Serikali yaahidi kulinda uhuru wa Mahakama Tanzania
- Atoa angalizo kwa majaji na mahakimu kutokutumia uhuru huo bila uwajibika, utu na uadilifu.
- Asema Watanzania wana matumaini makubwa na majaji.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kulinda uhuru wa makama ili kuhakikisha uwepo wa usawa katika kutoa haki suala litakaloimarisha misingi ya kidemokrasia nchini.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), uliofanyika leo Januari 13, 2026, Jijini Dodoma, Rais Samia amesisitiza kuwa uhuru wa mhimili huo una manufaa pia kwa Wananchi.
“Uhuru wa Mahakama si tu haki ya majaji, bali ni haki ya wananchi. Serikali itaendelea kulinda uhuru huu, lakini kwa pamoja tunapaswa kuhakikisha haki inatendeka bila hofu, upendeleo wala rushwa,” amesema Rais Samia.
Kauli ya Rais Samia inayotilia mkazo uhuru wa mhimili huo inakuja wakati baadhi ya wadau wa demokrasia na siasa wamekuwa wakihoji uhuru wa mahimili huo katika utoaji wa maamuzi wa kesi mbalimbali.
Akiangazia suala hilo Rais Samia amebainisha kuwa uhuru wa mhimili huo haupaswi kutumika bila uwajibikaji, na kwamba uadilifu, nidhamu, utii wa sheria na uzalendo kwa Taifa ni sehemu ya vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika utendaji wa maafisa wa mahakama.
Maslahi ya watumishi wa mahakama yamulikwa
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju amesema licha ya Serikali kutoa bajeti kwa Mahakama kwa kiwango kikubwa mahitaji ya mhimili huo bado ni makubwa, hususan katika maeneo ya miundombinu, rasilimali watu na teknolojia ya kisasa, akisisitiza haja ya kuendelea kuimarisha uwekezaji katika sekta hiyo.
“Mheshimiwa Raisi la tatu ni makazi bora na usalama kwa ajili ya mahakimu na majaji Mheshimiwa Raisi tunashauri kwamba mahakimu na majaji wawezeshwe kuishi katika maeneo salama yenye hadhi kama ilivyokuwa zamani.
…Hali iliyopo sasa ambapo majaji na mahakimu wengi wanapanga nyumba binafsi inaweza kuathiri kiwango chao cha kuwa huru katika maamuzi kwa waliowapangisha,” amesema Jaji Masaju.
Akijibu hoja hiyo Rais Samia amesema Serikali inatambua changamoto zinazokabili mhimili huo akiahidi kuzitatua.
“Twendeni pole pole maendeleo ni hatua tumeanza hatua za awali na nyie mmeona tumechukua hatua kubwa sana za kuirekebisha au kuijengea heshima mahakama yetu kuwa mahakama inayoheshimika duniani sasa, safari ni hatua tutakwenda polepole nikisema hivyo sisemi kwamba hatutaangalia maslahi yenu lakini twendeni polepole,” ameeleza Rais Samia.