Tanzania iko tayari kwa uchumi unaotegemea teknolojia? 

June 20, 2026 2:45 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Takwimu zinaonyesha kuwa licha ya Tanzania kuwa na malengo ya uchumi wa Dola za Marekani trilioni moja unaoendeshwa na teknolojia, sekta ya tehama inachangia asilimia 1.5 tu ya GDP.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikilenga kujenga uchumi wa kidijitali wenye thamani ya Dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, mafanikio ya azma hiyo yatategemea kasi ya maboresho ya sera, teknolojia na mifumo ya kidijitali

Ripoti ya Usimamizi wa Masuala ya Kidijitali nchini Tanzania iliyozinduliwa katika Jukwaa la Afrika la Ubunifu na Teknolojia 2026 inaonyesha kuwa licha ya kuongezeka kwa matumizi ya intaneti, huduma za kidijitali na ubunifu wa teknolojia nchini, mchango wa sekta ya Tehama katika uchumi unaendelea kusuasua ikilinganishwa na matarajio ya Taifa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa na kampuni ya Tech & Media Convergence (TMC) sekta ya Tehama kwa sasa inachangia kati ya asilimia 1.5 hadi 1.6 ya Pato la Taifa (GDP) ambalo kwa mwaka 2025 limefikia thamani ya Sh234.1 trilioni.

Mkurugenzi Mtendaji wa TMC, Asha Abinallah anasema kuwa jambo la msingi si tu ushiriki wa Tanzania bali bali mazingira, kiwango cha uharaka, usawa na maandalizi kama taifa ndio jambo la msingi. Picha | TMC

Mkurugenzi Mtendaji wa TMC, Asha Abinallah aliyekuwa akizungumza katika ufunguzi wa jukwaa hilo anasema Tanzania tayari ipo kwenye mbio za ushindani wa kidijitali duniani, lakini mafanikio yake yatategemea mazingira yatakayowekwa kuhakikisha wananchi, biashara na taasisi zinashiriki kikamilifu katika mageuzi hayo.

“Swali la msingi si kama tunashiriki au la, bali tunashiriki katika mazingira gani na kwa kiwango gani cha uharaka, usawa na maandalizi kama taifa,”  amehoji Abinallah.

Changamoto ziko wapi ?

Ripoti hiyo inaeleza kuwa moja ya changamoto kubwa inayozorotesha kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidigitali nchini ni sera, ikiwemo masharti ya lazima ya kuhifadhi data na baadhi ya vikwazo vya umiliki kwa uwekezaji wa kigeni.

Masharti hayo yanaongeza gharama za uendeshaji kwa wawekezaji jambo linalotoa motisha ndogo kuwekeza. 

“Baadhi ya taasisi za kifedha hulazimika kutumia kati ya Sh1 bilioni hadi Sh5 bilioni kujenga vituo vya kuhifadhi data nchini, gharama ambazo kwa kiasi kikubwa haziongezi uzalishaji wala ubunifu wa huduma mpya,” imeeleza ripoti hiyo.

Ripoti inaonyesha kuwa moja kati ya changamoto kubwa inayozorotesha kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidigitali nchini ni sera. Picha | TMC

Aidha, mwingiliano kati ya mamlaka za udhibiti na maslahi ya kibiashara ya baadhi ya makampuni makubwa unaathiri ushindani wa soko kwa kuwapa nafasi kubwa zaidi wawekezaji wakubwa, huku wabunifu na kampuni ndogo zikikumbana na mazingira magumu ya kuingia na kukua kwenye soko. 

Matokeo ya hali hiyo ni kupungua kupungua kwa kasi ya ubunifu, jambo linaloathiri pia upatikanaji wa ajira mpya katika uchumi wa kidijitali.

Vilevile, baadhi ya sera za kodi na tozo zinazowagusa watoa maudhui pamoja na biashara za kidijitali zinaweza kuathiri ukuaji wa uchumi wa ubunifu kabla haujafikia kiwango kikubwa cha kuchangia ajira na mapato.

