Rais Samia: Vijana 7,593 wamepata ajira nje ya nchi
- Vijana 7,593 wanufaika na ajira nje ya nchi kupitia uratibu wa Serikali.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema jumla ya vijana 7,593 wamenufaika na fursa ya ajira nje ya nchi suala linaloendelea kupunguza changamoto ya ajira nchini.
Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika mkoani Njombe amesema idadi hiyo imefikiwa kutokana na mikakati ya ushirikiano wa kimataifa.
“Katika hili nakubaliana na TUCTA kwamba tunahitaji kuwa na utaratibu wa wazi na usimamizi madhubuti wa Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ili kuhakikisha haki na maslahi yao yanalindwa ipasavyo,” amesema Rais Samia.
Ili kuendelea kufungua fursa nyingi zaidi za ajira nje ya nchi Rais Samia amesema Serikali yake itaendelea kuratibu fursa hizo ili zilete tija kwa vijana.
Hii sio mara ya kwanza kwa Serikali kuzungumzia suala la ajira nje ya nchi.
Januari 9,2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu alieleza kuwa Serikali imefanikiwa kuzalisha zaidi ya ajira 1,400 kwa vijana na wanawake kwenda kufanya kazi nje ya nchi kati ya Novemba 2025 hadi Januari 2026.
Katika kipindi hicho jumla ya vijana 1,432 walipata ajira nje ya nchi kama matokeo ya kuimarika kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na TUCTA pamoja na kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kadri uchumi utakavyo ruhusu.

Rais Samia amesisitiza kuwa katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kisiasa duniani, waajiri na wafanyakazi wanapaswa kujiandaa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.
Amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu, maarifa na ujuzi ili kuimarisha nguvu kazi ya taifa na kuiwezesha kushindana katika soko la ajira la sasa na la baadaye pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ambayo inaajiri mamilioni ya Watanzania.
Kwa upande wake, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya amesema bado kuna changamoto za kimuundo katika mifumo ya utumishi wa umma, ikiwemo masuala ya maendeleo ya watumishi wanaopata elimu ya juu lakini kukosa ulinganifu wa mishahara wanaporudi kazini.

Amesema changamoto hizo zimekuwa zikiathiri baadhi ya kada za wafanyakazi, wakiwemo watafiti, na kuomba Serikali kuzifanyia kazi.
Latest