Mambo matatu yanayomsubiri Museveni Uganda

January 19, 2026 7:47 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana na rushwa.

Dar es Salaam. Yoweri Museveni, huenda ndio jina linalosikika zaidi katika ulimwengu wa siasa za Afrika hivi karibuni mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Januari 15, 2026 nchini Uganda.

Tume ya Uchaguzi ya Uganda imemtangaza Museveni (81) kuwa mshindi katika uchaguzi huo akipata asilimia 71.6 ya kura zote zilizopigwa, akimtupa mbali mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine aliyepata asilimia 24.72 ya kura.

Ushindi wa Museveni unampa nafasi ya kusalia madarakani kwa miaka mitano mingine hadi mwaka 2031 ambapo utafanyika uchaguzi mwingine nchini humo.

Licha ya kukaa madarakani kwa miongo minne tangu mwaka 1986 bado kiongozi huyo mkongwe barani Afrika atakabiliwa na changamoto ambazo zinaweza kuweka kizingiti katika kuiendesha nchi hiyo.

Nukta habari imefanya uchambuzi wa mambo matatu yanayomsubiri kiongozi huyo ikiwa ataapishwa rasmi na kuwa Rais wa Uganda.

Vijana ndio kundi kubwa linaloathirika na uosefu wa ajira nchini Uganda.Picha| Development Aid

Ajira kwa vijana 

Ukosefu wa ajira nchini Uganda ni miongoni mwa changamoto kubwa inayowakabili vijana suala linalowafanya baadhi yao kuibukia mataifa ya kigeni kutafuta unafuu wa maisha.

Licha ya nchi hiyo kuendelea kupiga hatua kubwa za kiuchumi Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2024 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu Uganda (Ubos) inabainisha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kilikuwa asilimia 12.3 na kuwaacha zaidi ya vijana milioni nne bila ajira.

Vijana hao wasio na ajira nchini Uganda ni wenye umri katika ya miaka 15 hadi 24 wenye uwezo wa kufanya ambao ni karibu nusu (asilimia 42) ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini humo.

Kupambana na rushwa

Kwa miaka kadhaa sasa Uganda imeendelea kukabiliana rushwa suala linalozorotesha huduma za kijamii pamoja na za kiuchumi..

Kwa mujibu wa ripoti ya viwango vya rushwa ya mwaka 2024 inayotolewa na Taasisi ya Transparent International viwango vya mapambano dhidi ya rushwa nchini Uganda vimefikia asilimia 26.

Kiwango hicho kilichorekodiwa Uganda kwa miaka minne  inaifanya nchi hiyo kushika mkia ikiwa nafasi ya 140 kati ya nchi 180 duniani zilizoorodheshwa katika ripoti hiyo.

Viwango hivyo vya rushwa Uganda ndio vya juu zaidi Afrika Mashariki ambapo Tanzania imerekodi asilimia  41, Kenya ikiwa 32 na Rwanda ikiwa na asilimia 57 kati ya 100. 

Kuimarisha mapato ya Serikali na utegemezi wa misaada

Uganda bado inategemea kwa kiasi kikubwa mapato ya nje na mikopo kufadhili bajeti yake ya Taifa, licha ya jitihada za kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani. 

Kwa mujibu wa takwimu za Serikali ya Uganda, mapato ya ndani huchangia takriban asilimia 60 ya bajeti, huku sehemu iliyobaki ikitokana na mikopo ya ndani na nje pamoja na misaada ya wahisani. 

Hali hii huenda ikaifanya Serikali ya Museveni kuwa katika hali  tete kifedha, hasusan nyakati za misukosuko ya kiuchumi duniani.

Malalamiko yanayomkabili Museveni

Mbali na changamoto za kiuchumi na kisiasa, Museveni anakabiliwa na malalamiko kuhusu ukandamizaji wa haki za upinzani na kuzimwa kwa kwa intaneti wakati wa uchaguzi kulikozuia mamia ya Wananchi wanaoitegemea kushindwa kufanya shughuli zao.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na diplomasia wa Efron Mkungilwa anasema kuwa kuzimwa kwa intaneti ni ishara ya udhaifu wa kisiasa na kukataa kusikiliza sauti za wananchi. 

“Kuzima internet huo ndio udhaifu wenyewe ambao umekuwa ukikoselewa kwa muda mrefu kwa sababu kama wewe ni bora, mahiri  unaweza ukaongoza basi unaweza kuacha watu wakazungumza na ukachukua maoni yao na ukayatendea kazi ,” amefafanua Mkungilwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks