Wafanyabiashara wadogo kujumuishwa ukusanyaji wa maoni Mkumbi II
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema ili kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wadogo nchini itawashirikisha katika utayarishaji wa Mpango wa Pili wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II).
Mkumbi ni mpango wa Serikali unaolenga kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji kwa kupunguza vikwazo vya kiutaratibu, kuboresha mifumo ya kisera, na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kustawi.
Lengo kuu la Mkumbi ni kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa mahali rafiki kwa wafanyabiashara wa viwango vyote ikiwemo wafanyabiashara wadogo, wakubwa na wakati na kuwa kivutio kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Juni 6, 2025, amesema Serikali imechukua uamuzi huo naada ya kubaini malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu mazingira ya uendeshaji biashara, licha ya kazi kubwa iliyofanyika chini ya MKUMBI I.
Prof Mkumbo amesema Serikali iko tayari kupokea maoni na kuyatumia kuboresha zaidi katika mpango wa pili ambapo tayari kamati ya mpango huo imeshafanya uchambuzi wa mpango wa awali uliokuwa unatekelezwa tangu mwaka 2018.
Kwa sasa kamati hiyo kwa mujibu wa Prof Mkumbo inaingia katika hatua ya ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji ikiwalenga zaidi wafanyabiashara wadogo na wa kati ikiwemo wafanyabiashara wa chakula maarufu kama mama lishe.
“Tunakwenda kuonana na wadau wa biashara na uwekezaji kwenda kuzungumza nao kupata maoni yao, kupata mapendekezo yao kujua ni mambo yapi tunapaswa kuyazingatia ili biashara zilendelee kukua” ameeleza Profesa Mkumbi.
Aidha, kwa upande wake mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Faustine Kabuzora amesema kuwa mchakato huo unatarajiwa kuanza mnamo Juni 16, 2025 ukijumuisha mikoa 16.
Ukusanyaji wa maoni utaanzia katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro pamoja na Dodoma kisha kuelekezwa katika mikoa mingine.
“Biashara ndogondogo zinajumuisha watu wengi sana, kwaiyo na wenyewe tutawajumuisha kuwauliza ni jinsi gani wanadhani mazingira yao ya biashara yaboreshwe,” amesema Profesa Kabuzora.
Ushirikiswaji wa wafanyabiashara wadogo kwenye mpango huo unaweza kusaidia kutatua kero zao na uboreshwaji wa mazingira yao ya biashara kama kuwepo sera rafiki zinazolenga kupunguza urasimu, gharama zisizo za lazima, na kero zinazokwamisha biashara zao.
Pia, hatua hii inaweza kuchochea uanzishwaji wa huduma bora zaidi kama vile miundombinu ya masoko, maeneo rasmi ya kufanyia biashara, mikopo yenye masharti nafuu na mafunzo ya ujasiriamali.
Latest



