TRC yarejesha safari za treni za SGR
- Ni baada ya kukamilika kwa matengenezo ya mufa mfupi yaliyofanyika.
Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limerejesha safari za treni za umeme za SGR, baada ya kusitisha kwa muda leo.
Hatua hiyo imekuja baada ya matengenezo ya muda mfupi yaliyofanyika, kutokana na treni ya Electric Multiple Unit – EMU maarufu mchongoko iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma leo Alhamisi Oktoba 23, 2025 kupata ajali katika kituo cha Ruvu mkoani Pwani.
Taarifa kwa umma iliyotolewa mchana huu na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC, Fredy Mwanjala imeeleza kuwa safari sasa zinaendelea kama kawaida.
“Shirika la Reli Tanzania linapenda kuujulisha umma kuwa huduma za usafiri wa treni za SGR zimerejea na kuendelea kama kawaida. Shirika linaomba radhi wateja wake kwa usumbufu uliojitokeza na pia linawashukuru kwa uvumilivu wao.
Huduma bora kwa wateja wetu ndiyo kipaumbele cha Shirika,” imeeleza taarifa hiyo.
Awali taarifa iliyotolewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa umma ilitaja chanzo cha awali cha ajali hiyo kuwa ni hitilafu za kiuendeshaji.
Hata hivyo, hakuna kifo kilichoripotiwa kutokana na ajali hiyo.
Treni ya mchongoko, ambayo imekuwa ikifanya safari zake kutoka Dar es Salaam, Morogoro hadi Dodoma ilianza kutoa huduma Novemba Mosi, mwaka 2024.
Hii ni ajali ya kwanza iliyohusisha mabehewa matatu kuhama nje ya reli, awali zilikuwa zikiripotiwa hitilafu zinazodaiwa kuwa za umeme ambapo safari zilikuwa zikisimama kupisha matengenezo na kisha safari kuendelea.
Latest



