Tanzania kujibu mapigo Malawi, Afrika Kusini kuzuia mazao kuingia nchini kwao

April 17, 2025 9:54 am · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali yasema itazuia mazao yote ya kilimo na bidhaa zote ambazo ni za kilimo kutoka South Africa na Malawi.
  • Mazao hayo ni pamoja na unga, mahindi, mchele, tangawizi, ndizi.

Dar es Salaam. Tanzania inakusudia kuzuia mazao kutoka nchi za Malawi na Afrika Kusini kuingia nchini pamoja na kuzuia magari yanayosafirisha mazao ya nchi hizo kwenda nchi nyingine kutokana na nchi hizo kuchukua hatua hiyo dhidi ya mazao ya Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Kilimo Tanzania Hussein Bashe aliyoitoa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram imebainisha kuwa amemepokea taarifa kuwa Nchi ya Malawi imezuia mazao mbali mbali kuingia nchini kwao.

Mazao hayo ni pamoja na unga, mahindi, mchele, tangawizi, ndizi, na jambo lililosababisha wafanyabiashara Kitanzania kukwama kuingiza mizigo katika nchi ya Malawi.

Bashe ameongeza kuwa kwa kipindi cha miaka mitano, Serikali imekua ikifianya jitihada za kufungua soko la ndizi Afrika Kusini bila mafanikio akikumbusha kuwa ilichukua miaka 10 kupata soko la parachichi nchini humo baada ya kutishia kuzuia mazao ya nchi hiyo kuingia Tanzania.

“Ningependa kuwafahamisha tunaendelea na jitihada za kufanya mawasiliano na Serikali za South Africa(Afrika Kusini) na Malawi kwa mara ya mwisho, hadi kufikia Jumatano ijayo, kama watakua hawajaruhusu wafanyabiashara wa Tanzania na mazao yetu kuingia; Wizara ya Kilimo itazuia mazao yote  ya kilimo na bidhaa zote ambazo ni za kilimo kutoka South Africa na Malawi,” inasomeka taarifa ya Bashe.

Waziri huyo wa Kilimo amesema nchi haitutaruhusu zao lolote kutoka nchi hizo kupita ndani ya nchi yetu kwenda bandari ya Dar es Salaam au nchi nyingine yoyote hatua iliyochukuliwa mwaka 2024 mpaka mataifa hayo walipofungulia mazao ya Tanzania kwenda nchini mwao.

“Na pia kwakua tumekua tukiwauzia mbolea, tutazuia mbolea kwenda Malawi, kwahiyo natoa notisi hii kama kuna wafanyabiashara wa Kitanzania wana mizigo ya kwenda Malawi, kuanzia wiki ijayo kama watakua hawajabadilisha msimamo, wasipakie chochote,” amesisitza Bashe.

Hata hivyo, Notisi hiyo  itaanza kutekelezwa kuanzia Jumatano wiki ijayo ikiwa Serikali haitapata mrejesho chanya kutoka mataifa hayo mawili ambapo Bashe amesema jitihada zake za kuwasiliana na Waziri wa Kilimo wa Malawi hazijazaa matunda yoyote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks