Katiba ya CCM kujadiliwa kupitia mkutano wa mtandaoni Julai 26
- Ajenda kuu ya mkutano huo ni marekebisho ya katiba ya chama.
Dar es salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kujadili kufanya marekebisho ya katiba ya chama hicho katika mkutano mkuu maalum wa Taifa unaotarajiwa kufanyika kwa njia ya mtandao Jumamosi, Julai 26, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 25, 2025 Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amesema wameamua kufanya mkutano huo mtandaoni kwa sababu katiba yao inaruhusu.
“Vikao vilivyoainishwa chini ya ibara ya 99 (1) a hadi f ya katiba hii, vinaweza kuendeshwa kwa njia ya mtandao endapo kuna ulazima wa kufanya hivyo,” amesema Makala akinukuu Katiba ya CCM,”

Habari za CCM kuitisha mkutano kwa njia ya mtandao zilianza kusambaa jana Julai 24, 2025 huku vyombo mbalimbali vya habari vikiripoti jambo lililozua mijadala mbalimbali kwa baina ya wanachama wa chama hicho na watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii wengi wao wakitaka kujua sababu za mkutano kuitishwa kwa njia ya mtandao na ajenda zinazotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo.
Mkutano huo unafanyika ikiwa zimesalia siku siku tatu kufikia Julai 28, 2025 ambapo kikao cha Kamati Kuu ya CCM kinatarajiwa kukaa kuamua majina ya watia nia wa ubunge na uwakilishi wasiozidi watatu kwa kila jimbo.
Ratiba mpya ya uteuzi wa wagombea hao kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu ilitangazwa Julai 22, 2025 ikifanyiwa marekebisho baada ya ratiba iliyotangazwa awali Julai 19, 2025 kusitishwa.
Kwa mujibu wa ratiba mpya iliyotangazwa mchakato wa uteuzi ndani ya chama hicho utaanza Julai 27 kwa kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa, kitakachofuatiwa na kikao cha Kamati Kuu ya CCM Julai 28.
Hata hivyo, pamoja na Makala kuanisha ajenda ya mkutano huo hajaweka wazi vipengele vinavyotarajiwa kufanyiwa marekebisho na kusisitiza kuwa taarifa zitawekwa bayana hapo kesho baada ya mkutano kufanyika.
“Kesho ndio mtajua marekebisho hayo madogo ya katiba ni marekebisho gani,” amesisitiza Makala.
Huenda vipengele vya kikatiba vitakavyoboreshwa katika mkutano huo vikaleta ahueni au maumivu kwa wanachama chama hicho tawala nchini Tanzania wakati ikisalia miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Latest



