Fursa, vituo vya CNG vikiongezeka Tanzania
- Kuongezeka kwa vituo vya CNG kunatarajia kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza matumizi ya nisati safi, na kuongeza nafuu kwa sekta ya usafirishaji na viwanda.
Dar es Salaam. Huenda watumiaji wa vyombo vya moto nchini Tanzania vinavyotumia gesi asilia (CNG) wakapata ahueni kiduchu mara baada ya kampuni ya Puma Energy kuzindua kituo kipya jijini Dar es Salaam.
CNG, ni gesi asilia iliyoshinikizwa, ambayo hutumika kama nishati mbadala kwenye magari na matumizi mengine ikitajwa kuwa ni nafuu zaidi na rafiki kwa mazingira kulinganisha na nishati nyingine kama petroli na dizeli.
Gesi hiyo ilianza kupata umaarufu nchini Tanzania kuanzia mwaka 2022 kuelekea 2023, baada ya Serikali kuanza kusukuma matumizi ya nishati mbadala na kampuni binafsi kuanza kuweka vituo vya kujaza gesi pamoja na huduma za kubadilisha mifumo ya magari.
Umaarufu huu uliongezeka zaidi ambapo idadi ya magari yaliyobadili mfumo kutoka petroli au dizeli kwenda CNG na yaliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya matumizi hayo.
Kufikia mwishoni mwa mwaka 2025 vyombo vya moto 8,500 vilikadiriwa kufungiwa mfumo wa CNG kutokana na gharama nafuu za uendeshaji na upatikanaji wa vituo vya kujazia gesi katika maeneo ya Dar es Salaam na miji mingine.

Licha ya umuhimu wa gesi hiyo nchini bado watumiaji wa vyombo vya moto wanakumbana na adha ya upatikanaji wa gesi hiyo kutokana na vituo kuwa vichache.
Vituo vilivyotumika kwa ajili ya kujaza gesi hivyo jijini Dar es Salaam ni pamoja na TAQA Dalbit ya Misri , Master Gas, pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) vilivyopo jijini Dar es salaam jambo linalofanya kuwepo kwa msongamano katika vituo vya kujaza gesi.
Katika kupunguza changamoto za upatikanaji wa gesi hiyo, Februari 9, 2026 kampuni ya Puma ilizindua kituo kipya Salasala jijini Dar es Salaam na kufanya idadi ya vituo hivyo nchini Tanzania kufikia 16 suala litakaloenda kupunguza adha kwa watumiaji.
Kupitia kituo hicho kipya watumiaji wanaotokea nje kidogo ya jiji hilo wana uhakika wa kupata huduma hiyo bila kusafiri umbali mrefu wa kilomita 10 hadi 13 au kutumia dakika 30 hadi 40 kukifikia kituo cha karibu zaidi cha TPDC Mlimani.
Serikali yajipanga kuongeza vituo vya CNG
Kwa kutambua umuhimu wa gesi hiyo Serikali ya Tanzania imeweka mmikakati ya muda mrefu na mfupi ya kuongeza vituo hivyo katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.
Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kituo hicho jana ameiagiza Wizara ya Nishati kuongeza kasi ya kupanua mtandao wa usambazaji wa gesi asilia ili kukidhi mahitaji ya Taifa.

Amesema kwa kufanya hivyo kutawawezesha wananchi kupata nafuu ya gharama katika uendeshaji wa vyombo vya moto na matumizi mengine ya nishati pamoja na Serikali kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza mafuta.
Pamoja na hayo November, 2025 Serikali ililiagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza idadi ya vituo vya kujaza CNG nchi katika mikoa mingine kama Dodoma, Arusha, Morogoro na Tanga kwa ajili ya kupunguza gharama za maisha na kuboresha huduma kwa wananchi.
Latest