Maoni mchanganyiko tume ya uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29 ikiongezewa muda
- Wananchi wasema hawaoni sababu ya tume kuongezewa muda.
Dar es Salaam. Siku tatu baada ya tume ya kuchunguza matukio wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 kutangaza kuongezewa muda wa siku 42, baadhi ya wananchi na wadau mbalimbali wameibuka na maoni mchanganyiko kuhusu uamuzi huo.
Akizungumza katika mahojiano na Nukta Habari leo, Februari 23, 2026, mchambuzi wa siasa za kimataifa, Lugete Mussa Lugete amesema uamuzi wa kuongezewa muda kwa tume utasaidia kufanya kazi kwa weredi na kuwasilisha ripoti itakayosaidia kujenga umoja, mshikamano na maridhiano ya kitaifa.
““Watu waliopata maumivu ni wengi mashuhuda ni wengi na bado tume inafanya kazi ya kukusanya ushahidi nini kilichotokea madhara yaliyotokea na nini kifanyike kuelekea kwenye maridhiano na upatanishi wa kitaifa…
…Watu wana maumivu kwa hiyo lazima mchakato wa uchunguzi, upelelezi, kusikiliza pande mbali mbali uchukue muda,” amesema Lutege.
Akizungumzia ushirikishwaji wa wataalamu wa nje katika uchambuzi wa maoni na ushahidi, amefafanua kuwa suala hilo limefanyika ili kuongeza imani za Watanzania juu ya tume hiyo.
“Kuna watu hawana imani na wataalamu wa ndani hivyo lazima tupate wataalamu wa wa teknolojia, inteligensia na wataalamu mambo ya ujasusi…ili kwa pamoja turudishe misingi ya imani,” ameeleza.
Hata hivyo, si wananchi wote wanaounga mkono nyongeza hiyo ya muda. Mkazi wa Jiji la Arusha, Elihuruma Laiza, amesema hafurahishwi na uamuzi huo, akieleza kuwa haoni umuhimu wa kuongezwa kwa muda huo wa siku 42.
“Sioni kama kuna umuhimu wa tume kuongezewa muda, sababu siku 90 ni siku nyingi sana kuchunguza kitu ambacho kilikuwa kiko wazi kwa namna hiyo,’’ amesema Laiza.
Kwa upande wake Angela Mikaya mkazi wa jiji la Dar es Salaam amesema wakati wananchi wakisubiri kwa matarajio makubwa majibu kutoka kwa tume, Serikali imeamua kuongeza muda jambo ambalo kwake halionekani kuwa la busara.
Tume ya kuchunguza matukio yaliyotokea kabla ya baada ya uchaguzi mkuu iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan Novemba 19, 2025, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman pamoja na wajumbe wengine saba.
Sababu kubwa ya kuundwa kwa tume hiyo ilikuwa ni kuchunguza matukio hayo kubaini sababu na kuwasilisha ripoti ya kina kwa mkuu wa nchi ikipewa siku 90 kukamilisha kazi hiyo ambazo zilimalizika Februari 20, 2026.
Hata hivyo, Februari 20, 2026, tume hiyoo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari ilibainisha kuongezewa muda wa siku 42 utakaoisha April 3, 2026 ikilenga kutoa fursa ya kukusanya maoni zaidi kwa wananchi waliosalia.
Kulingana na tume hiyo, sababu za kuongezwa muda ni pamoja na wingi na mchanganyiko wa taarifa zilizokusanywa, ulazima wa kushirikisha wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi na kidijitali kutoka ndani na nje ya nchi, pamoja na kubainika kwa mapengo katika baadhi ya vielelezo vinavyohitaji kukamilishwa.
Aidha, tume imeeleza kuwa bado kuna baadhi ya wadau muhimu ambao hawajafika mbele ya tume licha ya kupatiwa mialiko zaidi ya mara moja.
Latest