Maumivu: Bei ya petroli, dizeli ikiendelea kupaa Tanzania

March 5, 2025 11:47 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yapaa mara ya pili mfululizo ndanu ya mwaka 2024
  • Petroli imepaa kwa Sh176, dizeli Sh182.

Arusha. Bei ya petroli na dizeli zimeendelea kupanda kwa miezi miwili mfululizo nchini Tanzania, jambo ambalo huenda likawaumiza vichwa wamiliki wa vyombo vya moto wanaotumia nishati hizo katika shughuli mbalimbali.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (Ewura) leo Machi 5, 2025 inabainisha kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Dar es Salaam imepaa kwa Sh176 huku dizeli ikipanda kwa Sh182.

Kwa kiwango hicho, watumiaji wa mafuta kupitia bandari ya Dar es Salaam watanunua lita moja ya petroli kwa Sh2,996, dizeli kwa Sh2,885 na mafuta ya taa Sh3,036.

Kwa mujibu wa Ewura bei hiyo imepaa kwa mara ya pili mfululizo kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli na mafuta ya taa huku gharama hizo zikishuka kwa mafuta ya dizeli.

“Bei za mafuta katika soko la dunia zimeongezeka kwa asilimia 1.44 na asilimia 5.87 kwa mafuta ya petroli na mafuta ya taa mtawalia na

zimepungua kwa asilimia 1.02 kwa mafuta ya dizeli,”  imesema taarifa ya Ewura.

Ewura imefafanua kuwa kwa mwezi Machi 2025, gharama za uagizaji mafuta (premiums) zimepungua kwa wastani wa asilimia 0.51 kwa mafuta ya petroli, asilimia 1.91 kwa mafuta ya taa na zimeongezeka kwa asilimia 24.42 kwa mafuta ya dizeli katika bandari ya Dar es Salaam.

Katika bandari ya Tanga gharama zimepungua kwa wastani wa asilimia 2.60 kwa mafuta ya petroli na dizeli na katika bandari ya Mtwara hakuna mabadiliko.

Kwa upande wa mafuta yanayoingia kwa bandari ya Tanga Petroli inauzwa kwa 3,042, dizeli Sh2,932 na mafuta Sh3,082 huku mkoani Mtwara wakinunua petroli kwa Sh3,069 na  dizeli kwa Sh2,958.

Kyerwa maumivu zaidi

Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera ndiyo inayonunua mafuta hayo kwa bei ya juu zaidi mwezi Machi kulinganisha mikoa mingine nchini ambapo lita moja ya Petroli inauzwa kwa Sh3234 kutoka 3,058 iliyorekodiwa mwezi Februari huku dizeli ikuzwa kwa Sh3,123 kutoka Sh2,941.

Wakati wakazi wa wilaya hiyo mkoani Kagera wakiugulia maumivu ya kununua mafuta hayo kwa bei ya juu, Ewura inabainisha kuwa mkoa wa Dar es Salaam ndiyo unaonunua mafuta hayo kwa bei ndogo zaidi kulinganisha mikoa mingine. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks