Wananchi watakavyonufaika na usambazaji wa umeme katika vitongoji 9,009

January 20, 2026 5:28 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema ni muhimu Serikali kuhakikisha inaweka gharama nafuu ili wananchi waweze kumudu huduma hiyo.

Dar es Salaam. Hivi karibuni, Serikali ya Tanzania imetia saini mikataba 30 yenye thamani ya Sh1.2 trilioni kwa ajili ya kusambaza umeme katika vitongoji 9,009, hatua inayolenga kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hususan katika maeneo ya vijijini.

Waziri wa Nishati na Madini, Deogratius Ndejembi aliyekuwa akizungumza katika hafla ya utiaji saini miradi hiyo January 18,2026 alisema mpaka kukamilika kwa miradi hiyo, takribani vitongoji 50,447 kati ya 64,359 vilivyopo nchini vitakuwa vimefikiwa na umeme.

Kupitia miradi hiyo ya ufikishwaji wa umeme maeneo ya pembezoni Watanzania 260,000 wanatarajiwa kunufaika na nishati hiyo baada ya kukamilika kwa usambazaji huo ndani ya miaka mitatu ijayo.

Zaidi ya idadi ya miradi hiyo ambayo inatarajiwa kutekelezwa katika mikoa 19, swali la msingi ni kwamba kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme ngazi ya vitongoji, kutawanufaisha vipi wakazi wa maeneo husika?

Umeme ni mhimili wa maendeleo

Mchambuzi wa masuala ya uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Alfred Kinyondo anasema kuwa kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme maeneo ya vijijini kutaongeza chachu ya maendeleo na ukuaji wa uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja.

Anafafanua kwamba uwepo wa umeme unaongeza fursa za uwekezaji kama vile viwanda, kuongezeka kwa makazi ya watu, pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya usafiri jambo ambalo huchochea uzalishaji wa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. 

“Watu wakisha ajiriwa, kutakuwa na mama lishe pembeni ambaye atakuwa anawauzia waajiriwa…kuna mtu pia atapangisha watu ambao waishi mbali na hawahitaji kutumia gharama kubwa za nauli kuja kazini,” amefafanua Profesa Kinyondo.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema ni muhimu Serikali kuhakikisha inaweka gharama nafuu ili wananchi waweze kumudu huduma hiyo. Picha | Mwananchi.

Mradi hiyo pia itaunganishwa katika vituo vya afya pamoja na shule zilizojengwa hivi karibuni hatua inayotajwa kuchangia upatikanaji wa huduma za kijamii na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Pamoja na kuunganisha umeme katika vitongoji ndejembi amebainisha kuwa upatikanaji wa umeme katika maeneo ya vijijini umefikia asilimia 70, huku vijiji 12,318 vikiwa tayari vimeunganishwa na huduma hiyo.

Gharama ni himilivu?

Profesa Kinyondo ameirai Serikali kuhakikisha umeme unaopelekwa vijijini unapatikana kwa gharama nafuu ili kuwawezesha wananchi kumudu gharama za kuunganishwa. 

“Mtu aliyeko kijijini inabidi awezeshwe ili asiwe tu mtazamaji wa huo umeme bali awe na uwezo wa kumudu kuuvuta na kuutumia,” amefafanua Profesa Kinyondo.

Wadau wanasema Serikali kuhakikisha umeme unaopelekwa vijijini unapatikana kwa gharama nafuu ili kuwawezesha wananchi kumudu gharama za kuunganishwa. Picha | Full Shangwe Blog.

Kwa mujibu wa mchambuzi huyo, gharama ya kuunganisha umeme ikiwa kubwa itasababisha wananchi wengi kushindwa kumudu gharama hatua itakayoitishwa mzigo mkubwa kwa Serikali kwenye gharama za uendeshaji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), gharama za wananchi kuunganishwa na huduma hiyo ni Sh27,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks