Milima 10 mirefu zaidi duniani
- Ni pamoja na Mlima Puncak Jaya, Vinscon Massif pamoja na Mlima Kilimanjaro.
Dar es Salaam. Milima ni mojawapo ya vivutio vya kijiografia duniani, baadhi ya nchi zimebahatika kuwa na vivutio hivi vinavyovutia mamia ya watalii kila mwaka na kuzinufaisha kiuchumi na kijamii.
Pamoja na kuwa kivutio cha utalii milima hutumika kama sehemu ya mazoezi na kuboresha afya huku baadhi ya watu hutafsiri kufika katika vilele vya milima waliyoipanda kama mwanzo mpya wa maisha yao au funzo la uvumilivu wa changamoto yoyote watakayokabiliana nayo maishani.
Kutokana na umuhimu wa kivutio hicho, Nukta Habari imefanya uchambuzi wa milima kumi mirefu zaidi duniani, unayoweza kuitembelea na kunufaika nayo kwa kurejea orodha iliyochapishwa na Kamusi ya Kiswahili inayotolewa na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) toleo la tatu.
10. Puncak Jaya
Mlima huu mrefu una mita 4,884 sawa na futi 16,023.6 juu ya usawa wa bahari kwenye kisiwa cha Guinea Mpya ( Papua New Guinea) katika nchi ya Indonesia.
Puncak Jaya ndio mlima pekee mrefu uliopo kwenye kisiwa na ndio mlima mrefu zaidi nchini Indonesia na unatajwa kuwa ni miongoni mwa milima migumu kuipanda kutokana na jiografia yake ya miamba licha ya kuwa unaweza kupandika misimu yote ya mwaka.
Awali ulikuwa ukiitwa Irian Jaya hadi mwaka 2005 ulipobadilishwa jina kuendana na mahali ulipo yaani kisiwa cha Guinea Mpya kilichopo Papua amnacho ndio kisiwa cha pili kwa ukubwa duniani.
9. Vinscon Massif
Ni mlima mrefu kuliko yote katika Bara la Antaktika wenye urefu wa mita 4,892 sawa na futi 16049.8 juu ya usawa wa bahari.
Unatajwa kama miongoni mwa milima saba yenye vilele vya juu (High peak) licha ya kuwa haujagunduliwa muda mrefu sana.
Kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya jiografia ya Nat Geo, mlima huu uligunduliwa na rubani wa ndege wa Marekani mwaka 1930 na ulianza kupandwa mwaka 1960 ambapo mwaka 1967 ndio wapandaji walifanikiwa kufika kileleni kwa mara ya kwanza.
Wapandaji wa mlima huu mara nyingi hupanda wakati wa Desemba na Januari kipindi cha majira ya kiangazi ambapo jua huwa likiangaza masaa 24 kwa siku, kutokana na uwepo wa baridi kali katika eneo jambo linalosababisha kuwepo na changamoto kuupanda mlima huo misimu yote ya mwaka.
8. Picode Orizaba
Hujulikana pia kama ‘Citlaltepetl’, ni miongoni mwa milima mirefu iliyopo Amerika ya Kaskazini ambapo wenyewe ni wa tatu ukiwa na urefu wa mita 5,636 sawa futi 18490.8 juu ya usawa wa bahari.
Mlima huu uliopo nchini Mexico ulipata jina la ‘Citlaltépetl’, ambalo linamaanisha “mlima wa nyota” kwa lugha ya ‘Nahuatl’, kutoka kwa wenyeji wa kiasili wa eneo hilo.
Changamoto kubwa ya kuupanda mlima huo ni hali ya baridi kali iliyopo eneo hilo hivyo wapandaji wanashauriwa kupanda msimu wa kiangazi ambao kiwango cha baridi hupungua kidogo.
7. Elbrus
Mlima Elbrus una urefu wa mita 5,642 sawa na mita 18510.4 ambao unaopatikana kiasi barani Ulaya na kiasi barani Asia katika Kusini mwa nchi ya Urusi.
Aidha, mlima huu ni sehemu ya milima ya ‘Caucasus’, ambayo inajumuisha mpaka kati ya Ulaya na Asia ambapo unatajwa kuwa ndio mlima mrefu zaidi nchini humo.
Ni miongoni mwa milima iliyogundulika zamani, kwa mujibu wa Nat Geo mlima huo wa volkano mfu una zaidi ya miaka milioni 2.5 ukiwa na umbile la mbegu za mti wa paini.
Upandaji wake si mgumu sana kulinganisha na milima mingine sita mirefu zaidi duniani kutokana na uwepo wa mashine zinazoweza kuwainua wapandaji wa mlima mpaka usawa wa futi 12,000.
6. Pico Cristobal Colon
Ndio mlima mrefu zaidi nchini Colombia ambapo una urefu wa mita 5,700 sawa na futi 18700.7 juu ya usawa wa bahari unaopatikana katika bara la Amerika ya Kusini.
Mlima huu ni mlima wa volkano ambao umepewa jina la Christopher Columbus kutokana na heshima yake kama mpelelezi maarufu wa Ulaya.
5. Logan
Logan ndio mlima mrefu zaidi nchini Canada na wa pili kwa urefu baada ya Mlima Denali katika bara la Amerika Kaskazini unaopatikana kaskazini mwa Jimbo la Yukon.
Urefu wake unafikia mita 5,959 sawa na futi 19550.5 juu ya usawa wa bahari na uko katika Milima ya Saint Elias, eneo la mpaka kati ya Canada na Marekani.
Mlima Logan ulipewa jina la Sir William Edmond Logan, ambaye alikuwa mtaalamu wa jiolojia na mchoraji wa ramani kutoka Kanada na alijulikana kwa mchango wake mkubwa katika utafiti wa jiolojia.
4. Kilimanjaro
Ndio mlima mrefu zaidi barani Afrika na moja ya mlima maarufu duniani. Una urefu wa mita 5,895 sawa na futi 19340.5 juu ya usawa wa bahari uliopo Mkoa wa Kilimanjaro Kaskazini Mashariki mwa Tanzania.
Kilimanjaro ni aina ya mlima wa volkano, ambao umepasuka kutoka kwenye kilele kilichozungukwa na miinuko ambayo ni kibo, mawenzi na shira.
Madhari yake ya kuvutia inajumuisha maeneo ya barafu, misitu, savanna pamoja na zaidi ya aina 2,000 za maua yanayostawi katika eneo hilo huku njia maarufu zitumiwazo kupanda mlima huu ni pamoja na Marangu, Machame, Lemosho na Rongai.
Kupanda Mlima Kilimanjaro mara nyingi kunachukua siku 5 hadi 9 kutokana na hali ya hewa ya baridi aidha, ingawa njia zote zinahitaji maandalizi na usimamizi wa wasaidizi maalumu.
3. Aconcagua
Mlima Aconcagua ni mlima mrefu zaidi nchini Argentina katika bara la Amerika ya Kusini huku ukiwa mlima wa pili kwa urefu nyuma ya milima ya Himalaya ukiwa na urefu wa mita 6,960.8 sawa na futi 22837.27.
2. Godwin Austen
Mlima huu pia unajulikana kama K2, ni mlima wa pili kwa urefu duniani baada ya Mlima Everest.
Urefu wake unafikia mita 8,611 sawa na futi 28251.31 juu ya usawa wa bahari katika milima ya Karakoram kwenye mpaka kati ya Pakistan na China, karibu na eneo la Gilgit-Baltistan nchini Pakistan na eneo la Xinjiang nchini China.
Kupanda K2 mara nyingi kunahitaji maandalizi ya kina, ujuzi wa hali ya juu na uzoefu wa kupanda milima ya juu.
Jina la mlima huu lilitolewa kwa ajili ya kumuenzi Kanali Henry Haversham Godwin-Auste mwanajiolojia wa Uingereza ambaye alitumia muda mwingi wa maisha yake kutafiti katika eneo hilo.
1. Mlima Everest.
Huu ndio mlima mrefu zaidi duniani, ukiwa na urefu wa mita 8,848 sawa na futi 29028.87 juu ya usawa wa bahari ambao upo katika safu ya milima ya Himalaya, kwenye mpaka kati ya nchi ya Nepal na Tibet.
Mlima Everest unaojulikana pia kama Sagarmatha nchini Nepal na Chomolungma nchini Tibet. Ni mlima mrefu zaidi duniani, ukiwa na urefu wa mita 8,848 kutoka ya usawa wa bahari. Mlima huu unavutia watalii kutoka kila pembe ya dunia, na ni alama ya changamoto, ujasiri na maajabu ya asili.
Jina “Sagarmatha” linatokana na lugha ya Kinepali. “Sagar” maana yake ni anga au mbingu, na “Matha” likiwa ni neno linalomaanisha “paji la uso”. Kwa pamoja, maneno haya yanamaanisha “Paji la Uso la Anga.” Jina hili linaashiria urefu na ukubwa wa mlima huu unaogusa mawingu.
Kwa upande wa Tibet, mlima huu unajulikana kama “Chomolungma,” ambalo linamaanisha “Mama wa Dunia.” Hii inaonyesha jinsi mlima huu unavyoheshimiwa na wenyeji wa Tibet kama sehemu takatifu na muhimu sana kiutamaduni.
Mlima huu ulipewa jina la “Mlima Everest” na mwanajiografia wa Uingereza Sir Andrew Waugh, ambaye alikuwa Mhakiki Mkuu wa India (Surveyor General of India) wakati huo.
Sir Waugh aliamua kuupa mlima huo jina la mtangulizi wake, Sir George Everest, ambaye alikuwa Mhakiki Mkuu wa India kabla yake. Sir George Everest alitoa mchango mkubwa katika upimaji na uchoraji wa ramani za Himalaya.