BoT yashusha riba benki kuu robo ya tatu 2025
- Benki hiyo inatarajia kuwa mfumuko wa bei utaendelea kuwa ndani ya wigo wa asilimia 3 hadi 5 na utakuwa tulivu.
- Gavana asema majadiliano na mikataba inayoendelea kufanywa na Marekani na mataifa mengine kuhusu ushuru yanatarajia kupunguza athari kwenye uchumi.
Dar es Salaam. Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania imeshusha kiwango cha riba ya benki (CBR) kutoka asilimia 6.0 hadi asilimia 5.75 katika robo ya tatu ya mwaka 2025 kutokana na mwenendo mzuri wa kuimarika shughuli za kiuchumi na udhibiti wa mfumuko wa bei.
CBR ni kiwango cha riba kinachotumika na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufanya biashara na benki za biashara ambazo hutakiwa kutekeleza sera hiyo kwa kufuata msingi wa kuwa ndani ya wigo wa usiopungua au zidi asilimia 2.0 ya kiwango kilichopangwa.
Riba hiyo, iliyoanza kutumika Januari 2024, hutumiwa na BoT kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Hii ni mara ya kwanza kwa BoT kushusha riba hiyo tangu ilipopandisha kiwango hicho katika robo ya pili ya mwaka 2024. Wakati utaratibu mpya unaanza mwaka mmoja na nusu uliopita, kamati hiyo ya fedha ilipanga CBR kuwa asilimia 5.5% kwa robo ya Januari hadi Machi 2024. Hata hivyo, kiwango hicho kilipanda hadi asilimia 6 ambayo ilibakizwa na kamati hiyo kwa robo nne zaidi.
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amewaeleza wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa benki hiyo itatekeleza sera ya fedha ili kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki (7-day interbank rate) inabaki ndani ya wigo wa asilimia 3.75 hadi 7.75.
Uamuzi huo wa kushusha CBR ya robo ya Julai hadi Septemba 2025, amesema, unaakisi imani ya kamati hiyo katika mwenendo wa mfumuko wa bei ambao umeendelea kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3 hadi 5, na matarajio yanayoonesha kuendelea kuwa tulivu ndani ya wigo huo.
“Hali hii inatokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti, kuanza kwa msimu wa mavuno, pamoja na utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania,” amesema Tutuba.
Licha ya migogoro ya kisiasa duniani na ongezeko la ushuru wa bidhaa za forodha kuongeza sintofahamu kwenye mwenendo wa uchumi wa dunia, bosi huyo wa BoT amesema mazungumzo na makubaliano ya hivi karibuni yanaashiria hatari hizi zinaweza kupungua.
Uchumi wa ndani bado imara
Katika tathmini yake, kamati hiyo ya sera ya fedha inayoongozwa na Tutuba, imebaini kuwa mwenendo wa uchumi wa ndani umeendelea kuimarika kwa kasi ya kuridhisha, ukichochewa na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu na kuongezeka kwa shughuli za sekta binafsi, kutokana na kuimarika kwa mazingira ya ufanyaji biashara.
“Hatari za misukosuko ya nje kwenye matarajio ya mwenendo uchumi ni ndogo, kutokana na muundo wa uchumi wetu wenye kutegemea sekta mbalimbali za uzalishaji, pamoja na utekelezaji thabiti wa sera na programu zinazochochea ukuaji wa uchumi, zinazotarajiwa kusaidia kuhimili misukosuko hiyo,” amesema Tutuba.
Uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 6 mwaka 2025, kwa mujibu wa Wizara ya Fedha huku mfumuko wa bei ukitarajiwa kuwa ndani ya wigo wa asilimia 3 hadi 5.
Latest



