Ifahamu miji 5 bora kwa utalii Afrika
- Ni pamoja na Cape Town, Marrakesh, Cairo, Nairobi na Zanzibar.
Dar es Salaam. Afrika ni miongoni mwa bara lililobarikiwa miji yenye vivutio vingi kulinganisha na sehemu nyingine.
Miongoni mwa vivutio hivyo ni fukwe za kuvutia, mbuga za wanyama na urithi wa kihistoria, sambamba na hilo miji kadhaa imekuwa kitovu kikubwa cha utalii kutokana na mchanganyiko wa mandhari ya kuvutia, tamaduni nzuri na huduma bora kwa wageni.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani(UN Tourism) inaeleza kuwa Bara la Afrika limeweka rekodi ya kuingiza watalii bilioni 1.4 kwa mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 11% kulinganisha na 2023.
Makala haya yanakuletea miji mitano bora barani Afrika inayopaswa kuwa kwenye orodha yako ya safari ijayo Kwa mujibu wa ripoti na mapendekezo ya taasisi mbalimbali za kitalii ikiwemo Discover Afrika na SafariBooking.
1. Zanzibar,[Stone Town] Tanzania
Stone Town ni mji wa kihistoria uliotambuliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa( UNESCO) kama urithi wa dunia, hapa ndipo makutano ya tamaduni za Kiswahili, Kiarabu, Kihindi na Ulaya zilizotengeneza mandhali ya kipekee.
Watalii wanaovutiwa na historia hufurahia kuona majengo ya kale, milango ya kale yenye uchoraji wa pekee na House of Wonders [Jumba la Maajabu].
Mbali na historia, Zanzibar inajulikana kama [Spice Island] kisiwa cha viungo kutokana na mashamba yake ya viungo, kama karafuu na vinginevyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa Zanzibar Dk Khalid Salum Mohammed amesema kuwa zaidi ya watalii 600,000 wametembelea Zanzibar kwa mwaka 2024 huku ikitarajiwa kupokea watalii 800,000.

2. Nairobi, Kenya.
Nairobi imepata umaarufu na kuitwa kitovu cha safari Afrika (Safari Capital of Africa kwa nafasi yake ya kipekee kwenye mbuga za wanyama.
Ni mji pekee unaojulikana kwa uwepo wa hifadhi ya Taifa kongwe nchini Kenya ambapo Simba, Twiga, Faru na aina mbalimbali za ndege wanaweza kuonekana kwa urahisi huku mandhari ya majengo makubwa ya jiji yakiwa karibu.
Mbali na hilo watalii hupenda kutembelea Girrafe Center, kituo cha David Sheldrick Elephant Orphanage na Karen Blixen Museum ambayo ina historia ya waandishi maarufu wa kitabu cha Out of Afrika.
Ripoti ya Waziri wa utalii na Wanyamapori nchini Kenya Rebecca Miano ya mwaka 2024 inaeleza kuwa nchi hiyo imeingiza watalii wa kigeni milioni 2.4 sawa na ongezeko la asilimia 15 ikilinganishwa na watalii waliotembelea kenya mwaka 2023.

3. Cairo, Misri
Cairo ni moja ya miji mikubwa na ya zamani zaidi barani Afrika, na inachukuliwa kama lango la kuingia katika historia ya ustaarabu wa kale wa Misri.
Miongoni mwa vivutio vikuu ni Piramidi na Sphinx ya Giza , ambazo ni kati ya maajabu ya dunia ya kale.
Wageni pia huvutiwa na makumbusho ya kifarao lililojaa maelfu ya hazina ya kale, pamoja na soko la Khan El- Khalili Bazaar linalouza bidhaa za kipekee kama vito, mitandio na viungo.
4 .Marrakesh, Moroko
Marrakesh ama maarufu kama Red City, ni kitovu cha historia na utamaduni wa kiarabu na kiafrika.
Mji huu una sifa kubwa kwa mchanganyiko wa usanifu wa kale na huduma za kisasa.
Uzuri wa mji huu ni uwepo wa Medina ya Marrakesh iliyohifadhiwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ambapo ni kivutio kikuu chenye mitaa midogo yenye msongamano wa maduka.
Vivutio vingine ni pamoja na Majorelle Garden, bustani yenye mimea adimu na rangi za kupendeza.
Nje ya jiji wageni wanaweza kufurahia milima ya Atlas, Bonde la Ourika na safari kuelekea jangwa la Sahara.

5 .Cape Town, Afrika ya Kusini
Cape Town umekuwa mji maarufu barani Afrika kutokana na mchanganyiko wake wa Milima, Bahari na usanifu wa sanaa.
Mji huu uko mwishoni wa Bara la Afrika, na unapakana na Bahari ya Atlantiki na Hindi, jambo linaloufanya uwe na mandhali ya kipekee.
Kulingana na Shirika la utalii duniani, sekta ya utalii nchini Afrika Kusini inachangia ZAR bilioni 102 katika pato la taifa la Afrika Kusini sawa na asilimia 10.3 ya nafasi za kazi nchini.
Vivutio vya mji huu ni pamoja na Table Mountain, kisiwa cha Robben ambacho kipo kwenye orodha ya urithi wa dunia chini ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifaa UNESCO) ambacho umaarufu wake utanotokana na kumfunga Baba wa Taifa la Afrika ya Kusini Nelson Mandela.

Latest