‘Miundombinu pekee haitoshi’

Akizungumzia mazingira yanayochochea ubunifu wa kidijiti kwenye jukwaa hilo Juni 18, 2026, Jeanne Clark kutoka Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema uzoefu unaonyesha kuwa ubunifu hustawi zaidi katika mazingira yaliyo wazi kuliko yale yenye udhibiti mkubwa.

Kauli hiyo inaendana na hoja zilizoainishwa kwenye ripoti kwamba ukuaji wa uchumi wa kidijitali hauhitaji tu uwekezaji wa miundombinu, bali pia mazingira yanayojenga imani kwa wawekezaji, wabunifu na watumiaji wa teknolojia.

Kwa upande wa biashara ndogo na za kati (SMEs), ripoti inaonyesha kuwa baadhi ya hatua za kifedha zilizowahi kuchukuliwa kwenye miamala ya simu zilichangia kupungua kwa matumizi ya njia za malipo za kidijitali, huku baadhi ya wananchi wakirejea kutumia fedha taslimu.

Jeanne Clark kutoka Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema uzoefu unaonyesha kuwa ubunifu hustawi zaidi katika mazingira yaliyo wazi kuliko yale yenye udhibiti mkubwa. Picha | TMC

Kwa mfanyabiashara mdogo, hali hiyo inapunguza urahisi wa kufanya biashara, kupokea malipo na kufikia wateja kupitia mifumo ya kisasa ya kifedha.

Kwa upande wa watumiaji wa kawaida, gharama za intaneti zinaendelea kuwa suala muhimu ambapo ripoti inaeleza kuwa muundo wa sasa wa umiliki na matumizi ya baadhi ya miundombinu mikuu ya mawasiliano unaweza kuathiri ushindani wa soko, hali inayoweza kuchangia gharama za huduma kubaki juu kuliko matarajio ya watumiaji.

Serikali yatia neno

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Nkundwe Mwasaga amesema takwimu zinazoonyesha mchango wa sekta ya kidijitali katika Pato la Taifa zinahitaji kueleweka kwa mapana zaidi ili kutoa picha halisi ya ukubwa wa uchumi wa kidijitali nchini. 

Mwasaga ameeleza kuwa Tanzania inatumia mfumo wa “core measure” pekee katika kupima mchango wa uchumi wa kidijitali, unaoonyesha mchango wa kati ya asilimia 1.5 hadi 1.6 ya GDP, lakini akasisitiza kuwa hiyo si picha kamili ya uchumi huo. 

“Kwa hakika, mchango wa uchumi wetu wa kidijitali si asilimia 1.6. Tatizo ni kwamba hatupimi kwa kutumia kipimo cha ‘narrow measure’.” amesema Mwasaga.

Kwa mujibu wake, Serikali ipo katika mchakato wa kuanzisha vipimo vipya vinavyopanua uelewa wa uchumi wa kidijitali, ikiwemo “narrow measure”, “broad measure” na hatimaye “digital society”, ambavyo vitahusisha sekta zote zinazotegemea au kuimarishwa na teknolojia. 

Alifafanua kuwa “core measure” ndiyo inayotumika sasa, inayojumuisha huduma na bidhaa za moja kwa moja za TEHAMA kama vifaa vya mawasiliano, programu, huduma za intaneti na miundombinu ya kidijitali. 

Hata hivyo, alisisitiza kuwa uchumi halisi wa kidijitali ni mkubwa zaidi kuliko asilimia inayoonekana kwa sasa, kwa sababu haujumuishi sekta nyingine zinazotegemea teknolojia kama afya, elimu, usafirishaji, kilimo na fedha. 

