Dk Nchimbi aikosoa “No reform no election” asema hakuna wa kuzuia uchaguzi
- Asema Chadema wakisusia uchaguzi wasilazimishwe.
- Awatoa hofu Watanzania, uchaguzi utafanyika.
Arusha. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk Emmanuel Nchimbi amekosoa kampeni ya ‘No reform no election’ inayoendeshwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akibainisha kuwa hakuna kiongozi mwenye mamlaka ya kuzuia uchaguzi Mkuu.
Kampeni hiyo ya ‘No reform no election’ (hakuna uchaguzi bila mabadiliko) ilianza kupata umaarufu mwanzoni mwa mwaka huu baada ya kupitishwa na Kamati Kuu ya Chadema Disemba, 2024 ikihamasisha Serikali kufanya mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Rais, Madiwani na Wabunge Oktoba mwaka huu.
Dk Nchimbi aliyekuwa akizungumza katika mkutano mkuu wa Jukwaa la Wahariri (TEF) leo Aprili 4, 2025 mkoani Songea amesema kuwa hakuna kiongozi yoyote yule ikiwemo Rais aliyepo madarakani anayeweza kuzuia uchaguzi huo usifanyike.
“Inapofika mwaka wa uchaguzi hakuna raia yoyote anayeweza kusema uchaguzi usifanyike hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hata Makamu wa wa Rais hata Waziri Mkuu hawezi kulitamkia Taifa kwamba uchaguzi usifanyike kwa sababu hili ni takwa la kikatiba…
…Nataka niwahakikishie Watanzania kuwa uchaguzi wa Rais, madiwani na Wabunge 2025 utafanyika,” amesema Nchimbi.
Kauli hiyo ya Nchimbi inajibu hoja za Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu ambaye kwa nyakati tofauti alifafanua maana ya kampeni hiyo kuwa “hawasusia uchaguzi bali watazuia uchaguzi”.

Dk Emmanuel Nchimbi akipokea zawadi kutoka kwa Jukwaa la Wahariri (TEF) alipohudhuria mkutano mkuu wa jukwaa hilo leo Aprili 4, 2025.Picha TEF/X
Lissu alisisitiza tena kuhusu kampeni hiyo Machi 2, 2025 katika mkutano wa TEF uliofanyika makao makuu ya chama hicho huku akiwataka wananchi kuiunga mkono.
“Hatujarembaremba hapo, tutawaalika Watanzania kuungana nasi kupinga mabadiliko hayo.” alisema Lissu.
Pamoja na hayo, Nchimbi amesema hakuna ulazima wa chama hicho kushiriki uchaguzi mkuu ikiwa hawataki kushiriki basi wana CCM na wanasiasa wengine wasiwalazimishe.
“Zimeanza kusikika sauti za baadhi ya wana CCM na wananchi wakishinikiza Chadema iingie kwenye uchaguzi. Lakini ukweli ni kwamba ni haki yao kususia. Mtu yeyote asiwalazimishe Chadema kuingia katika uchaguzi,” amesema Nchimbi.
Aidha, Nchimbi ametumia jukwaa hilo kuwafunda wahariri kupuuzia baadhi ya kauli sizizofaa za wanasiasa zinazoweza kuchochea chuki na migongano katika jamiii huku akiwataka kuendelea kuwa chanzo cha amani na utulivu katika kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Latest



