Akili unde: suluhisho jipya mapambano dhidi ya ebola, uviko 19

June 23, 2026 3:24 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataalamu waeleza mchango wake katika kuboresha huduma za matibabu. 

Dar es Salaam. Katika harakati za kukabiliana na mlipuko wa Ebola uliosababisha mamia ya maambukizi na vifo, wanasayansi wamebaini tiba mpya inayotumia Akili Unde (AI) kubadili namna chanjo zinavyotengenezwa ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko.

Ugunduzi huo, unaotajwa kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa ya karne hii katika sekta ya afya, unatarajiwa kuleta matumaini mapya katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza hususan Ebola ambayo imeendelea kuikumba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambapo milipuko imekuwa ikijirudia mara kwa mara.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi Juni 17, 2026 zaidi ya watu 896 walikuwa wameambukizwa Ebola nchini DRC, huku zaidi ya 230 wakipoteza maisha hali inayoendelea kuongeza shinikizo la kupata suluhisho la haraka na la kudumu.

Katika muktadha huo, timu za utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge nchini Uingereza zimeanza kutumia AI kubuni chanjo za kizazi kipya zinazolenga kutoa ulinzi mpana dhidi ya virusi kama Ebola na aina nyingine zinazoweza kusababisha milipuko ya baadaye. 

Teknolojia hiyo inatumia uchambuzi wa kina wa data za virusi ili kutengeneza ‘super-antigen’ inayoweza kuamsha kinga ya mwili dhidi ya aina nyingi za vimelea kwa wakati mmoja, badala ya kulenga aina moja tu kama ilivyo kwenye chanjo za kawaida.

Watafiti wanasema mbinu hiyo inaweza kubadili mfumo mzima wa afya duniani kutoka ule wa kuitikia baada ya mlipuko hadi ule wa kuzuia kabla ya mlipuko kutokea, jambo ambalo linaweza kupunguza kasi ya kuenea kwa magonjwa hatari na kuokoa maisha ya mamilioni ya watu.

Katika baadhi ya nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania mabadiliko haya ya kiteknolojia tayari yanaanza kuonekana katika sekta ya afya. Picha| Canva.

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa mfano, imeanza kutumia mifumo ya Akili Unde kusaidia ufuatiliaji wa wagonjwa waliolazwa wodini kupitia teknolojia ya Smart Bed inayoweza kufuatilia viashiria muhimu vya afya kwa wakati halisi.

Akizungumzia maendeleo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk Delilah Kimambo wakati wa mahojiano na chombo cha habari cha Azam Mei 22, 2026 alibainisha kuwa akili unde imekuwa msaada mkubwa kwa madaktari na wauguzi katika kugundua mapema dalili za hatari kabla hali ya mgonjwa haijawa mbaya kiasi cha kuhitaji huduma za ICU. 

Mfumo huo umeongeza kasi ya maamuzi ya kitabibu na kusaidia kuboresha usalama wa wagonjwa hospitalini.

Hata hivyo, kwa mtazamo mpana wa kimataifa WHO inasisitiza kuwa AI ina uwezo mkubwa wa kuboresha uchunguzi wa magonjwa, ufuatiliaji wa wagonjwa na kuongeza ufanisi wa mifumo ya afya, lakini inapaswa kutumika kwa uangalifu ili kuhakikisha usalama, maadili na ulinzi wa wagonjwa.

Kwa mujibu wa watafiti wa Cambridge, chanjo zinazotengenezwa kwa kutumia AI tayari zimeonyesha uwezo wa kuchochea kinga dhidi ya virusi vya uviko 19 na hata aina zinazohusiana na virusi vya wanyama ambazo zinaweza kuibuka na kusababisha milipuko ya baadaye. 

Ingawa bado zipo katika hatua za majaribio, matokeo ya awali yanaonyesha usalama na uwezo wa msingi wa teknolojia hiyo.

Mbali na matumizi yake katika utengenezaji wa chanjo, wataalamu wa afya wanaona Aakili unde ikiwa na mchango mkubwa katika kuboresha huduma za matibabu.

AI kuongeza ufanisi wa tiba 

Mtaalamu wa dawa za usingizi na ganzi, William Astone kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili, amesema ukuaji wa teknolojia hii ya akili unde pia utasaidia kupunguza gharama na muda wa mgonjwa kukaa wodini kwa kurahisisha matibabu.

“Itasaidia sana kwenye kuboresha huduma hasa matibabu lakini pia vipimo vya wagonjwa na kutambua tiba sahihi kwamba aina gani ya dawa au nini tunaweza kumpa mgonjwa ,” amesema Astone.

Naye Dk Omary Mwangaza Mratibu wa Tiba na Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni  ameongeza kuwa AI inaweza kuleta mageuzi makubwa katika kuhudumia wagonjwa wengi kwa wakati mmoja.

 “Ikiwa kuna wagonjwa 100, AI inaweza kuwahudumia kwa muda mchache zaidi na kutoa majibu na usimamizi bora kuliko binadamu wa kawaida,” amesema Dk Mwangaza.

Kauli za wataalamu hao zinaonyesha kuwa Akili Unde inaendelea kuwa moja ya teknolojia zinazotazamwa kuwa suluhisho muhimu katika mapambano dhidi ya Ebola, Uviko-19 na magonjwa mengine ya mlipuko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
23 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
23 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
23 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Baba Levo: Wazo la kuongeza tozo kwenye bodaboda litolewe, tuleteeni watu wa tungi

Baba Levo: Wazo la kuongeza tozo kwenye bodaboda litolewe, tuleteeni watu wa tungi

Nukta TV

Mwanzo mwisho mapokezi ya Rais wa Namibia Netumbo Nandi Ikulu Dar es Salaam

Mwanzo mwisho mapokezi ya Rais wa Namibia Netumbo Nandi Ikulu Dar es Salaam

Nukta TV

Sikia kisa cha bibi wa Mbagala, chanzo Jaji Mkuu Masaju kupanda cheo

Sikia kisa cha bibi wa Mbagala, chanzo Jaji Mkuu Masaju kupanda cheo

Nukta TV