Dk Mwigulu mgeni rasmi siku ya uhuru wa vyombo vya habari
- Kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kuwa Aprili 30, 2026 jijini Arusha.
- Ni fursa kwa wadau wa sekta ya habari na Serikali kujadili changamoto na mwelekeo wa tasnia ya habari nchini.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yatakayofanyika jijini Arusha, Aprili 30 mwaka huu.
Kwa kawaida maadhimisho hayo hufanyika nchini Tanzania na maeneo mengine duniani Mei 3 kila mwaka yakilenga kukutanisha wadau wa sekta ya habari na mawasiliano kufanya majadiliano ya kitaaluma, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili tasnia hiyo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Tech and Media Convergency (TMC), Asha Abinallah ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi kwa mwaka huu amesema maadhimisho ya mwaka huu yatagusia masuala muhimu ikiwemo akili mnemba.
“Tutakuwa na mijadala mbalimbali ikiangazia mambo yanyoibuka katika sekta ya habari, sasa hivi kuna watengeneza maudhui lakini pia kuna teknolojia ya akili mnemba ambayo inakuwa kwa kasi,” amesema Abinallah aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Machi 27, 2026 jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo utakaofanyika kwa siku tatu kuanzia April 28 hadi 30 jijini Arusha unatarajia kukutanisha takribani washiriki 600 ikiwa ni mara ya 33 tangu kuanzishwa nchini Tanzania.
Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa ni miongoni mwa waandaaji wa maadhimisho hayo, yanayotarajia kuleta matokeo chanya yatakayosaidia kukuza sekta ya habari nchini Tanzania
Kwa takribani miaka nane sasa, Nukta Africa imekuwa mdau muhimu katika sekta ya habari na mawasiliano nchini Tanzania kupitia utoaji wa mafunzo ya mara kwa mara kwa wanahabari yanayoendana na mahitaji ya soko la sasa, ikiwemo kozi za uthibitishaji habari (Fact-Checking), uandishi wa habari za takwimu (Data Journalism), ubunifu wa infografia (Infographics Design), na usimamizi wa maudhui ya kidijitali (Digital Content Management).
Wadau wengine wa maadhimisho hayo ni pamoja na Serikali kupitia Idara ya Habari–MAELEZO, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Umoja wa Mataifa (UN), pamoja na asasi mbalimbali za kiraia.
Serikali kukutanishwa na wadau
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari–MAELEZO, Evody Kyando akiwakilisha Serikali, amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu kwa wadau wa sekta ya habari kujadili changamoto na mwelekeo wa tasnia hiyo nchini.
“Maadhimisho haya ni fursa kwa Serikali kukutana na washirika wake wa maendeleo na asasi za kiraia kujadili masuala ya mabadiliko ya utendaji kazi katika sekta ya habari, usawa wa kijinsia, usalama wa waandishi wa habari pamoja na kuwaendeleza watayarishaji wa maudhui,” amesema Kyando.
Ameeleza kuwa jukwaa hilo pia litasaidia kuibua changamoto za kisera na kujadili maboresho yatakayochangia kuimarisha mchango wa vyombo vya habari katika maendeleo ya Taifa.
Latest