Kishindo cha wanawake majimboni 2025
- Wanawake 558 wajitokeza kuwania ubunge majimboni kupitia vyama 18.
- Idadi yao inaongezeka kila mwaka huku wachambuzi wakisema elimu ya uraia na jinsia imesaidia.
Dar es Salaam. Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unashuhudia sauti ya mwanamke ikisikika zaidi katika medani ya siasa za Tanzania, baada ya kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za kuchaguliwa kuwa wabunge.
Ushiriki huo anaashiria kuwa juhudi za usawa wa kijinsia zinazaa matunda na kuongeza ajenda za wanawake katika Bunge la 13 la Tanzania litakaloanza mwaka huu.
Orodha za wagombea wa viti vya ubunge mwaka 2025 iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inaonyesha kuwa wanawake 558 wamejitokeza kuwania ubunge katika majimbo 272 kupitia vyama vyao vya siasa 18 vinavyoshiriki uchaguzi mwaka huu.
Wanawake hao 558 ni sehemu ya wagombea 1,735 waliopitishwa na INEC kuwania ubunge katika majimbo ya uchaguzi.
Hiyo ni sawa na kusema asilimia 32.2 au karibu theluthi moja ya wagombea wote wa ubunge mwaka huu ni wanawake, jambo linaloashiria mwanga katika kufikia malengo ya 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2030.

Idadi hiyo ya wanawake wanaogombea ubunge imeongezeka kutoka 293 ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 90.4 ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Licha ya ongezeko hilo, bado idadi ya wagombea ubunge wanawake iko chini ikilinganishwa na wanaume.
Mwaka 2020 wanawake waliogombea ubunge walikuwa asilimia 23.3 ya wagombea wote 1,257 waliojitokeza kuwania majimbo 264.
Matokeo yake wanawake 26 kati ya 293 walifanikiwa kupata viti vya ubunge kwa njia ya kupigiwa kura na wananchi. Je mwaka huu idadi itaongezeka? Tusibiri uamuzi wa wapiga kura Oktoba 29.
Vyama vyenye wagombea wengi wanawake
Uchambuzi wa orodha za wagombea wa viti vya ubunge mwaka 2025 iliyotolewa na INEC uliofanywa na Nukta Habari unaonyesha vyama vidogo ndio vimesimamisha wagombea wanawake wengi kuliko vyama vikubwa.
Ikumbukwe kuwa mwaka huu, vyama 18 kati ya 19 vinashiriki Uchaguzi Mkuu, huku Chadema kikosa sifa baada ya kutosaini kanuni za uchaguzi.
Chama cha Demokrasia Makini (MAKINI) kimeshika nafasi ya kwanza kwa kusimamisha wagombea ubunge wanawake 50 sawa asilimia 8.9 ya wagombea wanawake wote 558 au sawa na kusema kwa kila wagombea wanawake 100 basi takribani tisa wanatoka MAKINI.
MAKINI kimefuatiwa kwa karibu na chama cha National League of Democracy ambacho kina wagombea wanawake 42 na nafasi ya tatu imeshikwa na Chama Cha Kijamii (CCK) (40) na Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kwa wagombea 40.

Nafasi ya tano imeenda kwa chama cha Democratic Party chenye wagombea wanawake 38, Chama Cha Mapinduzi (CCM) (38), Civic United Front (CUF) (35), Alliance for African Farmers Party (AAFP) (33), ACT-Wazalendo (31), na National Reconstruction Alliance (NRA) kimesimamisha wagombea wanawake 30.
NCCR-Mageuzi ndio chama kilichosimamisha wagombea wanawake wachache zaidi miongoni mwa vyama 18. Wanawake 12 katika chama hicho ndio wanawania ubunge sawa na asilimia 2.2 ya wanawake wote waliojitokeza mwaka huu.
Hata katika idadi ya waliojiandikisha kupiga kura, wanawake wanafanya vizuri.
Kwa mujibu wa INEC, kati ya Watanzania milioni 37.6 walioandikishwa kupiga kura mwaka huu, milioni 18.9 (asilimia 50.3) ni wanawake.
Sababu za wanawake kujitokeza kugombea ubunge
Baadhi ya wataalam wa masuala ya uchaguzi na jinsia, wanaeleza kuwa elimu ya mpiga kura na usawa wa kijinsia imeongeza muamko wa wanawake kushiriki katika shughuli za maendeleo ikiwemo kutimiza haki yao ya kuchagua na kuchaguliwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dk Rose Reuben, katika mahojiano na Nukta Habari, ameeleza kuwa sera na mazingira ya kisiasa yameboreshwa, jambo ambalo limewapa wanawake ujasiri wa kushiriki katika siasa.
Amesema hatua hizo zimehakikisha kuwa siasa ni eneo salama kwa wanawake, na hivyo wengi wamevutiwa kuingia katika ulingo huo kwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
“Sera zimewaruhusu, mazingira yamewaruhusu. Nikizungumzia mazingira namanisha jamii imeanza kuelewa kuwa mwanamke ni kiongozi halali anayeweza kugombea na kuwania nafasi mbalimbali katika siasa,” anasema Dk Rose.

Dk. Rose anasema ili kuvutia wanawake wengi zaidi kushiriki kwenye siasa, ni muhimu kuboresha mazingira ya kidijitali ambako wanakumbana na ukatili wa kimtandao na kuimarisha jitihada za kuwajengea uwezo, kuongeza ujasiri na kuimarisha uongozi wao.
Akizungumzia sababu za vyama vya siasa vyenye ushawishi mdogo kuweka wagombea wengi wanawake, Dk Reuben amesema kuwa hali hiyo ni matokeo ya kuongezeka kwa uelewa kuhusu elimu ya jinsia na uongozi.
“Sidhani kama wanawake wanawekwa kwa sababu ni wanawake tu. Vyama vinawaweka kwa sababu vinaona uwezo wao wa uongozi. Wanawake hawa wameonyesha uwezo huo ndani ya vyama vyao, na hivyo wanaamini wanaweza kugombea na kushinda,” anasema Dk Rose.
Latest