Deni la Serikali lazidi kupaa Tanzania likifikia Sh109 trilioni
- Ni sawa na ongezeko la asilimia 8.6 ndani ya mwaka mmoja.
- Mikopo ya nyuma iliyosainiwa yachangia ongezeko kubwa la deni hilo.
- Wachambuzi waeleza kuwa kukopa siyo shida, ishu ni matumizi yenye tija.
Dar es Salaam. Deni la Serikali ya Tanzania limeongezeka kwa takribani asilimia 8.6 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja hadi Sh109.01 trilioni Novemba mwaka jana likichochewa zaidi na mahitaji ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Ndani ya miaka 10 Serikali imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na bwawa la Julias Nyerere licha ya kuwepo presha ya kifedha kutokana na mapato ya ndani kutokidhi mahitaji yote ya kibajeti.
Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar, alisema bungeni Februari 2, 2026 kuwa hadi Novemba 2025, deni hilo limeongezeka kutoka kiwango cha Sh100.35 trilioni kilichoripotiwa Novemba 2024 kutokana na upokeaji wa mikopo mipya pamoja na mikopo iliyosainiwa miaka ya nyuma kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Kwa nyakati tofauti kumekuwa na mjadala mkubwa nchini juu ya kasi ya kuongezeka kwa deni la Serikali mwaka hadi mwaka huku baadhi ya wataalamu wa uchumi wakieleza kuwa mwenendo huo si rafiki kwa ukuaji wa uchumi.
Hata hivyo, Omar aliwaeleza wabunge wakati akiwasilisha miongozo ya maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha kati cha miaka mitatu (2026/27–2028/29) kuwa tathmini iliyofanyika Oktoba 2025 inaonesha kuwa deni la Serikali litaendelea kuwa himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.
Licha ya ongezeko hilo la deni la Serikali, Omar emeeleza kuwa Serikali inatarajia kukopa kwa wastani wa Sh15.5 trilioni kwa mwaka kutoka vyanzo vya ndani na nje katika kipindi cha muda wa kati.
Kwa mwaka wa fedha 2026/27 pekee, amesema Serikali inatarajia kukopa Sh15.24 trilioni, ambapo Sh7.4 trilioni zitatumika kugharamia miradi ya maendeleo na Sh7.8 trilioni zinatarajiwa katika ulipaji wa deni la Serikali.
Bajeti ya kihistoria yatangazwa
Pamoja na ongezeko la deni, Serikali imewasilisha bajeti kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini, ikipanga kutumia takribani Sh61.9 trilioni katika mwaka wa fedha 2026/27 ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kuimarisha rasilimali watu, pamoja na kukuza maendeleo ya kijamii na kimazingira.
Bajeti hiyo inaongezeka kwa Sh5.4 trilioni kutoka bajeti ya Sh56.49 trilioni iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2025/26 sawa na ongezeko la takriban asilimia 10 ndani ya mwaka mmoja.
Lengo kuu ni kujenga uchumi imara, shindani na jumuishi, huku ikitekeleza programu maalum zitakazobadilisha sekta muhimu za kiuchumi.
Kwa mwaka wa fedha 2026/27, mapato yanatarajiwa kufikia Sh46.69 trilioni, yakijumuisha mapato ya kodi ya Sh9 trilioni, mapato mengine Sh9.24 trilioni (ikiwemo Sh1.97 trilioni kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa), pamoja na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo yenye thamani ya Sh563.1 bilioni .
Kuongezeka kwa deni siyo tatizo, ishu matumizi
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema ongezeko la bajeti na deni linapaswa kutazamwa kwa muktadha wa matumizi yanayokusudiwa, hasa kama mikopo hiyo itaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo yenye tija.
Mkuu wa Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Prof Omari Mbura amesema ongezeko la deni la Serikali si jambo la ajabu kwani linazikumba hata mataifa makubwa kama Marekani ila jambo la msingi ni kuhakikisha fedha zilizokopwa zinatumika kwa malengo sahihi.
“Mikopo inayotumika kwenye miradi ya maendeleo huongeza uwezo wa uchumi kuzalisha mapato, lakini matumizi yasiyo na tija yanaweza kuwa mzigo mkubwa kwa taifa,” amesema Prof Mbura.
Mtaalamu wa uchumi kutoka Dar es Salaam, Paul Chengula ameiambia Nukta Habari kuwa kuimarika kwa mapato ya ndani kumeiwezesha Serikali kupanua bajeti bila kutegemea sana mikopo ya nje.
“Mapato ya ndani yanaendelea kuimarika na sasa yanachangia kwa kiwango kikubwa kugharamia bajeti, jambo linalopunguza utegemezi wa mikopo na misaada ya nje,” ameeleza Chengula.
Waziri Omar alieleza kuwa uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.3 mwaka 2026 kutoka asilimia 5.9 mwaka jana na katika muda wa kati unatazamiwa kukua kwa asilimia 6.9.
Latest