Tanzania yalaani ukiukwaji Sheria za Kimataifa, yataka ushirikiano wa haki Afrika

September 26, 2025 11:54 am · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Dk. Mpango asema Afrika inahitaji ushirikiano utakao nufaisha pande zote katika matumizi ya rasilimali zake.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Philip Mpango amesema Tanzania inalaani kuibuka upya kwa ukiukwaji wa sheria za kimataifa ikiwemo matumizi ya nguvu kama njia ya kutatua migogoro.

Kwa mujibu wa Dk Mpango hali hiyo inachangia ukatili uliokithiri kwa binadamu hususani watoto, wanawake, wazee pamoja na wagonjwa katika maeneo yenye migogoro.

Dk Mpango aliyekuwa akihutubia katika Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) amesema vitendo vya baadhi ya mataifa kuwa na matumizi mabaya ya nguvu za kijeshi na kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kukomesha umwagaji damu unaoendelea katika maeneo mbalimbali duniani ni jambo lisilokubalika.

“Tanzania inasimama bega kwa bega na wananchi ambao wanaendelea kunyimwa haki za msingi za uhuru, mamlaka kamili ya kitaifa na haki ya kujitawala. Vilevile, inalaani vikali aina zote za ugaidi unaotekelezwa ndani au kuvuka mipaka ya mataifa,” amesema Dk Mpango akiwa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York nchini Marekani.

Kwa sasa Jumuiya ya kimataifa inaendelea kugawanyika kutokana na migogoro inayoendelea katika pembe tofauti za ulimwengu, ukiwemo wa Israel na Gaza ambapo maamuzi ya baadhi ya mataifa kuitambua rasmi Palestina kama nchi huru umeonekana kuikwaza Israel na mshirika wake wa karibu Marekani.

Aidha, Dk Mpango ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutambua ongezeko la matumizi ya fedha katika masuala ya kijeshi ikiwemo utafiti na utengenezaji wa silaha kama jambo la kusikitisha na lisiloendana na maadili ya kimataifa.

Dk Mpango amesema hali hiyo inazuia jitihada za kutafuta amani duniani, na inachukua kiasi kikubwa cha rasilimali ambazo zingeweza kutumika kuendeleza maendeleo endelevu na ustawi kwa wanadamu wote.

Hata hivyo, Dk Mpango ambaye alimwakilisha Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo amesema mitizamo ya kibeberu kuhusu Afrika inapaswa kumalizika.

Miongoni mwa mitizamo ya kibeberu ambayo Dk Mpango amesema inapaswa kuisha ni pamoja na ile ya kuichukulia Afrika kuwa sehemu ya kuchukua rasilimali, kupora ardhi, na unyonyaji wa maliasili za Afrika.

“Afrika inahitaji ushirikiano utakao nufaisha pande zote ‘win-win’ katika matumizi ya rasilimali zake,” amesema Dk Mpango.

Aidha, amesema dunia inapaswa kuendelea kutafuta amani bila kuchoka kwa kuwa ndio sharti la maendeleo ya kijamii na kiuchumi akipongeza juhudi za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa dunia, na mashirika ambayo yanashiriki kikamilifu katika upatanishi na utatuzi wa migogoro katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan, Urusi, Ukraine, na Mashariki ya Kati. 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilianzishwa mwaka 1945 baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia na ni miongoni mwa vyombo sita vikuu vya Umoja huo, likihusisha wanachama 193. 

Baraza hilo hupokea hoja mbalimbali za kimataifa zikiwemo amani na usalama, maendeleo, haki za binadamu na sheria za kimataifa.

Mwaka huu kikao hicho kimefanyika kikiwa na kauli mbiu inayosema “Miaka 80 na zaidi, kwa amani, maendeleo na haki za binadamu”, ikisisitiza mshikamano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo huku ikilinda mafanikio yaliyopatikana katika miongo minane iliyopita.

Ushiriki wa Tanzania katika UNGA unaendeleza historia yake ya kuchochea mjadala wa masuala muhimu ya bara la Afrika ikiwemo maendeleo endelevu, haki za binadamu, upunguzaji wa umasikini, amani na mshikamano wa kikanda.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW