Vodacom yafanya AGM mapato yakivuka Sh1.5 trilioni

August 22, 2025 10:41 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Faida baada ya kodi ya ongezeko kwa asilimia 69.4 hadi Sh90.5 bilioni ndani ya mwaka mmoja.

Dar es Salaam. Kampuni ya Mawasiliano na Teknolojia ya Vodacom Tanzania PLC imefanya mkutano wake wa wanahisa kwa mwaka ulioishia Machi 2025 huku ikiripoti ukuaji imara wa kifedha ikiwemo kuongezeka mapato ya huduma kwa asilimia 20.5 hadi Sh1.5 trilioni. 

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Agosti 21, 2025 ongezeko la mapato ya huduma lilichochewa zaidi na kuongezeka wateja na matumizi ya huduma hasa M-Pesa na data.

Matokeo ya kifedha ya Vodacom kwa mwaka ulioishia Machi 2025 ni bora zaidi ya mwaka uliopita baada ya kuripoti ongezeko la asilimia 69.4 ya faida baada ya kodi kufikia Sh90.5 bilioni, ikichangiwa na mikakati ya kupunguza gharama iliyookoa Sh59 bilioni.

Mapato ya jumla ya Vodacom yalifikia Sh1.54 trilioni kwa mwaka ulioishia Machi 2025 kutoka takriban Sh1.3 mwaka ulioishia Machi 2024, kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2025.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa Vodacom iliongeza wateja wapya milioni  tatu na kuifanya kuwa na wateja milioni 22.6 mwishoni mwa mwaka.

Vodacom, kwa mujibu wa uchambuzi wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za robo iliyoishia Juni 2025, inaongoza nchini kwa kuwa na watumiaji wengi wa huduma za simu, akaunti nyingi za huduma za kifedha kupitia simu na watumiaji wa intaneti. 

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Vodacom Tanzania, David Tarimo (katikati), Mkurugenzi Mtendaji, Philip Besiimire (kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Hilda Bujiku (kulia), wakizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wakati wakitangaza matokeo ya kifedha ya mwaka wa fedha 2025 yaliyobainisha ukuaji wa mapato na faida. Tukio hilo limefanyika tarehe 21 Agosti kwenye Makao makuu ya Vodacom Dar es Salaam. Picha|Hisani.

Minara mipya 471 ya 4G yajengwa

Miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la watumiaji wa huduma za simu ziikiwemo simujanja (smartphones), simu benki, na intaneti jambo linalochagiza safari ya uchumi wa kidijitali Tanzania.

Katika mkutano huo, Vodacom imewaeleza wanahisa wake kuwa mapato ya M-Pesa yaliongezeka kwa asilimia 29.3, huku thamani ya miamala ikiongezeka kwa asilimia 33.8 mwaka hadi mwaka. 

Vodacom imesema kuwa matumizi ya simujanja ndani ya mtandaoni huo yaliongezeka kwa asilimia 33.4 huku ikijenga minara mipya 471 ya 4G ikiwemo 126 katika maeneo ya pembezoni kwa kushirikiana na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano Sawa kwa Wote (UCSAF), hatua itakayochochea upatikanaji wa huduma za kidijitali. 

Nguzo nyingine ya ukuaji huo wa Vodacom ilikua mapato ya data ya simu, yaliyoongezeka kwa asilimia 21.6, yakichangiwa na matumizi ya simujanja na uwekezaji katika miundombinu ya mtandao.

“Utendaji wetu mwaka huu unaonyesha nguvu ya mkakati wetu na dhamira yetu thabiti ya kuwaunganisha Watanzania na kesho iliyo bora. Kupitia ubunifu na ushirikiano, tunaziba pengo la kidijitali na kifedha,” amesema Philip Besiimire, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania.

Katika miaka ya hivi karibuni Vodacom imekuwa ikibuni bidhaa na huduma pamoja na washirika wake ikiwemo M-Koba na M-Wekeza zinazoendelea kusaidia makundi mbalimbali nchini ikiwemo wanawake. 

Watumiaji M-Koba wafikia milioni 1.3 

Vodacom imesema kwa sasa M-Koba, jukwaa la kuweka akiba kwa vikundi, linalohudumia zaidi ya wateja milioni 1.3 na M-Wekeza, inayosaidia uwekezaji kupitia simu, ilivutia amana za takribani  Sh25 bilioni ndani ya miezi michache tangu kuzinduliwa kwake. 

“Jukwaa la malipo ya kidijitali “LIPA kwa simu” lilichakata zaidi ya Sh1 trilioni kila mwezi, huku mikopo ya muda mfupi na Songesha zikikopesha zaidi ya Sh3 trilioni zilizowasaidia wateja na wafanyabiashara kote nchini,” imesema taarifa hiyo ya Vodacom.  

Kampuni hiyo imesema inatazamia mazingira thabiti ya kisheria na itaendelea kuwekeza katika upanuzi wa mtandao, huduma bora kwa wateja na ujumuishwaji wa kidijitali. 

“Tunapoadhimisha miaka 25 ya kuleta mabadiliko chanya kwa maisha ya Watanzania, tunaendelea kujikita katika ukuaji endelevu na mabadiliko yanayoongozwa na dhamira yetu na matokeo yetu yanathibitisha imani ambayo wateja na wanahisa wetu wanayo kwetu,” amesema David Tarimo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom Tanzania PLC.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks