Dar kuanza zoezi la kuboresha daftari la kudumu la kupiga kura Machi 17

March 5, 2025 8:04 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Litafanyika kwa siku saba na kutamatika Machi 23, 2025.
  • Dar es Salaam yatarajiwa kuwa na wapiga kura  milioni 4 watakaojiandikisha.

Arusha. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imebainisha kuwa  zoezi la kuboresha daftari la kudumu la kupiga kura katika mkoa wa Dar es salaam litafanyika kwa kwa siku saba kuazia Machi 17 hadi 23 mwaka huu.

Zoezi hilo litafanyika katika jiji la Dar es Salaam baada ya kukamilika katika mikoa mingine 28 Tanzania Bara na Zanzibar ikiwa ni maandalizi muhimu ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2025.

Jaji Jacobs Mwambegele, Mwenyekiti wa tume hiyo, aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Machi 5, 2025 amesema zoezi hilo litaanza saa mbili asubuhi na kufungwa saa10 jioni huku wazee na wajawazito wakipewa kipaumbele.

“Tumeshaelekeza vituo vyote wajawazito, wazee na wanawake watakaokuja na watoto katika kipindi cha kufanya maboresho daftari la kudumu la kupiga kura watapewa kipaumbele,” amesema Mwambelege.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufaani Jacobs Mwambegele (kulia) akiangalia namna mwendesha kifaa cha Biyometriki (BVR) anavyochukua picha wakati alipotembelea kituo cha Mafiga B Manispaa ya Morogoro mkoani Morogoro kuangalia zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililoanza mkoani humo Machi mosi na litafikia ukomo Machi 07, 2025. Picha| INEC.

Kwa upande wake Ramadhani Kailima, Mkurugenzi wa tume hiyo amesema kwa mkoa wa Dar es Salaam wanatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 643,420 wenye sifa ikiwa ni ongezeko la asilimia  18.7 kulinganisha na idadi waliyojiandikisha mwaka 2019/2020.

“Hivyo kama makisio yetu yakienda sawa daftari la mkoa wa  Dar es Salaam litakuwa na jumla ya wapiga kura 4,078,337 katika uchaguzi ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani,” amesema Kailima.

Hata hivyo, Kailima amesema kuwa Idadi hiyo inaweza kuongezeka au kupungua ikiwa kuna watu waliokidhi vigezo mwaka 2020 na hawakujiandikisha watajiandikisha.

Mpaka kukamilika kwa zoezi hilo la kuboresha daftari la kupiga kura INEC imesema inatarajia wapiga kura milioni 34.7 wataboresha taarifa zao huku wengine 594,494 wakitarajia kuondolewa katika daftari hilo kutokana na sababu mbalimbali na kuongeza jumla ya idadi ya wapiga kura wote nchini.

Pamoja na hayo tume hiyo imesema  itaweka utaratibu maalum kwa vyama vya siasa kuweka wawakilishi katika kila kituo ili kuhakikisha idadi ya wapiga kura watakaokuja kuhakiki taarifa zao au kujiandikisha huku ikikemea fujo na kuingilia shughuli za tume.

“Mawakala au viongozi wa vyama vya siasa hawaruhusiowi kuingilia mchakato wa uboreshaji wa daftari la kupiga kura kituoni hivyo niwaombe viongozi wa vyama vya siasa kuzingatia sheria ya uchaguzi na kanuni za uboreshaji,” amesema Mwambelege.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks