Majaliwa awataka madereva magari ya Serikali kutunza siri
- Ni pamoja na kutosema hadharani mambo wanayoyashuhudia au kuyasikia wakiwa kazini.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka madereva wa magari ya Serikali kuhakikisha wanatunza siri za Serikali pamoja na viongozi wanaowaendesha, akisisitiza kuwa ni wajibu wao kutosema hadharani mambo wanayoyashuhudia au kuyasikia wakiwa kazini.
Waziri Mkuu Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo Septemba 2 katika kongamano la nne la madereva wa Serikali Tanzania lililofanyika jijini Dodoma, amesema madereva wanapaswa kuwa waadilifu kwa kutunza siri za viongozi wao, ikiwemo maongezi ya simu wanayoyasikia.
“Nyie ni watu muhimu sana, lakini kwa umuhimu huu, mtambue kwamba nyie ni watu ambao mnapaswa kuwa nambari moja katika kutunza siri za Serikali,” amesisitiza Majaliwa.

Aidha, amewataka madereva kuongeza weledi katika kazi kwa kuzingatia usafi hasa katika mavazi, kufanya ukaguzi wa magari kabla ya safari, kujaza kumbukumbu za safari na kutoa taarifa inapohitajika magari yanapopata hitilafu.
Aidha, Majaliwa amewataka madereva kutoendesha magari yanapokuwa mabovu hata kama watalazimishwa na waajiri wao.
“Mwambie mwajiri wako huwezi kuendesha , kwa sababu gari kwa mujibu wa teknolojia ya sasa, inahitaji ifanyiwe ukarabati,” amesema Majaliwa.
Hata hivyo, Majaliwa amewataka madereva kutotumia namba feki za magari pamoja na kujiwekea ving’ora au vimulimuli katika magari ambayo hayana ruhusa , kuwa makini wakati wa kuendesha na kuepuka matumizi ya vilevi wawapo safarini.
Mara kadhaa madereva wa Serikali wamekuwa wakilalamikiwa na wadau kwa kukiuka sheria za barabarani ikiwemo kuendesha kwa kasi hata katika maeneo ambayo kiwango cha mwendo kimedhibitiwa.