CRDB yaripoti faida ya Sh724.6 bilioni 2025

February 3, 2026 7:16 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni sawa na ongezeko la asilimia 31.4 kutoka faida ya Sh551.5 bilioni iliyorekodiwa katika mwaka wa fedha unaoishia Desemba 2024.

Dar es Salaam. Benki ya Biashara ya CRDB imetangaza ongezeko la faida baada ya kodi la zaidi ya Sh173.1 bilioni ndani ya mwaka mmoja kufikia Sh724.6 bilioni katika mwaka wa fedha ulioishia Desemba 2025.

Faida hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 31.4 kutoka faida ya Sh551.5 bilioni iliyorekodiwa katika mwaka wa fedha ulioishia Desemba 2024.  Faida kabla ya kodi ya benki hiyo kubwa kwa thamani ya rasilimali, ilifikia Sh1 trilioni kutoka Sh778.8 bilioni iliyorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kiasi hicho cha faida ni kwa mara ya kwanza benki hiyo kukipata licha ya kuwepo kwenye soko la huduma za kifedha kwa tariban miaka 30.

Ongezeko hilo la faida kwa benki hiyo ni habari njema kwa wawekezaji wake ambao huenda wamekuwa wakisubiri kwa hamu kuongezeka kwa gawio ili kutunisha zaidi mifuko yao. 

NMB bado kinara wa mapato

CRDB si benki pekee ya biashara nchini iliyorekodi faida kubwa ya zaidi Sh500 bilioni. CRDB inachuana vikali na benki ya biashara ya NMB ambayo wiki iliyopita ilitangaza faida baada ya kodi ya Sh749.77 bilioni mwaka 2025. 

Kiwango hicho cha faida baada ya kodi cha NMB ni ongezeko la takribani asilimia 16 ikilinganishwa na Sh646.89 bilioni iliyorekodiwa mwaka 2024, jambo lililoifanya kuwa taasisi ya kwanza ya kibiashara ya fedha nchini kuripoti kiwango hicho cha faida.

Benki ya CRDB na NMB zimekuwa zikichangia kiasi kikubwa faida ya jumla ya sekta ambapo benki hizo mbili pekee zinawakilisha takriban asilimia 60 ya faida zote za benki nchini Tanzania mwaka 2025. 

Licha ya kwamba CRDB ni benki kubwa ya kibiashara kimali kulinganisha na benki nyingine, ikiwa na thamani ya jumla ya mali ya takribani Sh22.2 trilioni, bado imekuwa kwenye ushindani mkali na benki nyingine kwenye soko hususan NMB.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks