Vijana wa kitanzania kunufaika na uchumi wa kidigitali
- Serikali imesema inaandaa sera na miongozo itakayonufaisha vijana.
Arusha. Serikali ya Tanzania imesema inaendelea kuimarisha mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ili kutoa fursa kwa vijana kunufaika na uchumi wa kidigitali.
Uchumi huo unaohusisha matumizi ya teknolojia na mtandao katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ni miongoni mwa masuala yanayopewa kipaumbele duniani kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Waziri wa Wizara ya Vijana, Joel Nanauka aliyekuwa akizungumza Leo Mei 25, 2026 katika jukwaa la tisa la vijana (You Lead Summit 2026) linalowakutanisha viongozi vijana, watunga sera, wabunifu, watendaji wa asasi za kiraia pamoja na wadau wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika amesema Serikali inaendelea kuweka miundombinu wezeshi kwa vijana kunufaika na uchumi huo.
“Sera nyingi tunazozitengeneza sisi kama Serikali ni kuhakikisha kwamba uchumi wa kidigiitali unapanuliwa hasa kwa kuwasaidia vijana kupata ujuzi wa kisasa kwa mfano mambo ya akili mnemba, uchambuzi wa data na biashara mtandao,” amesema Nanauka leo Mei 25, 2026.
Mikakati hiyo ya Serikali inaenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kidijitali wenye ushindani atakaowezesha zaidi ya asilimia 80 ya huduma za Serikali kupatikana kupitia mifumo salama na jumuishi ya kidijitali huku asilimia 70 ya wananchi wakiwa na ujuzi huo wa kigitali.
Ili kutekeleza azma hiyo, Angellah Kairuki, Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari alisema bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 imeelekezwa katika kuimarisha uwekezaji wa miundombinu ya TEHAMA ili kuiwezesha Tanzania kusonga mbele kuelekea uchumi wa kidijitali.
Miongoni mwa miradi itakayotekelezwa ni ujenzi na uendelezaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano,minara ya mawasiliano vijijini, na kuimarisha mifumo ya TEHAMA kupitia miradi minane inayotekelezwa na wizara pamoja na taasisi zake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (MS TCDC), Dk Anna Haule amesema kongamano hilo hutoa fursa kwa vijana kupaza sauti kuhusu changamoto wanazokutana nazo kwa uhuru.
“Ni muhimu kwetu kuhakikisha vijana wana sehemu ya wazi kujadili kuhusu uongozi, biashara na mabadiliko ya mazingira, tunafurahi kuona vijana wanakuja wanaongea hapa na kupata suluhu ya pamoja,” amesema Dk Anna.
Baadhi ya washiriki wameimbia Nukta Habari kuwa wakati Serikali ikiendelea na maboresho wa sera na mifumo, ni wakati sahihi wa vijana kuanza kuchangamkia fursa zitokanazo na uchumi huo ili kukabiliana na changamoto ya ajira inayoendelea katika nchi nyingi duniani.