NMB yaweka kibindoni $80 milioni kukuza utoaji mikopo Tanzania
- NMB inatarajia kuongeza mtaji wa utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu na ya muda mrefu kwa wakulima, wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs).
Dar es Salaam. Benki ya NMB PLC imeingia makubaliano ya kifedha ya Dola za Marekani 80 milioni takriban Sh200 bilioni kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa mitaji kupitia mikopo ya masharti nafuu kukuza kilimo, biashara ndogo na za kati nchini.
Katika makubaliano hayo, NMB itapokea mkopo wa Dola za Marekani milioni 30 kutoka Taasisi ya Uwekezaji wa Maendeleo ya Serikali ya Norway (Norfund) na uwekezaji wa Dola milioni 50 kutoka Shirika la uwekezaji wa maendeleo la Serikali ya Uingereza la British International Investment (BII).
Kwa mujibu wa taarifa ya Norfund fedha hizo zitaongeza mtaji utakaoiwezesha NMB kupanua wigo wa huduma za kifedha kama vile utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu na ya muda mrefu hususan kwa wakulima pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs).
BII na Norfund ni taasisi za uwekezaji wa maendeleo zenye lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo katika nchi zinazoendelea kupitia uwekezaji katika sekta muhimu ikiwemo kilimo, huduma za kifedha, nishati na biashara.
NMB ni miongoni mwa benki kubwa mbili za biashara nchini ikichuana vikali na CRDB ambazo kwa mwaka wa fedha wa 2025 zilivuka faida kabla ya kodi ya Sh1 trilioni.

Ushirikiano huo mpya baina NMB na BII pamoja na Norfund utaendelea kuipa nafasi benki hiyo kuwa miongoni mwa taasisi za fedha zinazosaidia kukuza uchumi jumuishi na endelevu nchini.
NMB imeeleza katika mtandao wa LinkedIn kuwa makubaliano hayo yaliyofanyika jijini Kigali Mei 15, 2026 yataisaidia benki hiyo kufikia malengo yake ya kuchochea mabadiliko ya kiuchumi ya muda mrefu nchini.
Kwa muda mrefu wafanyabiashara wadogo na kampuni zimekuwa zikihaha kupata mikopo yenye riba nafuu ikiwemo kwenye sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi kama kilimo, nishati safi na viwanda.
Licha ya mikopo kwa watu na sekta binafsi kuongezeka mwaka hadi mwaka takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha bado viwango vya riba vipo juu huku baadhi ya benki za biashara zikiwa na masharti magumu kutimizwa.
Ripoti ya BoT inaonyesha kuwa wastani wa kiwango cha riba za mabenki ulikuwa asilimia 15.24 mwaka 2025 ikiwa ni ahueni kiduchu kutoka asilimia 15.71 iliyorekodiwa mwaka 2024.
Latest