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Nkundwe Mwasaga amesema mchango wa uchumi wetu wa kidijitali si asilimia 1.6. Tatizo ni kwamba hatupimi kwa kutumia kipimo cha ‘narrow measure’. Picha | TMC

Katika eneo la ujuzi wa akili mnemba (AI), amesema Serikali imeweka mkakati wa ngazi tatu, ujuzi wa msingi, wa kati na wa juu ili kuwaandaa vijana na wananchi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali wa baadaye.

Akizungumzia nafasi ya uwekezaji wa kimataifa katika kukuza uchumi wa kidijitali nchini, Nkundwe amesisitiza kuwa Tanzania inahitaji kuendelea kushirikiana na washirika wa nje ili kufanikisha malengo yake ya maendeleo ya muda mrefu, hususan katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inayolenga kujenga uchumi wa dola trilioni moja unaoongozwa zaidi na sekta binafsi. 

“Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imeweka wazi lengo la kujenga uchumi wa dola trilioni moja, ambapo asilimia 70 ya uchumi huo itatokana na sekta binafsi… lakini tunataka kuendelea kulinda na kudumisha maadili yetu hadi kiwango fulani,” amesema Mwasaga 

Mbali na kauli ya Mwasaga, Serikali pia imeanza kuchukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha Tanzania inaelekea mageuzi ya uchumi wa digitali.

Katika mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali 2026/27 ambayo ndiyo bajeti ya kwanza kuanza kutekeleza Dira 2050 Serikali imependekeza kufuta matumizi ya vocha za kukwangua katika maeneo ya mijini ili kupunguza matumizi ya pesa taslim na kuhamasisha malipo ya kidigiti.

Aidha, pamoja na mambo mengine imependekeza kupunguza muda wa kuanza kulipa kodi kwa wafanyabiashara wadogo na wakati kutoka miezi mitatu mpaka mwaka mmoja baada ya kusajili biashara huku ada za watengeneza maudhui zikipunguzwa kuchochea ukuaji wa uchumi huo.

TMC imetoa mapendekezo kwa Serikali, wadau na watunga sera ikiwemo ikiwemo kuondolewa kwa masharti ya lazima ya kuhifadhi data nchini na badala yake kutumia mifumo ya kisasa ya usalama wa data inayotambulika kimataifa. Picha | TMC

Nini kifanyike ?

Hata hivyo, TMC imetoa mapendekezo kwa Serikali, wadau na watunga sera ikiwemo ikiwemo kuondolewa kwa masharti ya lazima ya kuhifadhi data nchini na badala yake kutumia mifumo ya kisasa ya usalama wa data inayotambulika kimataifa.

Mapendekezo mengine ni kulegeza masharti ya usajili wa ‘Virtual Private Network’ (VPN) na leseni za maudhui ya mtandaoni, pamoja na kuimarisha ushindani katika matumizi ya miundombinu ya mawasiliano.

Akiwasilisha mapendekezo ya wadau mbalimbali walioshiriki mjadala huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tech & Media Convergence, Joan Kimirei, amesema majadiliano hayo yalilenga kutathmini fursa, changamoto na mageuzi ya kimuundo yanayohitajika ili kuiongoza Tanzania na Afrika kwenye mustakabali wa kidijitali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
15 Jul, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
16 Jul, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
16 Jul, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Kutana na ‘Poultry Plucker’, mashine inayonyonyoa kuku watatu kwa dakika moja

Kutana na ‘Poultry Plucker’, mashine inayonyonyoa kuku watatu kwa dakika moja

Nukta TV

Rais Samia: Kalamu yangu ina hatari, sijawahi kusaini mtu kunyongwa

Rais Samia: Kalamu yangu ina hatari, sijawahi kusaini mtu kunyongwa

Nukta TV

Rais Samia: Matumizi jina Samia, likiwa kila mahali inachosha, tafuteni wengine

Rais Samia: Matumizi jina Samia, likiwa kila mahali inachosha, tafuteni wengine

Nukta TV