Safari ya wanawake kugombea urais inavyoimarika Tanzania

October 27, 2025 4:34 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Uchaguzi wa mwaka huu wa 2025, wamejitokeza watatu wakivunja rekodi tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe 1992.
  • Idadi ya wanawake wanaogombea urais imekuwa ikiongezeka tangu 2015.

Dar es Salaam. Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka huu wa 2025 umevunja rekodi kwa kuwa na wanawake wengi wanaogombea nafasi ya urais tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe nchini 1992, jambo linalodhihirisha muamko wa kundi hilo kushiriki katika uongozi na maendeleo ya nchi. 

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), vyama vya siasa 17 kati ya 18 vinavyoshiriki uchaguzi wa mwaka huu, vimesimamisha wagombea urais. 

Chama cha ACT-Wazalendo, mgombea wake Luhaga Mpina aliwekewa pingamizi na hivyo hakuteuliwa na INEC kuwania nafsi hiyo huku Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakishiriki kabisa uchaguzi kwa sababu hakikusaini kanuni za uchaguzi.

Kati ya wagombea urais 17 watakaopigiwa kura na Watanzania Oktoba 29, 2025, watatu ni wanawake.  idadi ambayo ni ya juu tangu ufanyike uchaguzi wa vyama vingi  mwaka 1995. 

Wanawake wanaowania nafsi ya urais mwaka huu ni Rais Samia Suluhu Hassan kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM). Rais Samia aliingia madarakani mwaka 2021 baada ya kifo cha Rais John Magufuli wakati huo akiwa Makamu wa Rais. 

Saum Hussein Rashid anapeperusha bendera ya chama cha United Democratic Party ( UDP) ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho kwa sasa. Mwajuma Noty Mirambo wa Union for Multiparty Democracy (UMD). Mwajuma amekuwa akigombea udiwani na ubunge kwa nyakati tofauti kabla ya kujitosha katika nafasi ya juu kabisa ya urais. 

Ikiwa Watanzania watafanya uamuzi wa kumchagua mmoja kati yao, basi Tanzania itaandika historia wa kuongozwa na Rais wa kwanza mwanamke aliyechaguliwa kupitia sanduku la kura. 

Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan alipowasili Uwanja wa Kecha,Ilala Jijini Dar es Salaam kuendelea na mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu leo Oktoba 22, 2025. Picha | CCM.

Sio urais tu, wanataka pia na umakamu wa rais

Takwimu za INEC zinaonyesha kuwa vyama saba kati ya 17 vinavyowania urais  mwaka huu vimesimamisha wanawake katika nafasi ya mgombea mwenza wa Rais. Hii ni idadi ya juu kabisa ikilinganishwa na chaguzi zilizotangulia nchini Tanzania. 

Kwa nafasi zote mbili: urais na makamu wa rais, wanawake ni 10, jambo linaloonyesha mwanga kuhusu nafasi ya mwanamke katika uongozi. 

Mwaka wa kihistoria uliowaibua wanawake

Mwaka 2005 ulikuwa wa kihistoria katika siasa za vyama vingi nchini baada ya Chama Cha PPT Maendeleo kumsimamisha Anna Senkoro kugombea nafasi ya urais. 

Anna alikuwa mgombea pekee mwanamke akichuana na wagombea wanaume tisa ambao walipitishwa na Tume Huru ya Uchaguzi (NEC) kuwania nafasi hiyo. Alipata kura 18,783 sawa na asilimia 0.17 ya kura zote zilizopigwa akishika nafasi ya nane kati ya wagombea 10.

Licha ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kushinda nafasi hiyo, ushiriki wa Anna ulitoa hamasa zaidi kwa wanawake kujitosa kugombea nafasi za juu za uongozi. 

Ikumbukwe kuwa kabla ya hapo yaani katika uchaguzi wa 2000 na ule wa 1995 hakuna mwanamke aliyejitokeza kuwania nafsi ya urais. 

Uchaguzi uliofuata wa mwaka 2010, katika nafsi ya urais hakukuwa na mgombea mwanamke. Mwaka huo kulikuwa na wagombea sita akiwemo Rais mstaafu Kikwete ambaye alishinda. 

Wengine ni Profesa Ibrahim Lipumba wa chama cha Civic United Front (CUF), Dk Wilbroad Slaa wa Chadema , Mutamwega Mugahywa wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Peter Kuga Mziray wa APP Maendeleo, Hashim Rungwe wa NCCR-Mageuzi na Fahmi Dovutwa wa chama cha UPDP.

Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha United Democratic Party (UDP), Saum Hussein Rashid katika mkutano wa kampeni mjini Bunda. Picha | Mazingira FM.

Upepo ulivyoanza kubadilika

Hamasa ya wanawake kugombea nafasi za juu za uongozi ilizidi kuimarika katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 ambapo Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo alikuwa ni mwanamke pekee aliyejitokeza kugombea nafsi hiyo. 

Licha ya kuwa ACT-Wazalendo kuwa chama kichanga wakati huo, Anna alichuana na wagombea wengine saba katika uchaguzi huo uliomuweka madarakani Hayati Rais John Magufuli.  

Katika nafsi ya Makamu wa Rais, walijitokeza wanawake wawili: Samia Suluhu Hassan kutoka CCM na Leticia Msuya ambaye alikiwakilisha chama cha Tanzania Labour Party (TLP). 

Uchaguzi uliofuata wa 2020, idadi ya wanawake wanaowania urais ikaongezeka hadi wawili kati ya wagombea 15 waliojitokeza mwaka huo. 

Queen Sendiga kutoka chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara na Cecilia Mwanga kutoka chama cha Demokrasia Makini waliwania nafsi hiyo. 

Pia katika nafsi ya mgombea mwenza wa urais, CCM ilimsimamisha Rais Samia huku Satia Musa Bebwa akiiwakilisha Sauti ya Umma (SAU), kabla rekodi haijavunjwa mwaka huu kwa wanawake saba kuwania nafasi hiyo. 

Hii ni hatua kubwa katika harakati za kumkomboa mwanamke na kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwepo katika nafasi za uongozi ili kutoa fursa katika kundi hilo kuchangia katika shughuli za maendeleo. 

Miaka 30 iliyopita, katika Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Wanawake, viongozi kutoka mataifa 189 na zaidi ya wanaharakati 30,000 walikutana na kutengeneza na kupitisha mpango wenye dira ya kufanikisha haki sawa kwa wanawake na wasichana. 

Mpango huo ulitambuliwa kama Azimio la Beijing na Jukwaa la Hatua za Utekelezaji lililopitishwa mwaka 1995 imekuwa ni nyaraka iliyoidhinishwa zaidi duniani kuhusu ajenda ya haki za wanawake.

Hata hivyo, safari bado ni ndefu kutoa hamasa kwa wanawake wengi zaidi kugombea nafasi za uongozi ili kufikia malengo ya 50 kwa 50 ifikapo mwaka 20230.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks