Dira ya Taifa 2050 kukuza uchumi wa Tanzania

December 11, 2024 5:21 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Imelenga kukuza pato la mtu mmoja mmoja kati ya Sh12.5 milioni hadi Sh20.8 milioni

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amezindua rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo inalenga kukuza uchumi wa Tanzania kufikia uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050. 

Dira hiyo inayotoa mwongozo wa malengo na mwelekeo wa maendeleo ya nchi kwa miaka 25 itaanza kutekelezwa mwaka 2025 hadi mwaka 2050 ikihakikisha upatikanaji wa maendeleo yenye usawa kwa wananchi wote.

Rais Mwinyi aliyekuwa akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanyika Zanzibar leo Disemba 11, 2024 amesema dira hiyo ina malengo makuu matano yanayogusa sekta za uchumi, maendeleo ya jamii, utawala bora na utunzaji wa mazingira.

“Kwanza ni kuwa Taifa lenye uchumi endelevu na jumuishi wa kipato cha kati cha juu, uchumi huu utamilikiwa na makundi yote ikiwemo wanawake, watoto na watu wenye ulemavu na unaoongozwa na uvumbuzi” amesema Dk Mwinyi.

Itakumbukwa kuwa Julai 2, 2020 Benki ya Dunia iliiorodhesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kipato cha kati wa chini ikichangizwa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji wa megawati 2500.

Miradi hiyo ilitoa ajira kwa watu wengi hali iliyochangia kukua kwa pato la mtu mmoja mmoja kwa mujibu wa Dk Hassan Abasi aliyekuwa msemaji wa Serikali wakati huo.

Sambamba na hayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof Kitila Mkumbo amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 imelenga kuvuka pato la mtu mmoja la dira ya 2025 lililokuwa na wastani wa dola za Marekani 3,000 kwa mwaka, sawa na Sh6.9 milioni (kwa viwango vya kubadilisha fedha wakati dira hiyo ilipoandaliwa).

“Shabaha kuu ni Tanzania kuwa nchi yenye kipato cha kati ngazi ya juu, ikichagizwa na sekta za uzalishaji viwandani. Tunatarajia kufikia pato la mtu kati ya Sh12.5 milioni na Sh20.8 milioni, huku pato la taifa likifikia Sh1.8 ‘quadrillion’ ifikapo 2050,” amesema Prof Mkumbo.

Huenda utekelezaji wa malengo hayo ukaifanya Tanzania iingie katika orodha ya nchi zenye uchumi wa kati wa juu kama ilivyo nchi ya Afrika ya Kusini.

Malengo mengine makuu ya Dira ya Taifa 2050 Kwa mujibu wa Dk Mwinyi ni kufikia maendeleo ya watu wote kwa kuwa Taifa linalotoa fursa sawa za maendeleo kwa wanawake, vijana, watoto, na wanaume, ili kila mmoja aweze kutumia uwezo wake kwa manufaa ya jamii.

Ili kuhakikisha maisha bora na ustawi kwa wote ambapo Serikali inalenga kuhakikisha maisha bora kwa kila raia kupitia kuboresha huduma za jamii kama afya, elimu, na miundombinu.

Dira hiyo pia itabainisha mfumo wa utawala kuwa wazi, jumuishi, na wenye kudai uwajibikaji ili kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu katika maamuzi ya kitaifa.

Si hayo pekee Serikali kupitia dira hiyo pia itahakikisha utunzaji wa mazingira, uendelevu wa rasilimali za nchi kwa kizazi kijacho na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

 Sekta za kimageuzi

Katika hotuba yake Rais Mwinyi amesema mafanikio ya Tanzania kufikia uchumi wa kati wa juu yatategemea sekta chache ambazo zitakuwa na uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa na ya haraka katika uchumi wa nchi.

“Sekta zenye sifa hizo zitapewa kipaumbele hasa katika bajeti ili ziweze kuleta mageuzi makubwa hatimae kuifanya nchi yetu iwe yenye hadhi ya kipato cha kati cha juu,” amesema Rais Mwinyi.

Baada ya uzinduzi wa rasimu hiyo zoezi linalofuata ni ushirikishwaji wadau kwa ajili ya uhakiki ili kuona kama maoni waliyoyatoa yamezingatiwa kikamilifu na kama sivyo yafanyiwe tena kazi.

Enable Notifications OK No thanks