahitajika kwa mtu anaye tegemea biashara kulipa mkopo huo.

“Wewe kama ni mfanyabiashara maana yake mkopo ulioupata ukaufanyie biashara, ikupe faida alafu utoe katika faida kiwango ambacho utaenda kulipa. Hii inahitaji uwe na nidhamu kwamba nimepata faida hii, hiki sio cha kwangu nikirudisha kule,” ameeleza Profesa Kinyondo.

Tathimini kipato chako

Aidha, mtaalam huyo anaeleza kuwa kabla ya kuchukua mkopo ni muhimu kutathmini hali halisi ya kipato chako na uwezo wa kuurejesha endapo biashara au uwekezaji hautafanikiwa.

Anaeleza kuwa vijana wengi hukosea kwa kuchukua mikopo mikubwa wakisukumwa na ndoto za mafanikio bila kujiandaa na uwezekano wa kupata hasara.

“Ukichukua kiwango kidogo hata ukisema kwamba jamani nyumba yangu inauzwa nadaiwa milioni 5, watu wataingia mfukoni watakupa, lakini we unadaiwa milioni 100, wenyewe wakuuliza ulianzaje kwanza kukopa,” ametahadharisha mchumi huyo.

Anasisitiza kuwa kabla ya kukopa, mtu anapaswa kujiuliza kama ataweza kuendelea kulipa mkopo kwa kutumia kipato chake cha kawaida iwapo biashara itakwama.

“Ukiona huwezi kufanya hivyo, basi huo mkopo ni mkubwa kuliko uwezo wako,” anatahadharisha.

Elewa gharama za riba

Profesa Kinyondo anasema kiwango cha riba na muda wa kurejesha mkopo ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo mkopaji anapaswa kuyachambua kabla ya kusaini mkataba wa mkopo.

Anaeleza kuwa si busara kuvutiwa na kiasi cha fedha unachokopeshwa bila kuangalia gharama halisi za mkopo, kwani riba kubwa na muda mfupi wa marejesho vinaweza kuongeza mzigo wa kifedha na kuathiri maendeleo ya biashara.

Anashauri wakopaji kutafuta mikopo yenye riba nafuu na muda mrefu wa marejesho, kwani hali hiyo huwapa nafasi ya kuendesha biashara, kuzalisha mapato, kupata faida na kutenga fedha za kulipa marejesho bila kuathiri mtiririko wa shughuli zao.

“Mkopo mzuri ni ule ambao unachukua kwa riba nafuu lakini unalipa kwa muda mrefu,” amesisitiza Profesa.

Elimu ya fedha ni muhimu

Mbali na kuzingatia masharti ya mkopo na uwezo wa kuurejesha, elimu ya usimamizi wa fedha imeelezwa kuwa nguzo muhimu ya kuhakikisha mikopo inaleta maendeleo badala ya kuwa chanzo cha madeni na kupoteza mali za wakopaji.

Akizungumzia suala hilo, Profesa Abel Kinyondo anasema Serikali, ambayo kwa muda sasa imekuwa ikitoa mikopo ya riba nafuu kwa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum, inapaswa kwenda hatua zaidi kwa kuhakikisha wanufaika wanapatiwa elimu ya matumizi sahihi ya mikopo hiyo.

Vilevile, anazitaka taasisi za fedha kutokujikita katika kutoa mikopo na kuchukua dhamana za wakopaji wanaposhindwa kulipa, bali kufanya mafunzo ya usimamizi wa mikopo kuwa sehemu ya huduma wanazotoa.

“Kwenye nchi za wenzetu, ukishakidhi vigezo vya kupata mkopo, mafunzo ya jinsi ya kuutumia huwa sehemu ya mkopo unaopewa. Bahati mbaya sana sisi huku hatuna,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
30 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
30 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
30 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Matumizi ya Dola miamala ya ndani yanavyoweza kuathiri uchumi wa Tanzania

Matumizi ya Dola miamala ya ndani yanavyoweza kuathiri uchumi wa Tanzania

Nukta TV

"Kuzuia mikutano ya kisiasa kunaminya demokrasia

"Kuzuia mikutano ya kisiasa kunaminya demokrasia

Nukta TV

Mwigulu: Hatuna ugomvi na vyama vya siasa, watu wasichanganye mambo

Mwigulu: Hatuna ugomvi na vyama vya siasa, watu wasichanganye mambo

Nukta TV