RISE: Mradi unaobadili maisha ya Watanzania vijijini kupitia barabara na madaraja

April 20, 2025 9:00 am · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link

Wakati mshale wa saa unazunguka saa 24 siku saba za wiki, haikuwa hivyo kwa mamilioni ya Watanzania wa vijijini kabla ya mwaka 2023, mvua ziliponyesha, mshale wao wa saa ulisimama. 

Akina mama walilazimika kuvuka mto wenye mafuriko wakibeba watoto wao mgongoni kwenda kliniki. Wakulima waliona mazao yao yakiozea mashambani, huku wanafunzi wakikosa masomo. 

Wakazi wa kijiji cha Itunya, Katavi wanasimulia kwamba wao mvua iliponyesha, na maisha yalisimama. Mto Ifume ulijaa kwa hasira, ukaziba njia zote. Watoto walibaki nyumbani, shule zilifungwa. 

Wagonjwa walilala kwenye vitanda vya maumivu, wakisubiri mto kupwa. Wakulima walisimama kwenye mashamba yao, wakitazama mazao yao yakiwa yanaharibika, wakijua kuwa soko lilikuwa mbali mno.

Kwa miaka mingi, hii ilikuwa desturi. Yani mvua inanyesha, maisha yanasimama.Lakini leo, simulizi hiyo imebadilika.

Mradi wa Rural Infrastructure Support for Economic Empowerment (RISE), unaotekelezwa na TARURA kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, haujengi barabara tu. Unajenga matumaini. 

Unafungua njia si tu za usafiri, bali za maisha. Leo, zaidi ya kilomita 500 za barabara na madaraja 30 yamejengwa; watoto wanakwenda shule, wakulima wanapeleka mazao sokoni, na akinamama wajawazito wanavuka mito kwa usalama.

Daraja la Ifume: Ukombozi kwa Katavi

Michael Lupasha, mzee wa miaka 67, anasimama kwenye daraja jipya la Ifume, akishika ukuta wake kwa fahari. “Tulikuwa wafungwa wa hali ya hewa,” anasema, akitazama mto uliopwa chini yake. “Mwaka 2019, tulipoteza majirani zetu wakati walipojaribu kuvuka. Wamama waliobeba watoto, wakulima waliobeba mazao, na watoto waliotaka kwenda shule, mto ulikuwa kigugumizi kwa maisha yetu.”

Lakini sasa, daraja hili la mita 40 limeondoa hofu. Watu wanaweza kuvuka kwa usalama, hata wakati wa mvua. “Watoto wetu wanaenda shule kwa wakati. Mahindi yetu yanafika sokoni kabla ya kuharibika. Hakuna tena maisha yanayosimama kwa sababu ya mto,” anasema Lupasha.

Simulizi hii si ya Itunya pekee. Inasikika kutoka Kalambo hadi Uvinza, kutoka Nzega hadi Igunga, na kutoka Mngazi hadi Lumbiji. 

Rukwa: Mto Kalambo Unavyorejesha Tumaini

Safari yetu inatupeleka Rukwa, ambapo daraja la Kalambo limeunganisha vijiji vya Mkowe, Mao, na Katapulo. Hivi ni vijiji vilivyokuwa vimejitenga kwa miaka 30. “Watoto wetu walikufa wakivuka mto,” anasema Diwani wa Mkowe, Alfred Mpandashalo. “Leo, wanavuka kwenda shule kwa salama.”

Alfred Mpandashalo, diwani wa kata, anakumbuka: “Kila msimu wa mvua, tulipoteza watu na mifugo. Mto ulikuwa kama mwenyeji mbaya, akituchukulia kila kitu.”

Joseph Chakupewa, mkulima wa mahindi na maharage, anasema kuwa daraja hili limebadilisha kila kitu. “Sasa hatuhitaji kungoja maji kupwa. Tunaweza kusafirisha mazao yetu sokoni kwa wakati, na bei zimeongezeka.” Shule ya Katapulo imeona idadi ya wanafunzi ikiongezeka kutoka 112 hadi 189 kwa muhula mmoja, uthibitisho kwamba daraja sio tu la mawe na saruji, bali pia la elimu na maendeleo.

Morogoro: Barabara ya lumbiji na mapinduzi ya kilimo

Huko Lumbiji, Morogoro, wakulima wa tangawizi walikuwa wakiuza mazao yao kwa bei ya chini kwa miaka mingi. “Walanguzi walituibia,” anasema Laurian Mkuchu, mkulima wa tangawizi. “Walijua hatuwezi kufika sokoni, kwa hivyo walituonea kwenye bei. Tuliuza kilo moja kwa shilingi 500 tu.” 

Barabara ya Ludewa-Lumbiji imetengeneza uchumi mpya. Hii ni barabara ya kilometa 21.6 ambayo imefungua milango ya fursa. Bei ya tangawizi imepanda kutoka TZS 500 hadi TZS 3,000 kwa kilo. 

“Kampuni ya Korea sasa inatuma malori kila wiki kununua bidhaa zetu moja kwa moja,” anasema Mkuchu kwa furaha. Vijana wengi wamerudi kutoka Dar es Salaam, wakianzisha mashamba kwa sababu ya barabara hii. Kimsingi ni vijana 23 wamerudi kutoka Dar es Salaam kuanza kilimo.

Kigoma: Daraja la Msombwezi linavyopunguza umasikini

Wilayani Uvinza, Kigoma, daraja la Msombwezi limeondoa mateso kwa wakazi wa vijiji vya Sunuka na Msimbazi. Edward Telekwa anaeleza: “Kabla ya daraja, ilichukua saa mbili kufika hospitali. Sasa, tunafika kwa saa moja tu.”

Amani Mavumbi, mwanakijiji, anaongeza: “Sisi wakulima tulikuwa tunapoteza mazao yetu kila msimu wa mvua. Sasa, tunaweza kusafirisha bila shida.”

Idadi ya watoto wanaohudhuria shule imeongezeka hadi asilimia 92 katika baadhi ya maeneo huku vifo vya wajawazito vikipungua kwa asilima 22% katika maeneo yaliyopata madaraja. Picha l Annastazia Rugaba

Chato: Barabara ya Mulanda-Imweru na ukombozi wa elimu

Katika wilaya ya Chato, Geita, barabara ya Mulanda-Imweru ilikuwa njia ya mateso. Semeni Marko, mzee wa kijiji cha Buseresere, anasema: “Watoto wetu walikosa shule, wagonjwa hawakuweza kufika hospitali. Lakini sasa, barabara hii imetupa mkombozi.”

Ernest Nyanda, Meneja wa TARURA Chato, anasisitiza: “Tulichagua kufanyia kazi barabara hii kwa sababu ni muhimu kwa elimu, afya, na biashara.”

Kule Igunga, daraja la Igunga Gorge linawekwa kwa mikono ya mafundi waliolala site kwa wiki, wakijua kuwa kila jiwe linamaanisha maisha yaliyookolewa. “Hii si miundombinu tu,” anasema Mhandisi Stewi Emmanuel wa TARURA. “Ni fidia kwa muda uliopotea wa kizazi kizima.”

Katika maeneo ya Uvinza, Nzega, na Kibondo, akinamama hawazai tena kwenye kingo za mito. Maji hayawazuii tena wanafunzi kwenda shule. Barabara ya Songambele-Banyibanyi imewawezesha wakulima wa mahindi kufikia masoko kabla ya mazao kuharibika.

Na kule Chato, mtoto Neema mwenye umri wa miaka 12 sasa anarudi nyumbani kutoka shule na vitabu vyake vikiwa vikavu. “Zamani tulivuka maji ya hadi kiunoni,” anakumbuka. “Leo tunapanda basi.”

Hadithi hizi zote zinaambatana na namba ambazo zingeweza kuonekana kama takwimu tu ikiwemo kuzalishwa kwa aidi ya ajira 40,000 ambapo gharama za usafirishaji zimepungua kwa asilimia 40 mpaka 60.

Uhudhuriaji wa wanafunzi umeongezeka kwa 92% katika baadhi ya maeneo huku wakulima 87,000 wakipata masoko mapya.

Idadi ya watoto wanaohudhuria shule imeongezeka hadi asilimia 92 katika baadhi ya maeneo huku vifo vya wajawazito vikipungua kwa asilima 22% katika maeneo yaliyopata madaraja.

Wakati huo huo bei ya mazao kama tangawizi na nyanya imepanda mara tano huko Lumbiji.

Lakini nyuma ya kila namba kuna mtu, familia, kijiji kizima kilichoibuka kutoka kwenye kizuizi cha kijiografia hadi fursa ya kiuchumi.

Mama Caroline Chambala wa Katavi anasema: “Sijali tena mvua. Ninaweza kumpeleka mtoto wangu kliniki kwa wakati.” Khamis Shadrack, mkulima wa pamba huko Bukombe, anaongeza: “Kabla ya daraja, nililipa shilingi 20,000 kwa siku kusafirisha mazao yangu kwa mtumbwi. Sasa, malori yanafika shambani kwangu!”

Mipango ya kesho Tanzania inayosonga mbele

Kazi haijakwisha. TARURA ina mpango wa kupanua miradi hii hadi katika wilaya 12 zaidi zenye mafuriko kufikia 2026. Mipango hiyo inajumuisha, barabara zenye nishati ya jua, kufundisha vijana ujenzi wa madaraja pamoja na kuongeza barabara za lami kwenye njia zenye msongamano mkubwa.

Kama alivyosema Waziri wa Kazi na Uchukuzi: “Madaraja haya ni makumbusho yetu ya taifa. Baada ya miaka mingi, watoto wataonnesha na kusema: Hapa ndipo Tanzania ilipobadilika.”

Miundombinu siyo tu mawe, bali ni tumaini

Mradi wa RISE sio tu kuhusu ujenzi wa barabara na madaraja. Ni kuhusu kurejesha heshima, kuwapa wananchi fursa, na kuwawezesha kuwa sehemu ya maendeleo ya nchi. 

Kama alivyosema Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Seif M. Seif: “Madaraja haya si tu mawe na saruji, ni njia za utu, heshima, fursa, na maisha bora kwa kila Mtanzania.” 

Aliongeza kwamba: “Barabara hizi si zege tu, ni kiapo. Kwamba hakuna mtoto mwingine atakayekosa mtihani kwa sababu ya mvua. Hakuna mama atakayejifungua kwenye kingo za mto kwa kukosa daraja. 

Hakuna mzigo wa mahindi utakaoozea shambani kwa sababu ya korongo lisilopitika. Hii si hesabu ya saruji pekee. Ni hesabu ya utu. Daraja moja  limeokoa uhai wa watu wengi ndani ya msimu. Kilomita moja ya barabara  ni sawa na biashara 47 mpya ndani ya miezi 18.”

Katika kuelekea Dira ya Taifa 2050, miradi kama RISE inafanya ndoto kuwa kweli. Miundombinu ya vijijini imekuwa chanzo cha mapinduzi ya kijamii na kiuchumi, ambapo wanawake wa Lumbiji wanajiunga katika vikundi vya matengenezo kwa kutumia WhatsApp kuripoti uharibifu. Ambapo daraja la Mnekezi lina misingi inayostahimili tembo wanaotaka kuvuka na taa za usalama kwa wamama wanaosafiri kabla ya alfajiri.

Kumbe wakati mwingine maendeleo huja polepole kama jiwe juu ya jiwe. Lakini sasa tumeona mwendo wa haraka. Kuanzia Kigoma hadi Mbulu, kutoka Arumeru hadi Bahi, kutoka Mvomero hadi Longido, nchi inajifungua upya.

Tanzania ya 2050 inachorwa leo kwa matofali ya mawe, kwa barabara zenye lami, kwa daraja linalounganisha si tu kingo mbili za mto, bali ndoto mbili za kizazi. Kama alivyoeleza Mhandisi Seif M. Seif wa TARURA: “Tuliposikia maombi ya wanavijiji, hatukwenda na PowerPoint, tulikaa chini ya mibuyu tukawasikiliza na kutekeleza”

Hii ndiyo Tanzania mpya, Tanzania inayojengwa kwa ushirikiano wa kisiasa, ubunifu wa wahandisi, na nguvu za wananchi.

Na katika kila daraja jipya, kuna ahadi isiyoandikwa: Kwamba maendeleo hayatakuwa tena ya mijini tu. Kwamba kila kijiji, kila mama, kila mwanafunzi, ana nafasi sawa ya kufanikiwa

Habari hii imeandikwa na Annastazia Rugaba ambaye ni Mkurugenzi wa Utetezi na Ushirikishwaji katika Twaweza Afrika Mashariki. Yeye ni mtaalamu wa mawasiliano ya maendeleo na anaweza kupatikana kupitia namba 0687222197 au barua pepe annarugaba@gmail.com

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW