Elon Musk aunganisha xAI na SpaceX, utajiri wake wafika Dola bilioni 852
- Muunganiko huo unafanya kuzaliwa kwa kampuni ya binafsi yenye thamani kubwa zaidi duniani ikiwaacha mbali makampuni mengine shindani ya teknolojia kama vile Nvidia na OpenAI.
Dar es Salaam. Tajiri namba moja duniani Elon Musk ameunganisha kampuni yake ya roketi ya SpaceX na kampuni yake ya akili bandia (AI) na mitandao ya kijamii ya xAI na kufanya thamani ya kampuni hizo kufikia Dola za Marekani trilioni 1.25.
Kwa mujibu wa makadirio ya Jarida la Kimataifa la Biashara na Uchumi la Forbes, muungano wa kampuni hizo mbili umefanya ongezeko la thamani la karibu Dola za Marekani bilioni 200 ambapo kabla SpaceX ilikuwa na thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni 800 huku xAI ikikadiriwa kuwa na thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni 250.
Kuunganishwa kwa SpaceX na xAI kunafanya kuzaliwa kwa kampuni ya binafsi yenye thamani kubwa zaidi duniani na kuwaacha mbali makampuni mengine shindani ya teknolojia kama vile Nvidia na OpenAI.
Utajiri wake waongezeka
Mbali na kuongeza thamani ya kampuni, muungano huo pia umeongeza karibu Dola za Marekani bilioni 84 katika utajiri wa Musk anayemiliki asilimia 46 ya jumla ya hisa zote za SpaceX na asilimia 49 ya hisa za xAI.
Kwa mujibu wa makadirio ya Forbes, kwa sasa utajiri wa Musk umefikia thamani ya Dola za Marekani bilioni 852, sawa ongezeko la asilimia 11 kutoka utajiri wa Dola za Marekani bilioni 768 mwanzoni mwa mwaka 2026.

Uwekezaji katika sekta ya teknolojia hususan AI ndio chanzo kikuu cha utajiri wa Musk ambaye pia ni mmiliki wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter)
Musk alianza kushika orodha ya watu matajiri zaidi duniani mwaka 2021 licha ya panda shuka zinazomtoa ama kumrudisha katika nafasi hiyo kutokana na mabadiliko ya thamani ya hisa na mali zake.
Katika kipindi hiki ambacho hisa za makampuni kama BILL, American Express Global Business Travel na DigitalOcean zikiripotiwa kushuka kutokana na wasiwasi wa wawekezaji juu ya athari za teknolojia ya AI kwenye biashara na mapato ya kampuni, Musk amekuwa akionyesha ustadi katika kuendesha uwekezaji wake katika sekta ya teknolojia.
Kwa makadirio, utajiri wa Musk unaweza kufadhili bajeti yote ya Serikali ya Taifa la Afrika Kusini ambayo ni Randi 2.59 trillioni za Afrika Kusini (Dola za Marekani bilioni 135) kwa zaidi ya miaka sita.
Latest