CCM yavuna Sh2.7 bilioni makada wakichuana ubunge

July 3, 2025 5:38 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Kati ya watia nia hao 4,109 walioenda majimboni, wanawake ni 263  tu sawa na asilimia 6.4.
  • Wanachama 161 wajitokeza katika kinyang’anyiro cha ubunge wa viti maalum kupitia Umoja wa Vijana wa CCM.

Dar es Salaam. Hapana shaka mchuano wa kusaka ubunge ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) utakuwa mkali mwaka huu baada ya makada 5,475 kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo na kukisaidia chama hicho tawala kuingiza zaidi ya Sh2.7 bilioni ndani ya wiki moja. 

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema kuwa hadi zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu ndani ya CCM linakamilika Julai 2, 2025 wanachama 5,475 walichukua fomu za ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Kwa mujibu wa Makalla, gharama za fomu moja ya ubunge ilikuwa Sh500,000 wakati udiwani ilikuwa Sh50,000. 

Kwa hesabu za haraka, chama hicho kikongwe nchini kimeingiza si chini ya Sh2.74 bilioni kupitia ada za fomu. 

Makalla amewaambia waandishi wa habari leo Julai 3, 2025, Jijini Dar es salaam kuwa CCM ina hazina kubwa ya makada na wanachama wake wa makundi mbalimbali kutokana na mwitikio wa watu waliojitokeza kuchua fomu.

Makalla amebainisha kuwa watia nia 3,585 wamechukua fomu upande wa bara na 524 wamechukua upande wa Zanzibar. 

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla Makalla. Picha/CCM Tanzania.

Wanawake ‘kiduchu’ majimboni

Kati ya watia nia hao 4,109 walioenda majimboni kuwania ubunge na uwakilishi Zanzibar ni 263 sawa na asilimia 6.4. Hii ni sawa na kusema kwa kila watia nia 1,000, 64 tu ndo wanawake. 

“Upande wa Uwakilishi kule Zanzibar wamechukua fomu wanachama 503, Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) wao wamechukua 623 Bara na ndani yake wapo 91 wa Makundi maalum lakini kule Zanzibar wamechukua 8 na viti maalum uwakilishi 9 kwa hiyo jumla UWT waliojitokeza ni 640,” ameeleza Makalla.

Kwa upande wa Jumuiya ya Wazazi, Tanzania Bara imeshuhudia wanachama 55 kuchukua fomu, Zanzibar watatu, na wanne wamejitokeza kwa viti maalum, hivyo jumla kuwa 62. 

Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umejumuisha wanachama 161 wanaowania viti maalum vya ubunge. Kati ya vijana hao, 154 wanatoka Tanzania Bara na saba kutoka visiwani Zanzibar.

Hata wakati makada wa ubunge wakiwa roho juu kusubiri hatma yao, Makalla ameeleza kuwa bado wanachakata data za wanaowania nafasi ya udiwani huku takriban kata 3,960 zikiwa bado hazijakamilisha majumuisho. 

“Nafasi za udiwani bado wanaendelea kuchakata lakini wameniambia katika kata 3,960 tunaweza kuwa na wagombea zaidi ya elfu 15, kwa hiyo CCM tuna wanachama waliojitokeza katika nafasi za ubunge na udiwani kufikia elfu 20, ni idadi kubwa ya waliojitokeza kuliko wakati wowote,” amesema Makalla. 

Wajumbe kuanza kazi yao Julai 4

Mchujo wa wagombea ndani ya chama hicho utaanza rasmi Julai 4, 2025, kuanzia ngazi ya kata na kuendelea wilaya na mikoa ambapo majina ya wagombea watakaopigiwa kura yatachaguliwa. 

Sanjari la hayo, kamati za mkoa zitarasimisha uteuzi wa awali Julai 9, 2025 kabla ya uteuzi wa mwisho kufanywa na Kamati Kuu ya CCM.

Kuna idadi kubwa ya makada wa chama hicho waliojitokeza kuchukua fomu mbali ya wabunge wanaotetea nafasi zao wakiwemo waliokuwa wakuu wa mikoa kama Paul Makonda, maofisa wa Serikali, wasanii, wanahabari na wengineo lukuki.

Kujitokeza kwa wingi kwa wanachama hao kumezidi kuibua mjadala mtandao iwapo idadi hiyo inamaanisha hamasa ya kuwatumikia wananchi ama ni matamanio ya makada hao kuuaga umaskini kupitia nafasi hizo za kisiasa bungeni. 

Katibu huyo amewaomba wanachama na wafuasi wa CCM kuwa watulivu na kuheshimu mchakato wa mchujo, huku akisisitiza kuwa vikao vya kuchuja wagombea vitakuwa vya huru, haki hakutokuwa na ushawishi wowote.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV