Fahamu vigezo na sifa za kujiandikisha JWTZ

May 2, 2025 3:46 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na wataalamu wa taaluma adimu na fani mbalimbali zikiwemo tiba na uhandisi.

Dar es salaam. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi za kuandikishwa kwenye jeshi hilo kwa vijana wa Kitanzania wenye  kuanzia elimu ya sekondari hadi elimu ya juu ambao utahusisha pia vijana wa Kitanzania wenye taaluma adimu.

Taarifa ya JWTZ iliyotolewa na  Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa jeshi hilo Kanali Gaudentius Gervas Ilonda imebainisha kuwa wataalamu hao wataandikishwa jeshini na watapatiwa mafunzo ya kijeshi pamoja na mafunzo ya kuwaendeleza kitaaluma kulingana na fani zao.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, sifa kuu zinazotakiwa kwa mwombaji ni pamoja na kuwa raia wa Tanzania mwenye kitambulisho cha Taifa, afya njema na akili timamu, pamoja na tabia na nidhamu nzuri isiyo na doa la makosa ya jinai. 

Muombaji pia anatakiwa awe na vyeti halisi vya kuzaliwa, vya elimu ya shule na taaluma, na awe hajatumikia vyombo vya ulinzi kama Polisi, Magereza, Kikosi cha Kuzuia Magendo au Chuo cha Mafunzo. Pia anatakiwa awe amehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mkataba wa kujitolea au mujibu wa sheria.

Wataalamu hao wataandikishwa jeshini na watapatiwa mafunzo ya kijeshi pamoja na mafunzo ya kuwaendeleza kitaaluma kulingana na fani zao. Picha | JWTZ.

Kwa vijana wenye elimu ya kidato cha nne na sita, umri usizidi miaka 24. Wenye stashahada umri uwe chini ya miaka 26, shahada ya kwanza miaka 27, na kwa madaktari bingwa wa binadamu umri uwe chini ya miaka 35.

Taaluma adimu zinazohitajika na JWTZ, zimo fani mbalimbali zikiwemo tiba na uhandisi. 

Kwa upande wa tiba, JWTZ linahitaji madaktari bingwa wa upasuaji wa jumla, mifupa, mkojo, mionzi, masikio-pua-koo, usingizi, magonjwa ya ndani, macho, watoto, wanawake na uzazi, saratani, uchunguzi wa vinasaba, magonjwa ya akili, dharura na magonjwa ya damu. 

Pia wanahitajika madaktari wa kawaida, madaktari wa meno, madaktari wa mifugo, wahandisi wa vifaa tiba, mafundi wa maabara ya meno, wataalamu wa mionzi, macho, mazoezi ya viungo (physiotherapy), na madaktari wa anga.

Kwa upande wa uhandisi, fani zinazohitajika ni pamoja na uhandisi wa umeme, mitambo, baharini, usafirishaji na sayansi ya usafiri wa majini, injini za dizeli baharini, usimamizi wa anga, uchunguzi wa ajali za ndege, hali ya hewa, usimamizi wa safari za ndege na uhandisi wa anga. 

Aidha, JWTZ linahitaji mafundi mchundo waliobobea kwenye uchomeleaji wa aluminiumu pamoja na uchomeleaji na utengenezaji wa vyuma.

Taaluma adimu zinazohitajika na JWTZ, zimo fani mbalimbali zikiwemo tiba na uhandisi. Picha | JWTZ.

Maombi yote yatakayowasilishwa yanatakiwa yaandikwe kwa mkono na kuwasilishwa kuanzia tarehe 1 Mei hadi 14 Mei 2025 katika Makao Makuu ya Jeshi jijini Dodoma. 

Waombaji wanatakiwa kuambatanisha nakala ya kitambulisho cha taifa au nambari ya NIDA, cheti cha kuzaliwa, vyeti vya shule na taaluma, cheti cha JKT kwa waliomaliza mkataba wa mafunzo, pamoja na namba ya simu ya mkononi. 

Maombi hayo yatatumwa kwa anuani ya Mkuu wa Utumishi Jeshini, Makao Makuu ya Jeshi, Sanduku la Posta 194, Dodoma.

Tangazo hili ni fursa kwa vijana waliohitimu katika taaluma mbalimbali kwa kuwa inafungua ukurasa mpya kwa vijana wa kitanzania kutumikia Taifa lao. 

Kwa wataalamu pia, hii ni nafasi ya kipekee ya kuitumikia nchi yao wakitumia taaluma zao kwa manufaa ya Taifa. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks