NIDA kubadili bure vitambulisho vinavyofutika maandishi

November 27, 2025 6:21 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma kupitia vitambulisho hivyo bila usumbufu.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imetangaza kubadilisha bure vitambulisho vya taifa vilivyofutika maandishi ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma kupitia vitambulisho hivyo bila usumbufu.

Akizungumza leo Novemba 27, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, amesema wananchi wote wenye vitambulisho vilivyoanza kufifia maandishi wanapaswa kuvirejesha katika Ofisi za NIDA za wilaya ambapo watapatiwa vitambulisho vipya bila malipo.

Kaji amesema hatua hiyo inalenga kutatua changamoto iliyolalamikiwa na baadhi ya wananchi, ambao wengine wameshindwa kuvitumia vitambulisho vyao kutokana na vitambulisho hivyo kutosomeka kwa kufifia maandishi. 

“Tumekuja na suluhu ya vitambulisho vinavyofutika maandishi. Kama unacho, ukirudishe katika ofisi ya wilaya, unaandika jina na unasaini, na utapata kitambulisho kipya bila malipo,” amesema Kaji.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa utaratibu huo unawahusu tu wale ambao vitambulisho vyao vimeharibika kutokana na hitilafu ya kiufundi, na si kutokana na uzembe au uharibifu wa makusudi akisisitiza kuwa walioharibu vitambulisho hivyo kwa bahati mbaya au makusudi watalazimika kulipia gharama.

Wananchi wote wenye vitambulisho vilivyoanza kufifia maandishi wanapaswa kuvirejesha katika Ofisi za NIDA za wilaya ambapo watapatiwa vitambulisho vipya bila malipo. Picha | Diramakini

“Kuna wale walioviharibu mfano mtu alikalia kikavunjika, hao watalazimika kulipia gharama ya Sh 20,000 ya kutengeneza kitambulisho kipya,” amefafanua Kaji.

Aidha, Kaji amesema vitambulisho vya awali vilivyokuwa na ukomo wa muda havitakuwa tena na kikomo hicho huku akifafanua kuwa, kwa yeyote anayekereka na tarehe hiyo kuendelea kuonekana kwenye kitambulisho chake, atalazimika kulipia gharama ili kubadilishiwa kitambulisho kipya.

NIDA imetoa wito kwa wananchi kufika katika ofisi zao za wilaya kwa wakati, ili kuhakikisha wanapata vitambulisho sahihi na vyenye ubora unaotakiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks