Fahamu utaratibu wa watu wenye ulemavu kupiga kura Oktoba 29

October 28, 2025 10:04 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wanaruhusiwa kwenda na wasaidizi kwenye vituo vya kupigia kura.
  • INEC yaandaa vifaa maalum kuwawezesha kutimiza haki yao.

Arusha. Wakati Watanzania wakijiandaa kupiga kura ya kumchagua Rais, wabunge na madiwani Oktoba 29 mwaka huu, watu wenye ulemavu wameandaliwa utaratibu wa kisheria kuwawezesha kutimiza haki yao ya kikatiba.

Utaratibu huo ni pamoja na kupewa kipaumbele katika vituo vya kupigia kura na kwenda na wasaidizi wanaowaamini.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, watakaoruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi huo ni makundi mbalimbali ya watu waliotimiza umri wa miaka 18 na kujiandikisha katika daftari la kupiga kura.

Katikati ya makundi hayo lipo kundi la watu wenye wenye ulemavu wa aina mbalimbali ikiwemo wasioona, wasiosikia na walemavu wa viungo ambao wana haki ya kushiriki uchaguzi huo.

Tofauti na makundi mengine kundi hili hupewa kipaumbele zaidi kwa kuzingatia mahitaji yao muhimu ili kuongeza ujumuishi katika uchaguzi.

Takwimu za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) zilizotolewa hivi karibuni zinabainisha kuwa jumla ya watu wenye ulemavu 49,174 wanatarajia kushiriki katika uchaguzi utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.

Hivi ndivyo watakavyopiga kura

Utaratibu utakaotumika katika kupiga kura kwa watu wenye ulemavu umeanishwa katika Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 kifungu cha 84 (3), (b).

Sheria hiyo inaeleza kuwa mtu wenye mahitaji maalum ikiwemo wasiona anaruhusiwa kuomba usaidizi kwa mtu wake wa karibu ili aweze kupiga kura.

“Ikiwa mpiga kura hawezi kupiga kura kwa sababu ya ulemavu wa kutoona au sababu nyingine ya kimaumbile au hawezi kusoma, mpiga kura huyo anaweza kumuomba mtu atakayemchagua,” imeeleza sehemu ya sheria hiyo.

Sheria hiyo inaeleza zaidi kuwa msimamizi wa kituo, msimamizi msaidizi wa kituo, karani mwongozaji, mlinzi wa kituo au wakala wa upigaji kura hawatakiwi kutoa usaidizi kwa mpiga kura mwenye ulemavu.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, msaidizi anapaswa kuwa mmoja, isipokuwa pale ambapo katika kaya kutakuwa na mtu zaidi ya mmoja ambaye anahitaji msaada.

Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele amesema INEC imeandaa mikakati mingine ya kuwawezesha walemavu kupiga kura kwa faragha.

“Wenzetu wenye ulemavu wa viungo ambao hawawezi kusimama na kushindwa kutumia vituturi kama vilivyo, tume imeandaa vituturi ambavyo vikigeuzwa chini juu vitawawezesha watu wenye ulemavu wa viungo kupiga kura kwa faragha,” amesema Mwambegele.

Jaji Mwambegele alisema hayo Julai 31, 2025 alipokuwa akizungumza na wawakilishi wa watu wenye ulemavu jijini Dar es Salaam.

Mwambegele alibainisha kuwa mbali na usaidizi wa mtu wa karibu wasioona wataandaliwa karatasi maalum za maandishi ya nukta nundu ili kuwawezesha kusoma na kushiriki uchaguzi huo kirahisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks