Tanzania, Uganda kuimarisha ushirikiano maeneo ya kimkakati

February 7, 2026 3:54 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ujenzi wa mradi wa EACOP kukamilika Julai, 2026
  • Rais Samia, Museveni waahidi kuondoa vikwazo mipakani, kupannua masoko, ujenzi wa miundombinu ya usafiri majini, ardhini.

Arusha. Tanzania na Uganda zimefikia makubaliano ya kuendeleza ushirikiano katika maeneo ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa miradi ya nishati, uhuru, masoko, miundombinu, ulinzi na usalama suala litakalochochea ustawi wa nchi hizo mbili.

Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akizungumza na wanahabari  leo Februari 7, 2026 katika mapokezi ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni aliyepo ziarani nchini Tanzania amesema Watanzania wapo tayari kufanya kazi na Uganda akimshukuru kwa kufanya ziara hiyo nchini.

“Watanzania wapo tayari kufanya kazi bega kwa bega kwa ajili ya maendeleo ya nchi hizi mbili…Naomba mniunge mkono kumshukuru (Museveni) kufanya ziara hii, inaonesha anatoa umuhimu mkubwa sana kwa ajenda za ushikiano baina ya Uganda na Tanzania,” amesema Rais Samia.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.Picha/Ikulu.

Viongozi hao wa nchi hizo mbili zenye historia pana na mahusiano ya kindugu wamezungumzia kukamilika kwa ujenzi wa mabomba ya nishati ikiwemo  bomba la mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) ambalo linatarajiwa kukamilika Julai, 2026.

EACOP ni mradi unaohusisha ujenzi na uendeshaji wa bomba la mafuta lililofukiwa chini linalovuka mpaka kwa ajili ya kusafirisha mafuta ghafi kutoka Ziwa Albert nchini Uganda hadi pwani ya mashariki ya Tanzania kwa ajili ya kuuza nje kwenye masoko ya kimataifa.

Kukamilika kwa mradi huo wenye karibu miaka10 kunatarajiwa kutarahisisha usafirishaji wa mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania ukifungua fursa za ujenzi wa mambomba mengine mawili yatakayoendelea kutoa nafasi za ajira na kukuza uchumi.

“Tumezungumza mabomba mengine mawili, bomba la gesi kutoka Tanzania kupeleka Uganda na bomba la mafuta safi yatakayosafishwa Uganda kwenda huko yatakapouzwa tutatumia ushoroba huo huo,” amesema Rais Samia.

Pamoja na hayo Rais Samia amesema wamezungumza kuhusu kukamilisha ujenzi wa miradi ya reli, na usafiri wa majini pamoja na kuondoa vikwazo vya biashara maeneo ya mpakani.

Kwa upande wake Rais Museveni, amegusia mambo matatu muhimu waliyozungumza ikiwemo uhuru, masoko na usalama miongoni mwa nchi za Afrika.

“Kama unataka mafanikio zalisha huduma au bidhaa na uuze, suala la masoko ilikuwa ni sehemu ya ukombozi wa Afrika bila hiyo hakuna namna tunaweza kufanikiwa,” amesisitiza Museveni.

Museveni aliyechaguliwa tena kuwa Rais wa Uganda hivi karibuni anatarajiwa kumaliza ziara yake ya kikazi leo Februari 7, 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks