Tanzania mwenyeji mkutano wa mabunge duniani 2026
- Kufanyika kwa siku sita Oktoba, 2026 jijini Arusha.
- Rais Samia anatarajiwa kuwa mgeni Rasmi.
Arusha. Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) utakaofanyika jijini Arusha Oktoba 2026 ukitarajia kukutanisha zaidi ya wanachama 1,500 kutoka mataifa mbalimbali duniani
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Amos Makalla aliyekuwa akizungumza baada ya kuupokea ujumbe wa IPU leo Disemba 04, 2025 amesema sababu kubwa ya mkutano huo kufanyika nchini ni historia pana ya IPU na Tanzania ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
“Tanzania ni mwenyeji na sababu kubwa ni ushiriki na historia yake katika IPU na kikubwa zaidi ni namna wao wanavyoiona Tanzania na sisi tumewahakikishia tupo tayari kuwapa ushirikiano kufanikisha mkutano huo mkubwa wa Kihistoria.” Amesema Mhe. Makalla.
Pamoja na hayo, Makalla amesema mkutano huo utafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi wa jiji hilo hivyo amewataka wananchi kujiandaa vyema.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Amos Makalla (Katikati) akizungumza na wajumbe kutoka Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). ORC.
Mkutano huo wa siku sita utafanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania ikiwa ni miaka miwili tangu aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania Tulia Ackson achaguliwe kuwa rais wa umoja huo Oktoba 2023.
Pamoja na mambo mengine mkutano huo ambao hufanyika mara mbili kwa mwaka pia utachagua mwenyekiti mpya atakayeiongoza IPU kwa miaka mitatu ijayo baada ya uongozi wa wa Dk Tulia kukoma.
Ujumbe wa IPU uliotembelea Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Arusha leo umeongozwa na Balozi Ande Filip, Mkuu wa Kitengo cha Mabunge Wanachama na Mahusiano ya Nje, Makao Makuu ya IPU, Jijini Geneva, akiongozana na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa Geneva,Uswisi Dkt. Hoyce Temu.
Akizungumza kwa niaba ya maafisa wengine wa IPU Balozi Ande amesema washiriki wa mkutano huo watapata fursa za kufanya utalii kwa kutembelea maeneo ya kihistoria na vivutio vya utalii vilivyopo Arusha na maeneo mengine ya jirani.
Latest