Rais Samia amtaka Dk Mwigulu kutekeleza majukumu ya Serikali kwa kasi

November 14, 2025 1:15 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Majukumu hayo ni yale yaliyoainishwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM.

Arusha. Rais wa Tanzania Samia Suluhu amemuapisha Waziri Mkuu Mteule Dk Mwigulu Nchemba na kumuagiza kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa kasi kubwa ndani ya miaka mitano ijayo.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Novemba 14, 2025 katika hafla ya kumuapisha Dk Mwigulu Nchemba iliyofanyika Chamwino, Dodoma akibainisha kuwa muda wa miaka mitano uliopo ni mchache kulinganisha na ahadi walizoziahidi katika ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hivyo hana budi kutekekeza majukumu hayo kwa kasi kubwa.

“Hatuna budi kuongeza kasi katika utendaji wetu, utakwenda kusimamia Baraza la Mawaziri ambao nao wanaongoza sekta tofauti tofauti, ni wajibu wako kuhakikisha kasi ya utekelezaji wa yale tuliyoyapanga inaongezwa ili tuweze kuyatekeleza yote ndani ya muda mfupi,”amesema Rais Samia.

Maelekezo hayo ya Rais Samia yanaenda sambamba na ahadi ya waziri mkuu huyo mpya wakati akihutubia kwa mara ya kwanza mara tu baada ya kuthibitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania akiahidi kutumika kukidhi mahitaji ya Watanzania.

“Watumishi wa umma na Watanzania sote kwa ujumla lazima twende na spidi ya kupandia mlima, twende na gia ya kupita kwenye mawimbi, twende na gia ya kupita kwenye anga lenye mawingu, lazima chombo kifike salama na watu wake wafike salama,”lisema Dk Mwigulu Novemba 13,2025 Bungeni Dodoma.

Pamoja na hayo Rais Samia amemtaka Dk Nchemba kutekeleza majukumu yake kwa weledi kuepuka vishawishi kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki akibaonisha kuwa uteuzi wake ulikuwa na ushindiani mkubwa.

“Uteuzi  wako umepitia ushindani mkubwa na katika vigezo kadhaa, umeibuka na vigezo vingi kidogo kuliko wengine ulioshindana nao n vigezo vyote tumepima maeneo mbalimbali ya nchi yetu kubwa zaidi ni kuwatumikia Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…

…Kwa umri wako mzigo huu ni mkubwa, kwa umri wako vishawishi ni vingi vya marafiki ndugu, jamaa, nafasi yako ile haina rafiki, hina ndugu, haina jamaa ni nafasi ya kulitumikia Taifa la Tanzania,” amesisitiza Rais Samia.

Kwa uapisho huo Dk Mwigulu ambaye pia amewahi kuwa Waziri wa Fedha kwa awamu mbili zilizopita anakuwa Waziri Mkuu wa 12 akichukua nafasi ya Kassim Majaliwa aliyehudumu nafasi hiyo kwa miaka 10 iliyopita chini ya Rais wa awamu ya tano John Pombe Magufuli na baadae Rais Samia Suluhu baada ya mtangulizi wake kupoteza maisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks