Rais Museveni kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania

February 6, 2026 10:54 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Anatarajiwa kufanya mazungumzo yatakayojikita kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi.

Dar es Salaam. Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku moja kesho, Februari 7, 2026 ikiwa  ni sehemu ya kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Uganda.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu leo Februari 6, 2026 inabainisha kuwa katika ziara hiyo Museveni anatarajiwa kukutana na Rais Samia Suluhu kwa ajili ya mazungumzo ya faragha na baadaye mazungumzo rasmi yatakayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

“Mazungumzo yao yatajikita kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili, na kujadili masuala muhimu ya kikanda na kimataifa,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Mseven anaitembelea Tanzania ikiwa ni siku 23 tangu atangazwe rasmi kuwa mshindi wa kiti cha urais wa nchi hiyo katika uchaguzi uliofanyika Januari 15 mwaka huu, jambo linaloashiria mwendelezo wa uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa karibu kati ya mataifa hayo mawili.

Rais Museveni aliwahi kuitembelea Tanzania Julai 2019, katika Serikali ya awamu ya sita iliyoongozwa na Rais John Magufuli ambapo pamoja na mambo mengine alisistiza uhusiano wake na Tanzania kupitia ujenzi wa bomba la mafuta toka Hoima hadi Tanga, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na uwanja wa ndege wa Chato.

Tangu wakati huo Tanzania na Uganda zimeendelea kuwa na uhusiano wa karibu wenye tija kwa nchi zote mbili.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, masuala yatakayozungumza katika ziara ya museveni wakati huu ni nishati hususan Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP), ambao unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa nchi zote mbili na kanda kwa ujumla.

Baada ya mazungumzo hayo, Rais Museveni na mwenyeji wake, Rais Samia, wanatarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu makubaliano na maeneo ya ushirikiano yatakayojadiliwa.

Rais Museveni anatarajiwa kuondoka nchini baada ya kumaliza ziara hiyo ya siku moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks